Tafuta

VENEZUELA-US-CONFLICT-CRISIS

UN yaonya hatari ya kuongezeka mvutano kufuatia hatua ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela

Baraza la Usalama la Umoja lilifanya kikao cha dharura baada ya operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela tarehe 3 Januari 2025,hatua iliyozua hofu ya kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na utulivu nchini humo na katika eneo zima.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kunako tarehe 3Januari 2026 dunia iligubikwa na ripoti za Marekani kushambulia Venezuala na kumtwaa Trump Rais wa nchi hiyo Nicolás Maduro pamoja na mkewe ili wajibu tuhuma dhidi za uhalifu mkubwa dhidi yao nchini Marekani. Baraza la Usalama, chombo cha Umoja wa Mataifa chenye wajibu wa kusimamia amani na usalama kilitangaza kukutana tarehe 5 Januari kwa  kujikita kwenye suala hilo ambapo hotuba ya Katibu Mkuu Antonio Guterres ilisomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Idara ya UN ya masuala ya siasa, (DPPA) Bi. Rosemary DiCarlo ambaye alisema, “Bado nina wasiwasi mkubwa kwamba kanuni za Umoja wa Mataifa hazikuheshimiwa katika shambulizi la kijeshi la tarehe 3 Januari. Chata ya Umoja wa Mataifa inakataza kitisho au matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya eneo au uhuru wa kisiasa wa taifa lolote.”

Wakati huu ambapo Rais Maduro na mkewe walifikishwa mahakamani Januari 5 hapo New York, Marekani Bi. DiCarlo alisema, “Kile ambacho hakina uhakika zaidi ni mustakabali wa sasa wa Venezuela. Nina wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na utulivu nchini humo, madhara yake kikanda, na mfano unaoweza kuwekwa juu ya uhusiano kati ya nchi na vile mataifa yanavyoendeshwa."

Mgogoro wa sasa unatokea baada ya miaka ya misukosuko, iliyozidishwa na uchaguzi wa rais wa mwezi Julai  2024 uliobishaniwa ambapo Bi. DiCarlo alisema, “Tumekuwa tukisisitiza uwazi na kuchapishwa kwa matokeo yote ya uchaguzi. Kama tulivyoripoti kwenye Baraza Desemba 23, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, imeorodoshesha ukiukwaji mkubwa.” Licha ya hali  ya sasa Katibu Mkuu kupitia DiCarlo alisema, “ninatoa wito kwa wana Venezuela wote kushiriki kwenye mazungumzo jumuishi na ya kidemokrasia ambamo kwamo sekta zote za jamii zitaamua mustakabali wao.” Na zaidi ya yote, “utawala wa sheria lazima uzingatiwe. Sheria ya kimataifa ina mbinu za kutatua masuala kama vile usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, mizozo kuhusu rasilimali na masuala ya haki za binadamu.”

Katika mkutano huo, wawakilishi wawili kutoka mashirika ya kiraia walizungumza, ambapo mmoja alialikwa na Marekani na mwingine aliakwa na Urusi na China. Baada ya Bi. DiCarlo alifuatia Jeffrey Sachs, Rais wa Mtandao wa Umoja wa Mataifa wa Majawabu ya Maendeleo Endelevu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo Endelevu katika Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani. Yeye alisisitiza kuwa suala linalozingatiwa leo si tabia ya Venezuela. “Hoja ni kama nchi mwanachama yeyote ina haki, kwa kutumia nguvu, shinikizo au nugu za kiuchumi, kuamua mustakabali wa kisiasa wa Venezuela au kudhibiti masuala yake ya ndani.”

