Tafuta

Shirika la Afya Duniani WHO limeeleza masikitiko yake makubwa kufuatia notisi ya Marekani ya kujiondoa katika Shirika hilo. Shirika la Afya Duniani WHO limeeleza masikitiko yake makubwa kufuatia notisi ya Marekani ya kujiondoa katika Shirika hilo.  (AFP or licensors)

Marekani Yajitoa Rasmi Shirika la Afya Duniani WHO! Lajibu Shutuma za Marekani

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza masikitiko yake kufuatia uamuzi wa Marekani kujiondoa rasmi katika shirika hilo, likisema hatua hiyo inaongeza hatari kwa Marekani na usalama wa afya duniani katika ujumla wake ujumla. Marekani ilitoa notisi ya kujiondoa tarehe 20 Januari 2025 kupitia amri ya Rais Donald Trump, na kujitoa rasmi Januari 22, 2026, ikieleza nia ya kufanya kazi za afya moja kwa moja na Mataifa mengine bila kupitia Mashirika ya kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza masikitiko yake kufuatia uamuzi wa Marekani kujiondoa rasmi katika shirika hilo, likisema hatua hiyo inaongeza hatari kwa Marekani na usalama wa afya duniani katika ujumla wake. Marekani ilitoa notisi ya kujiondoa tarehe 20 Januari 2025 kupitia amri ya Rais Donald Trump, na kujitoa rasmi Januari 22, 2026, ikieleza nia ya kufanya kazi za afya moja kwa moja na Mataifa mengine bila kupitia Mashirika ya Kiimataifa. WHO imesema taarifa ya kujiondoa itajadiliwa katika kikao cha Bodi ya Utendaji tarehe 2 Februari 2026 na Mkutano wa Afya Duniani utakaofanyika mwezi Mei 2026. Shirika la Afya Duniani limekanusha madai ya Marekani kuwa limeharibu heshima na uhuru wake, likisisitiza kuwa limekuwa likishirikiana na Marekani kwa nia njema na kwa kuheshimu mamlaka yake ya kitaifa. Kuhusu lawama za Marekani juu ya mwitikio wa WHO katika kukabiliana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Shirika hilo limesema lilitoa mapendekezo ya kiafya kama matumizi ya barakoa, chanjo na umbali wa kimwili bila kulazimisha sera hizo, na lilitoa taarifa sehemu mbalimbali za dunia mapema sana kuhusu hatari ya ugonjwa huo tangu taarifa za awali kutoka China zilipolifikia mwishoni mwa mwaka 2019.

Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani

‎Shirika la Afya Duniani (WHO), pia limeeleza kuwa ni Shirika huru na lisiloegemea upande wowote, linaloongozwa na nchi wanachama 194, na limeendelea kuimarisha mifumo ya maandalizi na mwitikio dhidi ya majanga mbalimbali yanayoendelea kuibuka sehemu mbalimbali za dunia. Aidha, limepongeza nchi wanachama kwa kupitisha Mkataba unaolenga kuimarisha usalama wa afya duniani. Kwa sasa, WHO inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa kushirikiana na nchi zote, huku ikieleza matumaini kuwa Marekani, kama mwanachama mwanzilishi aliyetoa mchango mkubwa katika mafanikio ya afya ya umma duniani, itarejea kushiriki kikamilifu katika Shirika hilo siku zijazo.

Kujitoa kwa Marekani kutoka kwenye Shirika la Afya Duniani ni hatari
Kujitoa kwa Marekani kutoka kwenye Shirika la Afya Duniani ni hatari   (AFP or licensors)

Shirika la Afya Duniani, WHO limeelezea masikitiko yake makubwa kufuatia notisi ya Marekani ya kujiondoa katika Shirika hilo likionya kuwa hatua hiyo “inaifanya Marekani na dunia kuwa katika hali isiyo salama zaidi.”  Katika taarifa iliyotolewa tarehe 22 Januari 2026 WHO ilisisitiza mchango wa muda mrefu wa Marekani kama mwanachama mwanzilishi, ikiwa ni pamoja na mafanikio makubwa ya afya duniani kama vile kutokomeza ugonjwa wa ndui na kupiga hatua dhidi ya Polio, Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi, Ebola, Malaria na magonjwa mengine ya hatari. “WHO inaendelea kujisadaka kikamilifu kufanya kazi na nchi zote katika kutimiza dhamira yake kuu,” imehitimisha taarifa hiyo huku, ikithibitisha tena jukumu lake la kikatiba la kuhakikisha “kiwango cha juu zaidi cha afya kinachowezekana kama haki ya msingi kwa watu wote.”

Shirika la Afya Duniani , WHO

 

26 Januari 2026, 10:23