Tafuta

Mahema mengi ya wakimbizi Mahema mengi ya wakimbizi  (AFP or licensors)

Jamhuri ya Afrika ya Kati:Dharura ya Kimya ya Kibinadamu Ukingoni mwa Taifa

Katika eneo la Kusini-Mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR),mgogoro wa kibinadamu umefikia kiwango kikubwa.Kwa miaka mingi,vurugu na ukosefu wa usalama vimewafanya wakazi kutoroka kutoka majumbani mwao na kuwaacha zaidi ya watu 30,000 wakimbizi wakitafuta mahali pa kuishi.

Sr. Christine Masivo, CPS- Vatican.

Katika mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC), maelfu ya familia sasa wanaishi katika umaskini uliokithiri, ambao kwa kiasi kikubwa umesahaulika na ulimwengu wa nje. Watu zaidi ya 30,000, wakimbizi wametorka makwao na hawana mahali pa kukaa.

Hali yazorota

Kulingana na Askofu mwandamizi Aurelio Gazzera, wa Jimbo la Bangassou,nchini DRC,  hali inayozunguka mji wa Zémio ni mbaya sana. Familia zilikimbia zikiwa na nguo walizokuwa wamevaa, zikitoroka mapigano mapya yaliyozuka mwishoni mwa 2023. Kwa sasa wengi wametawanyika kati ya misheni za Kikatoliki huko Zémio na Zapaye zilizo karibu, ng'ambo ya mpaka nchini DRC. Hawana mahitaji ya msingi kama chakula, maji safi, malazi, na huduma ya afya, na basi kusababisha maisha kuwa magumu zaidi. Watoto ni miongoni mwa walioathiriwa zaidi. Elimu, ambayo hapo awali ilikuwa njia tete ya maisha, sasa imesitishwa. Kabla ya wimbi la mapigano mapya, shule ya Sekondari ya  Zémio iliandikisha karibu wanafunzi 1,000. Sasa, ni wanafunzi 72 pekee waliosalia. Wengine wamelazimika kuacha masomo yao, mustakabali wao ukiwa umesimamishwa na ukosefu wa usalama na kuhama.

Hali mbovu ya kiuchumi na usalama

Eneo la Zémio ni mojawapo ya maeneo ya mbali na yaliyopuuzwa zaidi nchini, ambapo miundombinu haipo kabisa. Barabara moja inayounganisha mji na Bangassou, mji mkuu wa kikanda, ina urefu wa takriban kilomita 300 na inaweza kuchukua hadi masaa 17 kupita katika hali ngumu. Wakati wa mvua, sehemu za barabara huwa hazipitiki, na hivyo kuziacha jamii ambazo tayari zimetengwa na kufanya ufikiaji wa kibinadamu kuwa mgumu zaidi. Kwa zaidi ya miaka 15, eneo hili linalojumuisha Mbomou, Haut-Mbomou, na Boki limevumilia ukosefu wa utulivu usiokoma. Makundi yenye silaha yameacha makovu makubwa zaidi. Jeshi la Upinzani la Lord’s Resistance Army (LRA), waasi wa Seleka, vikundi vilivyogawanyika kama vile (Unite pour la Paix en Centrafrique (UPC) yaani Muungano kwa ajili ya Amani, na  hivi karibuni wanamgambo wa Azandé Ani Kpi Gbé,  wote walichangia katika mizunguko ya vurugu. Ingawa baadhi ya vikundi vilidai kuwalinda watu wa eneo hilo, uwepo wao mara nyingi umeongeza mvutano na ukosefu wa usalama.

Misaada wa dharura

Juhudi za kibinadamu zinakabiliwa na vikwazo vikubwa. Kanisa la eneo hilo, likifanya kazi na washirika kama Caritas, linajitahidi kusambaza chakula na vifaa muhimu. Lakini hata kufika Bangassou ni ngumu kimantiki, na safari ya kuelekea Zémio ni hatari. Mashambulizi ya zamani dhidi ya wafanyakazi wa misaada yanasisitiza hatari halisi zinazohusika, na kuzua hofu kwamba msaada huenda usiwafikie wale wanaouhitaji zaidi. Hata vituo vya afya havijaokolewa. Askofu Gazzera alisimulia mashambulizi dhidi ya hospitali na wanaume wenye silaha waliotafuta wapiganaji waliojeruhiwa, ukumbusho mkali kwamba hakuna nafasi hata iwe ya upande wowote iliyo salama kweli.

Amani inahitajika

Kama Askofu alivyosisitiza, amani ya kudumu haiwezi kupatikana kupitia hatua za kijeshi pekee. Kushughulikia chanzo kikuu cha mgogoro huu umaskini sugu, kutengwa, ukosefu wa miundombinu, na ukosefu wa ulinzi madhubuti wa serikali ni muhimu. Hadi wakati huo, makumi ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao bado wamenaswa katika hofu na kupuuzwa, wakiishi pembezoni mwa mojawapo ya majimbo dhaifu zaidi duniani, wakisubiri kuonekana na kusikilizwa.

Huko CAR: Afrika ya Kati

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

15 Januari 2026, 11:23