Haiti, Unicef:dharura juu ya elimu na kuajiri watoto katika magenge ya kihalifu
Vatican News
Mnamo Januari 2025 tu, vikundi vilivyojihami viliharibu shule 47 katika mji mkuu wa Haiti. Huku shule 284 ziliharibiwa mwaka 2024, mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya elimu yanaongezeka, na kuacha mamia ya maelfu ya watoto bila mahali pa kujifunzia. Hii ni dharura iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto(UNICEF) kupitia Neetanjali Narayan, mwakilishi wa shirika hilo katika nchi ya Caribbean. "Wakati vurugu zikiongezeka Haiti yote, elimu ambayo ni tumaini la mwisho kwa watoto wengi na kipaumbele cha juu kwa wazazi zimekuwa ndiyo hatarini zaidi, kuliko hapo awali, na kwamba siku chache zilizopita, ripoti za shambulio jingine ziliibuka. Video hizo zinaonesha watoto wakipiga kelele sakafuni, wakiwa wameganda kwa hofu kwa kusisitiza kuwa hki ni "Kikumbusho cha kutisha kwamba mashambulizi haya husababisha madhara ambayo huenda mbali zaidi ya kuta za darasa," Narayan alisema.
Tahadhari ya kuacha shule
Kutokana na mashambulizi haya, kuhama na umaskini unaozidi kuwa mbaya, UNICEF inakadiria kuwa mtoto 1 kati ya 7 nchini Haiti hayuko shuleni. Na karibu milioni 1 nyingine wako katika hatari ya kuacha shule. "Elimu, ambayo ni tumaini la mwisho kwa watoto wengi wa Haiti na kipaumbele cha juu kwa wazazi, imekuwa hatarini kuliko hapo awali” kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la watoto. Pia linashutumu ukweli kwamba mwaka 2024 uandikishaji wa watoto katika vikundi vyenye silaha uliongezeka kwa 70%. Hivi sasa, hadi nusu ya wanachama wa vikundi vyenye silaha ni watoto, baadhi yao wakiwa na umri wa miaka 8! Bila kupata elimu, watoto wako katika hatari zaidi ya kunyonywa na kuajiriwa na makundi yenye silaha. "Elimu ni mojawapo ya zana bora zaidi tunazopaswa kuvunja mzunguko huu," alisema.
Uwekezaji katika elimu
Licha ya changamoto za kimfumo, kujua kusoma na kuandika ni mafanikio yanayothaminiwa sana nchini Haiti, na familia hujivunia kuwekeza katika elimu ya watoto wao, kuanzia jinsi watoto wanavyokwenda shuleni, hadi familia zinazotenga sehemu kubwa ya mapato yao kwa ajili ya shuleni. Kwa familia za Haiti, elimu inasalia kuwa njia muhimu ya maisha. UNICEF inasimama karibu na familia nchini Haiti na kutoa huduma za elimu rasmi na zisizo rasmi ili kuhakikisha watoto walioathiriwa na janga hilo wanapata elimu bora, ikiwa ni pamoja na kukarabati shule zilizoharibiwa wakati wa mashambulizi. Kuanzisha nafasi za muda za kujifunzia na kuwajumuisha tena watoto waliohamishwa shuleni. Pamoja na washirika, madarasa ya kurekebisha pia yanafanyika ili kufidia muda uliopotea wakati wa kufungwa kwa shule.
Kusaidia familia katika matatizo ya kifedha
UNICEF pia inatoa vifaa vya shule na uhamisho wa fedha ili kusaidia familia kukabiliana na changamoto za kiuchumi za elimu ya watoto wao, na inaratibu afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia, pamoja na shughuli za kuongeza ufahamu juu ya unyanyasaji wa kijinsia. Msaada huu, hata hivyo, ni mdogo ikilinganishwa na kiwango cha mahitaji ya nchi. UNICEF inataka dola milioni 38 kuhakikisha watoto 600,000 wanaendelea na masomo licha ya mzozo huo. "Kiasi hiki kingefadhili kila kitu kutoka kwa uundaji wa nafasi za muda za kujifunza katika maeneo ya watu waliohamishwa hadi madarasa zaidi ya kurekebisha na mipango ya elimu rasmi na isiyo rasmi," taarifa hiyo inasomeka. Lengo pia ni "kukarabati shule na kuwapa watoto vifaa muhimu vya shule. Hata hivyo, hatua hizi muhimu zinafadhiliwa kwa 5%. "Amani na utulivu vinahitajika sana nchini Haiti, lakini pia ufadhili. Hivi sasa, zaidi ya watoto nusu milioni hawapati msaada wa elimu wanaohitaji na kwamba UNICEF na washirika wake wanaweza kutoa, si kwa sababu ya makundi yenye silaha, lakini kwa sababu ya ukosefu wa msaada wa wafadhili.”