Jukwaa la GreenAccord 2026:kuanzia mifumo ya chakula,habari hadi Ikolojia ya kiroho!
Marina Tomarro na Francesca Merlo - Treviso, Italia.
Jukwaa la XVII la Kimataifa la Taarifa kwa Ajili ya Ulinzi wa Mazingira, lililoandaliwa na GreenAccord,yaani Mkataba wa Kijani lilifunguliwa alasiri ya tarehe 18 Machi 2026 huko Treviso, Kaskazini mwa Italia, na litaendelea hadi Jumamosi tarehe 21 Machi. Kwa kuwaleta pamoja zaidi ya waandishi wa habari 100 kutoka zaidi ya nchi 40, pamoja na wawakilishi wa taasisi, wasimamizi wa umma, biashara, wasomi, na wanachama wa sekta ya utamaduni, jukwaa hili linaunda nafasi ya mazungumzo ya kimataifa kuhusu changamoto za mazingira na kijamii.
Kaulimbiu ya mwaka huu 2026 ni, "Kujenga Mustakabali Pamoja - Ubinadamu mpya wenye kiu ya mustakabali," inaweka hali ya majadiliano, ambayo yamepangwa kuzunguka kikao cha ufunguzi na vikao sita vya mada. Mada muhimu ni pamoja na ikolojia fungamani, ushirikiano kati ya Ulaya na Marekani, teknolojia safi, mustakabali wa maeneo ya milimani, uendelevu wa matukio makubwa, na uwajibikaji wa vyombo vya habari vya kimataifa katika ulimwengu uliogawanyika unaoakisiwa na ukosefu wa usawa.
Kabla ya ufunguzi: wito wa matumaini na uwajibikaji
Kabla ya ufunguzi rasmi, Alfonso Cauteruccio, Rais wa ‘GreenAccord,’ ambacho ni chama cha kiutamaduni kisicho cha faida, kilichoongozwa na Ukristo, kilichoanzishwa ili kuhimiza kujitolea kwa wanaume na wanawake wote wa imani zote na madhehebu ya kidini kwa ajili ya ulinzi wa asili”alizungumza na Marina Tomarro mwandishi wa Vatican News, akielezea nia iliyo nyuma ya jukwaa la mwaka huu.
"Tunakabiliwa na mandhari ya kimataifa ambayo huibua wasiwasi na mara nyingi hufanya mustakabali uonekane usio na uhakika," alisema. "Badala yake, tunataka kuzungumza kuhusu ubinadamu unaotaka kujirekebisha, kuchukua hatua madhubuti, na zaidi ya yote kutazama mustakabali kwa matumaini." Pia alizungumzia hisia inayoongezeka ya wasiwasi wa kimazingira, hasa miongoni mwa vizazi vichanga, akielezea kama hofu ya jinsi hali ya mazingira inaweza kuwa mbaya zaidi katika miaka ijayo. Jukwaa hilo, alielezea, linalenga kujibu wasiwasi huu kwa kuhimiza mazungumzo yenye taarifa na ushiriki wa vitendo.
Kuanzia mifumo ya chakula hadi"ikolojia ya kiroho"
Katika siku zijazo, jukwaa litachunguza mada mbalimbali: kilimo endelevu, mifumo ya chakula, urejeshaji wa mijini, usanifu wa kibiolojia, uchumi wa ustawi, na uvumbuzi wa kidijitali. Umakini maalum utapewa hasa juu ya mnyororo wa usambazaji wa chakula, ikiwa ni pamoja na michango kutoka kwa wapishi walio na nyota ya Michelin kuhusu jinsi ya kupunguza upotevu na kukuza mazoea endelevu zaidi. Sambamba na mada hizi, programu pia inajumuisha tafakari juu ya kile ambacho waandaaji wanachokielezea kama "ikolojia ya akili na kiroho," inayohusishwa na maadhimisho ya miaka 800 ya Wimbo Sifa kwa Viumbe ulioandikwa na Mtakatifu Francis wa Assisi karibu 1225, mwaka mmoja kabla ya kifo chake mwaka 1226. Ujumbe ulioandaliwa na Kardinali Pietro Parolin utasomwa wakati wa jukwaa, ambao utasomwa na Kardinali Beniamino Stella, Mwanadiplomasia na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Makleri(2013-2021) na Askofu Mkuu wa Porto-Santa Rufina
Jukumu la vyombo vya habari katika ulimwengu uliogawanyika
Lengo lingine kuu la jukwaa ni jukumu la waandishi wa habari katika kushughulikia masuala ya mazingira kwa usahihi. "Leo tunazungumzia mengi kuhusu ikolojia jumuishi," Cauteruccio alibainisha, "lakini pia ni rahisi kukutana na kile kinachoitwa habari za kugushi." Kwa sababu hii, sehemu ya majadiliano itahusisha waandishi wa habari kutoka sehemu tofauti za dunia, wakichunguza jinsi taarifa potofu zinavyoweza kushughulikiwa kupitia utafiti na kuripoti kwa uwajibikaji. Alisisitiza hitaji la kuwasaidia waandishi wa habari katika kazi zao, kuhakikisha wanapata data na taarifa za kuaminika. "Kazi yao ni ya thamani," alisema, "na wanahitaji kuungwa mkono na wale ambao wanaweza kutoa taarifa sahihi ili kuwapa wasomaji na hadhira."
Mazungumzo katika sekta zote
Jukwaa hilo pia linajumuisha nafasi ya mazungumzo kati ya biashara, hasa kupitia kubadilishana kati ya makampuni ya Italia na Marekani yanayohusika katika uzalishaji endelevu. Kwa kuunganisha sekta na mitazamo tofauti, mpango huo unalenga kukuza ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja katika kukabiliana na changamoto za mazingira, kuchanganya uvumbuzi wa kiteknolojia, tafakari ya kiutamaduni, na taarifa sahihi kama vipengele muhimu katika kuunda hatua za baadaye.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.