Wanajihadi wa ADF Wafanya Mauaji Mapya Mashariki mwa DRC
Na Sr. Christine Masivo CPS – Vatican.
Kulingana na Kanali Alain Kiwewa, Msimamizi wa kijeshi wa Eneo la Lubero, wapiganaji wa ADF walianzisha mashambulizi ya vurugu katika kijiji cha Musenge kuanzia usiku wa Januari 24. Washambuliaji hao wanaripotiwa kuchoma moto karibu kijiji kizima, na kuharibu nyumba kadhaa, kituo cha afya, na Kanisa Katoliki. Watu 25 wameuawa kwenye mashambulizi hayo, yanayohusishwa na Vikosi vya Washirika vya Kidemokrasia (ADF) katika Mkoa wa Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mamlaka mahalia zilisema.
Mashambulizi na maafa
"Tokea usiku wa Januari 24, ADF wamewatisha wakazi wa Musenge," Kanali Kiwewa alisema. "Nyumba kadhaa ziliteketezwa moto, pamoja na kituo cha afya na kanisa Katoliki." Afisa huyo wa Congo aliongezea kusema kuwa, wanajeshi wawili walifariki baada ya kupata majeraha makali wakati wa mashambulizi hayo. "Kwa sasa tunaomboleza wanajeshi wawili ambao miili yao haitambuliki kutokana na kiwango cha majeraha yao," alisema. Idadi kubwa ya wakazi wamekimbia eneo hilo, wakitafuta makao katika jiji la Butembo, lililoko umbali wa karibu kilomita 30. Mamlaka zinaonya kwamba idadi ya vifo vya sasa inabaki kuwa ya muda huku vikosi vya usalama vikiendelea kutathmini hali hiyo. "Tunasubiri taarifa zaidi kutoka kwa vikosi vya usalama vya Kongo na Uganda vilivyowekwa katika eneo hilo ili kupata tathmini kamili," Kanali Kiwewa aliongeza.
Uharibifu wa mali
Musenge iko katika Mkoa wa Mwenye, eneo ambalo limepitia mashambulizi ya mara kwa mara ya ADF katika miezi ya hivi karibuni. Mashirika ya kiraia yanaripoti kwamba mashambulizi ya awali katika eneo hilo tayari yamesababisha vifo vya raia zaidi ya 25 na kusababisha uharibifu wa angalau nyumba 63. Ukosefu wa usalama unaoendelea pia umelazimisha kufungwa kwa vituo vitano vya afya vya eneo hilo, na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa huduma ya matibabu kwa wakazi. Wakati huo huo, vurugu za ADF zimeendelea katika jimbo jirani la Ituri. Angalau raia watatu waliuawa wakati wa shambulio mara mbili katika vijiji vya Ahombo na Mangwalo katika Eneo la Irumu usiku huo huo. Vyanzo vya ndani vinaripoti kwamba wakazi kadhaa kutoka vijiji hivyo viwili bado hawajulikani walipo.
Tangu mnamo mwezi Mei 2021, Mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri yamekuwa chini ya hali ya kuzingirwa, hatua maalum ya kiutawala ya kijeshi inayolenga kuimarisha juhudi za Vikosi vya Wanajeshi vya Kongo, (FARDC) dhidi ya ADF na makundi mengine yenye silaha ambayo yamekuwa yakisumbua eneo hilo kwa miongo kadhaa. Hata hivyo, karibu miaka mitano baada ya hatua hiyo kuanzishwa, ukosefu wa usalama bado umeenea. Makasisi kutoka Dayosisi ya Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, wanasema hali imezorota chini ya utawala wa kijeshi, huku vurugu zikiendelea kuchukua maisha ya raia na kuhamisha jamii.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here