Tafuta

Siku ya Uelewa wa Saratani Ulimwenguni. Siku ya Uelewa wa Saratani Ulimwenguni.  (ANSA)

WHO,Siku ya Saratani Duniani:40% ya wagonjwa wa satani ulimwenguni yanaweza kuzuilika

Katika ripoti mpya iliyotolewa tarehe 3 Februari 2026 mjini Geneva na Lyon,kuhusu uchambuzi wa kwanza wa aina yake umebaini kuwa asilimia 37 ya magonjwa yote mapya ya saratani ambayo ni sawa na wagonjwa milioni 7.1 yamehusishwa na sababu zinazoweza kudhibitiwa,ambazo zimetajwa kuwa ni pamoja na matumizi ya tumbaku, pombe,uzito uliopitiliza na kwa mara ya kwanza,maambukizi tisa yanayosababisha saratani yamejumuishwa.Ni katika siku ya Uelewa wa Saratani Duniani,Februari 4.

Na Angella Rwezaula - Vatican

Katika kuelekea Siku ya Saratani Duniani inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 4 Februari ya  kila mwaka, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la Utafiti Kuhusu Saratani (IARC) walibainisha kuwa hadi visa vinne kati ya kumi vya saratani duniani vinaweza kuzuilika kupitia mabadiliko ya mfumo wa maisha na mazingira. Haya yalionekana katika ripoti yao mpya iliyotolewa  tarehe 3 Februari  2026 mjini Geneva na Lyon, uchambuzi huo wa kwanza wa aina yake ulibaini kuwa asilimia 37 ya magonjwa yote mapya ya saratani ambayo ni sawa na wagonjwa milioni 7.1 yamehusishwa na sababu zinazoweza kudhibitiwa, ambazo zimetajwa kuwa ni pamoja na matumizi ya tumbaku, pombe, uzito uliopitiliza, na kwa mara ya kwanza, maambukizi tisa yanayosababisha saratani yamejumuishwa. Utafiti huo uliotumia takwimu kutoka nchi 185 umeitaja tumbaku kama chanzo kikuu kinachosababisha asilimia 15 ya magonjwa yote mapya, ikifuatiwa na maambukizi asilimia 10 na unywaji wa pombe asilimia 3. Saratani za mapafu, tumbo, na mlango wa uzazi zimechangia karibu nusu ya visa vyote vinavyoweza kuzuilika duniani kote.

Alama ya Uelewa wa Saratani
Alama ya Uelewa wa Saratani

Umuhimu wa takwimu 

Naye Dk. Ilbawi, Kiongozi wa Timu ya WHO ya Kudhibiti Saratani, alisisitiza umuhimu wa takwimu hizi akisema “Huu ni uchambuzi wa kwanza wa kimataifa kuonesha ni kiasi gani cha hatari ya saratani hutokana na sababu tunazoweza kuzizuia.” Mzigo wa saratani zinazoweza kuzuilika umeonekana kuwa mkubwa zaidi kwa wanaume ambapo ni asilimia 45 ikilinganishwa na wanawake asilimia 30, huku uvutaji wa sigara ukiwa sababu kuu kwa wanaume. Katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, mzigo huo kwa wanawake umefikia asilimia 38, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko maeneo mengine kutokana na maambukizi kama virusi vya Saratani ya shingo ya Kizazi (HPV).

Chanzo kinachozuilika ni muhimu

Kwa upande wa Dk  Isabelle Soerjomataram kutoka IARC alibainisha kuwa “Kushughulikia sababu hizi zinazozuilika ni moja ya fursa zenye nguvu zaidi ya kupunguza mzigo wa saratani duniani.” Ili kukabiliana na hali hii, WHO imehimiza nchi kuimarisha hatua za udhibiti wa tumbaku, kanuni za pombe, na kutoa chanjo dhidi ya maambukizi yanayosababisha saratani kama vile HPV na Homa ya Ini B (Hepatitis B). Pia, uboreshaji wa ubora wa hewa na kuweka mazingira salama ya kazi kumetajwa kama nyenzo muhimu. Hatua hizi jumuishi zimekuwa zikilenga si tu kupunguza idadi ya wagonjwa, bali pia kupunguza gharama za matibabu za muda mrefu na kuboresha ustawi wa jamii.

Siku ya Saratani

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here

04 Februari 2026, 11:52