Tafuta

Tanzania-Zanzibar:Toleo la 5 la Kimataifa la mchezo wa Kitesurf 2026:"Zanzibar Cup" litafanyika tarehe 7 Februati 2026 kwenye Fukwe za Kiwengwa. Tanzania-Zanzibar:Toleo la 5 la Kimataifa la mchezo wa Kitesurf 2026:"Zanzibar Cup" litafanyika tarehe 7 Februati 2026 kwenye Fukwe za Kiwengwa. 

Tanzania,Shindano la Zanzibar Cup 2026:Thamani ya mchezo kwa watu

"Ujumbe wetu wa amani na udugu miongoni mwa watu wote umezinduliwa Ulimwenguni kote,kwa nguvu zaidi katika kila matukio yetu.Wakati huu jambo jipya ni kwamba ujumbe wetu utasambazwa zaidi,shukrani kwa matangazo ya Televisheni ya Azam(TV),pamoja na matangazo ya lugha ya Kiswahili,Kitaaliano na Kiingereza ya Radio Vatican."Haya yalisemwa na Dk Conte,Mwanzilishi wa Shindano la Zanzibar Cup,ambalo limefikia Toleo la 5 na litafanyika tarehe 7 Februari 2026 huko Kiwengwa,Zanzibar,Tanzania.

Na  Angella Rwezaula – Vatican.

Kwa mara nyingine tena, Baraza la Michezo la Taifa Zanzibar(ZNSC) na Kamati ya Kiwengwa Kitesurf(KKC) inayowakilishwa na shule mbili za zanzibar  za kitesurf za  Onelove Kite na Jambo Kite wanatoa mwaliko wa kushiriki mashindano huko Zanzibar, Tanzania yatakayofanyika tarehe 7 Februari 2026. Hili ni toleo la V,  tangu kuanza kwake. Masindano hayo hata hivyo yanategemea kipindi bora cha upepo mwanana wa kitropiki!  Kwa mujibu wa muandaaji mkuu Daktari Stefano Conte, ambaye ni Daktari wa Watoto, kama mpenda mchezo huo, alifanya juhudi kubwa ya maadalizi kutokana na uzoefu wake ili kuunganisha watu wa mataifa mbali mbali kufanya uzoefu huo wa pamoja, kwa mara ya kwanza katika eneo hilo la Zanzibar na hadi sasa mafanikio yanaonekana.

Ushindi wa tolie la 4 la Zanzibar Cup Desemba 2025
Ushindi wa tolie la 4 la Zanzibar Cup Desemba 2025

Katika mchezo ni kufafanua kile ambacho Hayati Baba Mtakatifu Francisko wakati wa uhai wake alikazia  kusema kuhusu thamani ya mchezo kwa watu kuwa: “Kukuza mchezo ambao ni kwa ajili ya kila mtu, mshikamano unaoweza kufikiwa na kulengwa kwa kila mwanamume  na mwanamke ni dhamira kubwa na changamoto ambayo hakuna mtu anayeweza kuifanya peke yake. Kiukweli, kwa kucheza tu kama timu na kuwa pamoja inawezekana kufikia malengo ya kauli mbiu ya Olimpiki: altius, citius, fortius, yaani: juu zaidi, haraka zaidi na nguvu zaidi(Hotuba Kongamo la Kimataifa la Michezo mnamo tarehe, Septemba 30,2022). Vatican News, imemfikia Dk. Conte akiwa Zanzibar, Tanzania  kuhusiana na toleo hilo la Tano, na hata tunakuleta mahojiano kamili:  

Dk. Stefano Conte tarehe 7 Februari mnaendeleza Toleo jingine  ikiwa sasa  mmeanza kuwa na uzoefu. Kuna maandalizi tofauti na matoleo mengine ya Zanzibar Cup huko Kiwengwa  Zanzibar?

Asante kwa swali lako mpendwa Angela. Jambo jipya katika toleo hili la Tano, la Zanzibar Cup, litakuwa ni Televisheni mbashara ya Azam katika Kipindi cha michezo tarehe 7 Februari 2026 na Mikutano miwili na Vyombo vya Habari, itakayofanyika tarehe 3 Februari, mmoja katika Hotel ya Marumaru kwa ajili ya REGATTA na mmoja katika Hotel ya Golden Tulip, kwa ajili ya shindano la Freestyle. Katika mikutano hii pia tutangaza kwa umma majina ya wanariadha Saba ambao wana nafasi zaidi ya kushinda mashindano hayo.