Baraza linapaswa kuamua kama litalinda au litapuuza Ibara ya 2, kifungu cha 4 cha Chata ya Umoja wa Mataifa inayokataza tishio au matumizi ya nguvu dhidi ya uadilifu wa eneo au uhuru wa kisiasa wa nchi yoyote. Mercedes De Freitas, Mhasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kiraia la Transparencia Venezuela, alilieleza Baraza la Usalama kwamba mashirika ya kihalifu yana “uhusiano wa manufaa” na utawala wa Nicolás Maduro, yakitumia miundo ya serikali kwa biashara ya dawa za kulevya, unyang’anyi na biashara ya binadamu. Alisema rushwa imekula fedha za umma, na kuwaacha raia wakiwa na huduma duni, ukosefu wa chakula, na unyang’anyi wa kila siku unaofanywa na makundi yenye silaha. “Familia nyingi sana zinategemea mlo mmoja tu kwa siku,” ameonya, akiongeza kuwa kuongezeka kwa kutoadhibiwa kunachochea ukandamizaji, mateso na vifo vinavyosababishwa na ukosefu wa huduma za matibabu — matukio ambayo yameandikishwa na Umoja wa Mataifa. Akitoa wito wa uwajibikaji, alihimiza kuundwa kwa “serikali iliyo wazi na yenye uwazi” na kuachiliwa huru kwa wafungwa wote wa kisiasa.

Maoni ya Colombia: Kulaani tukio la Januari 3

Mwakilishi wa kudumu wa Colombia kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Leonor Zalabata Torres  Yeye alilaani vikali tukio la Januari 3, akisisitiza  kuwa Chata ya Umoja wa Mataifa inaruhusu matumizi ya nguvu katika hali za kipekee tu, kama vile kujilinda, na si kwa lengo la kutwaa udhibiti wa kisiasa wa nchi nyingine. Alionya kuwa hali ya kutokuwa na uhakika iliyosababishwa na “mashambulizi” hayo inaweza kuchochea wimbi kubwa la wahamiaji, jambo ambalo litahitaji rasilimali kubwa kusaidia jamii zinazowapokea. Kama hatua ya kuzuia, alisema, Colombia imechukua hatua za kudumisha utulivu mpakani na kushughulikia mahitaji ya kibinadamu yanayoweza kutokea, ikiwemo yale ya wahamiaji.

Kwa upande wa Urusi inabainisha Maduro aachiwe huru

Vassily A. Nebenzia ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa alisema Urusi inalaani  Marekani kwa kile alichokitaja kuwa uchokozi wa kijeshi dhidi ya Venezuela unaokiuka sheria za kimataifa, akihimiza Marekani kumwachilia mara moja “Rais aliyechaguliwa kihalali” pamoja na mwenzi wake. Aliwataka wanachama wa Baraza kuachana na viwango viwili na kutojaribu kuhalalisha “kitendo hiki cha wazi na cha kutisha cha uchokozi” kwa kuogopa kile alichokiita,  “askari polisi wa dunia wa kimarekani”. Akionya kuwa Marekani inalenga kudhibiti rasilimali asili za Venezuela, Balozi Nebenzia alisema  hatua zake zinazalisha “msukumo mpya wa ukoloni mamboleo na ubeberu.”

Marekani inabainisha kutekeleza opereshi ya kisheria ya usalama

Kwa upande wa  Mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Michael G. Waltz ambaye aliwaambia wajumbe kuwa, Marekani ilitekeleza “operesheni ya kisheria ya usalama iliyolengwa kwa usahihi” ili kuwakamata wakimbizi wawili waliokuwa wamefunguliwa mashtaka, akiwataja kuwa “gaidi wa dawa za kulevya Nicolás Maduro na mkewe Celia Flores”. Alisisitiza kuwa “hakuna vita dhidi ya Venezuela au watu wake”, amelinganisha hatua hiyo na kukamatwa kwa Manuel Noriega mwaka 1989. Alimwelezea Rais Maduro kama mkimbizi wa sheria na kiongozi wa “shirika katili la kigaidi la kigeni”, akidai kuwa ana uhusiano na mitandao ya biashara ya dawa za kulevya inayotumia “mihadarati haramu kama silaha.” Akitaja wasiwasi mpana wa haki za binadamu, ameelekeza kwenye madai ya mauaji kinyume cha sheria, mateso na kukamatwa kiholela, akibainisha kuwa zaidi ya wavenezuela milioni 8 wamekimbia nchi hiyo.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

 

07 Januari 2026, 12:48