Nigeria,Mashambulizi ya Silaha katika Jimbo la Plateau katika mkesha wa Mwaka Mpya
Vatican News
N i karibu watu tisa waliuawa na watu wenye silaha wakati wa sherehe za Mkesha wa Mwaka Mpya katika Jimbo la Plateau, kaskazini-kati mwa Nigeria.Mamlaka ilisema shambulio hilo lilitokea Jumatano jioni katika kijiji cha Chigwi,Wilaya ya Vwang,katika Eneo la Serikali ya Mitaa ya Jos Kusini,wakazi walipokuwa wakikusanyika kwa ajili ya sherehe za kiutamaduni za Mkesha wa Mwaka Mpya 2026. Katibu Mkuu wa Wilaya ya Vwang Iliya Chung alisema kwamba miili sita ilikuwa imepatikana kufikia Jumatano jioni, lakini idadi ya vifo iliongezeka hadi tisa siku iliyofuata kutokana na kulazwa hospitalini.
Jimbo la Plateau limekumbwa na vurugu za ndani kwa muda mrefu
Jimbo la Plateau limekuwa likikumbwa na vurugu zinazohusishwa na mapigano kati ya wanamgambo wenye silaha, migogoro kati ya wafugaji na wakulima, na vitendo vya magenge ya wenyeji. Aprili iliyopita, takriban watu 51 waliuawa katika mfululizo wa mashambulizi ya kutumia silaha katika maeneo ya Zike na Bassa.
Vitisho vya Marekani dhidi ya Nigeria
Mgogoro wa usalama nchini Nigeria hivi karibuni umevutia umakini wa kimataifa, hasa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kutuma jeshi nchini humo ili kudhibiti kile alichokiita mateso ya jumuiya za Wakristo. Usiku kati ya Desemba 24 na 25, mashambulizi mengi ya anga ya Marekani yalipiga kambi mbili za kijeshi zinazoaminika kuhusishwa na Dola la Kiislamu katika Msitu wa Baunel, kaskazini magharibi mwa nchi.
Hotuba ya Mwaka Mpya ya Rais Bola Tinubu
Katika hotuba yake ya Mwaka Mpya, Rais wa Nigeria, Bwana Bola Tinubu alisisitiza maendeleo ya kiuchumi na juhudi zinazoendelea ili kuhakikisha usalama zaidi. Kwa hivyo, mkuu wa nchi alitangaza mwanzo wa "awamu ya ukuaji imara zaidi wa uchumi" kwa mwaka wa 2026, unaosababishwa na matarajio ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka uliomalizika hivi punde, ambao alikadiria kuwa "zaidi ya 4%." Katika upande wa usalama, Tinubu alisisitiza "hatua kali" zilizochukuliwa Desemba 24 dhidi ya malengo ya kigaidi kaskazini magharibi, kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Marekani. Tangu wakati huo, Vikosi vya Jeshi vimeendelea kufanya kazi dhidi ya ngome za kigaidi na za uhalifu kaskazini magharibi na kaskazini mashariki, alihitimisha.