Shindano la Freetyle  Desmba 2025
Shindano la Freetyle Desmba 2025

Tangu awali kuanzisha mchezo huu   kiini cheke ni kuunganisha tamaduni na mataifa mbali mbali kwa ajili ya amani na urafiki kati ya watu. Mchezo kwa Asili yake ni furaha ya kukutana na kuishi kidugu. Leo hii kuliko hapo awali tunahitaji maelewano na kudumisha urafiki wa kweli kati yetu na wengine, katika mtazamo daima wa ujenzi wa amani. Dk. Conte hili utalisisitizia zaidi kwa wale wote watakaoshiriki?

Kweli kabisa! Ujumbe wetu wa amani na udugu miongoni mwa watu wote umezinduliwa Ulimwenguni kote, kwa nguvu zaidi katika kila matukio yetu. Wakati huu ujumbe wetu utasambazwa zaidi, shukrani kwa matangazo ya Televisheni ya Azam (TV), pamoja shukrani kwa matangazao ya lugha ya Kiswahili, Kitaaliano na Kiingereza ya Radio Vatican. Wimbo wetu ambao binafsi nilitunga na Muziki na nyimbo, vinazungumza wazi jinsi gani sisi sote tunaweza kuishi kwa furaha na mambo rahisi kati ya kaka na dada, badala ya kufuata hadithi za uongo za utajiri na tamaa. Leo hii watu wengi wanateseka kwa sababu ya vita na wale wanaotaka kuiba mali zao tu. Sera za nchi matajiri za Magharibi leo hii ni mbaya sana, na kwa njia yangu ndogo ninazilaani vikali.

Matoleo mengine wamejitokeza wanamichezo kutoka mataifa mengine kadhaa, je Toleo hili mliweza kuwapata waliojiandikisha hata kutoka Afrika?

Katika toleo hili kuna washiriki 42 kutoka nchi 6 tofauti. Mbali na Tanzania, nchi nyingine inayowakilisha bara la Afrika ni Afrika Kusini. Ningependa pia wajitokeze kutoka nchi nyingine za Afrika, hasa zilizo karibu na Bahari na Maziwa Makuu kama vile: Kenya, Msumbiji, Malawi,  Uganda, lakini hadi sasa haijawezekana. Ni matumaini kuwa matoleo yanayofuata wataweza kujitokeza.

Dk Stefano katikati akiwa na wenzake
Dk Stefano katikati akiwa na wenzake

Matarajio yako ni yapi katika Toleo hili la kwanza kwa mwanzo wa Mwaka Mpya 2026?

Matarajio yangu kwa mwaka huu mpya, ni sawa na yale ya siku zote: kuikuza Zanzibar Cup,  ili ipate umaarufu duniani, na ili kila mtu aweze kuiga mfano wetu wa amani na udugu baina ya watu, na kwamba wanamichezo wengi waweze kuja Zanzibar kufanya mazoezi ya kitesurfing.

Tunapofikia mwisho wa mahojiano haya,  Dk. Conte Je  unalo la ziada kwa ufupi unalotaka kuwashirikisha wasikilizaji wa Radio Vatican?

Ninawaomba wasikilizaji wote wa Radio Vatican kutusaidia kushirikisha ujumbe wetu na kufuatilia tukio letu moja kwa moja kwenye Ufukwe wa Kiwengwa tarehe 7 Februari 2026 na hasa walio karibu na maeneo hayo au kutazama tukio hilo Mbashara kupitia televisheni niliyoitaja mwanzoni kuhusu mambo mapya ya tukio hili. Napenda kuzishukuru Serikali za Tanzania na ile ya Zanzibar kwa msaada wao mzuri, na wale wote wanaotusaidia kuwezesha  tukio letu lizidi kuwa muhimu bila kuwasahau  Wadhamini wetu wote.

Wakati wa mashindano ya matoleo ya 2025
Wakati wa mashindano ya matoleo ya 2025

Dk. Conte, Tunawatakia mashindano mema ya Zanzibar Cup

Asante kwa matashi mema na mahojiano haya mazuri. Tutumaini kwamba kutakuwepo upepo mzuri siku ya mashindano, maana upendo ndiyo Injini na kwamba ushindi daima uwe na sifa ya mchezo wa haki.  Ikiwa kila kitu kitakwenda vizuri, mpango wangu ni kuandaa Toleo la Sita la Zanzibar Cup, mnamo Agosti 29, 2026. Kwa sababi hui karibuni nilipokea mapendekezo kutoka nchi zingine ulimwenguni, ili kuandaa hafla kama hiyo. Ni matumaini kwamba tunaweza kuendelea kufanya hivyo hapa Zanzibar na kuongeza wasikilizaji wa ujumbe wetu katika sehemu nyingine za duniani pia.

Zanzibar Cup 7 Februari 2026
03 Februari 2026, 10:56