Onyo la UNHCR:Dunia inakabiliwa na mzozo wa kibinadamu usio na kifani
Na Federico Azzaro na Angella Rwezaula – Vatican.
Ulimwengu unakabiliwa na janga la kibinadamu ambalo halijawahi kutokea. Huku zaidi ya watu milioni 120 wakilazimika kuyahama makazi yao kutokana na migogoro na ghasia, rasilimali za usaidizi wa kibinadamu zinapungua kwa kiasi kikubwa. Katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican, Filippo Ungaro, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi(UNHCR,) alitoa wito ili jumuiya ya kimataifa isiwape kisogo walio hatarini zaidi. Kiukweli, kupunguzwa kwa ufadhili kunaweka mamilioni ya maisha katika hatari.
Wanawake, watoto na wakimbizi, waathirika wakuu
Waathirika wa kwanza ni wanawake, watoto na wakimbizi ambao wanajikuta bila kupata huduma muhimu. "Wanawake na wasichana wanaokimbia wanakabiliwa na ubakaji na unyanyasaji, wakati watoto wanahatarisha kuwa waathirika wa utumikishwaji wa watoto, biashara haramu ya binadamu au ndoa za utotoni," Ungaro alielezea. Matokeo yanaonekana katika maeneo yote ya maisha ya kila siku ya wakimbizi: chakula kidogo, maji kidogo, ulinzi mdogo. Hali ni ya kushangaza katika nchi zinazohifadhi idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao, kama vile Sudan, Sudan Kusini na Chad, ambazo tayari ziko katika hali tete. Msemaji wa UNHCR, alisisitiza kuwa “ Mgogoro wa ufadhili unasababisha mzozo wa uwajibikaji, na itakuwa na athari sio tu kwa maisha ya watu, lakini kwa utulivu wa kanda nzima."
Madhara ambayo tayari yanaonekana
Kulingana na makadirio, karibu wakimbizi milioni 13, wakiwemo watoto milioni 6.3, wanaweza kuachwa bila huduma ya matibabu ya kuokoa maisha. "Kutakuwa na ongezeko la magonjwa ya mlipuko, utapiamlo na hali ya afya ya akili isiyotibiwa," Ungaro alisisitiza. Bangladesh ni mojawapo ya nchi zilizoathirika zaidi: karibu wakimbizi milioni moja wako katika hatari ya kupoteza huduma za msingi za afya, na wanawake wajawazito 40,000 ambao wanaweza wasipate huduma za kutosha za ujauzito na watoto 19,000 wana utapiamlo bila matibabu.
Elimu nayo iko hatarini
Elimu nayo iko hatarini. Bila ufadhili, maelfu ya watoto wakimbizi watakatishwa masomo, na kuwaweka kwenye mustakabali wa unyonyaji na umaskini. "Miaka kumi iliyopita, idadi ya wakimbizi ilikuwa nusu ya ilivyo leo," Ungaro anakumbuka, akisisitiza jinsi ongezeko la dharura za kibinadamu na kupunguza rasilimali ni mchanganyiko unaolipuka. Mgogoro wa kibinadamu sio tu suala la misaada, lakini pia la usalama wa kimataifa: "Kuna mazungumzo mengi kuhusu usalama, lakini hii pia inahusisha uimarishaji wa idadi ya watu na maendeleo ya nchi zilizoathirika."Ni muhimu kurejesha hisia za "jumuiya ya wanadamu," kama vile Papa Francisko alivyokumbusha katika hotuba yake kwa bodi za kidiplomasia: ushirikiano wa maendeleo lazima ubakie kipaumbele ili kuzuia mamilioni ya watu kulazimishwa kukimbia nchi yao ili kuendelea kuishi.
Wito kwa wafadhili
Kutokana na hali hii ya dharura, msemaji wa UNHCR alitoa wito kwa serikali na sekta binafsi kutimiza ahadi zao: "Tunashukuru kwa wafadhili wa kimataifa na tunathamini chaguo la Italia la kutopunguza fedha za kibinadamu, lakini tunahitaji nchi nyingine kutoa ufadhili ulioahidiwa." Hatari ni kwamba, bila kubadilika kwa mtindo huo, mamilioni ya maisha yataachwa bila kulindwa. "Tunahitaji uingiliaji madhubuti, wa umma na wa kibinafsi, ili kukomesha matokeo ya mzozo huu wa kifedha," anahitimisha Ungaro. Kwa sababu nyuma ya idadi kuna watu, familia na watoto ambao wanastahili maisha ya baadaye.