Tanzania:Balozi Mongella katika Toleo la Tuzo ya TWCC 2025:"Kama tunataka maendeleo tushirikiane"
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Haki za wanawake ni haki za binadamu zinazowalenga zaidi wanawake na wasichana wote Ulimwenguni kote. Vuguvugu la haki za wanawake lilianza tayari tangu karne ya 19. Haki hizo zinaungwa mkono na sheria, mila na desturi za jamii mbalimbali, ambapo katika nchi nyingine, haki hizo hazizingatiwi na hivyo hukandamizwa au kukanywagwa tu. Haki za wanawake zinatofautiana kutoka jamii moja kwenda nyingine kuendana na historia, utamaduni na desturi zilizozoeleka. Masuala ambayo kwa kawaida huhusishwa na dhana ya haki za wanawake ni pamoja na uhuru wa kujitawala, kutokuwa na unyanyasaji wa kijinsia, kupiga kura, kushika nafasi za uongozi, umiliki wa mali na kuingia mikataba ya kisheria. Wanawake wanachangia usawa wa kijinsia katika jumuiya pana kwa kushiriki kikamilifu katika mbinu za kuelimisha, mipango na ushirikishwaji unaokuza usawa wa kijinsia, na unaosaidia mtaji wa kijamii katika mitandao ya wanawake. Na zaidi Wanawake wanajihusisha na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubuni bidhaa mbalimbali huku wengine wakifanya biashara katika vikundi au mtu mmoja mmoja.
Mabilionea 6 wanawake Tanzania
Hii imewezesha nchi ya Tanzania kujivunia kuwa miongoni mwa mabingwa wa uongozi wa wanawake, na kupata kutambuliwa katika kitengo cha “Mwanamke Anayeinuka la V la Tuzo ya Wanawake nchini Tanzania ikiongozwa na kauli Mbiu: “Mwanamke Anayeinuka 2025! Hayo yote yaliibuka kwa kuona Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania(TWCC), Jumatano tarehe 26 Machi 2025 kikiwatunuku wajasiriamali wanawake waliofanya vizuri zaidi hasa kwa kutambua na kusheherekea mchango wao bora wa wajasiriamali wanawake katika sekta ya viwanda na biashara nchini Tanzania. Miongoni mwa waliopokea tuzo hiyo ni wanawake sita mabilionea ambao ni: Bi Angelina Ngalula, Bi Eva Fumbuka, Bi Sara Masasi, Bi Judith Mhina, Bi Zainab Ansel na Aisha Mzee.
Katika hafla hiyo ya kutoa tuzo iliyofanyika katika Kituo cha Biashara, Mlimani City Dar Es Salaam, Rais wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Angelina Ngalula alieleza sababu kubwa ya kwa wafanyabiasha wanawake kutokukua kwamba: "Biashara hazikui kwa sababu baadhi ya watu hufungua biashara nyingi kwa wakati mmoja.” Katika hafla hiyo kati ya wageni waalikwa waliokuwapo ni Balozi Gertrude Mongella aliyekuwa ni Katibu Mkuu wa zamani wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa 4 wa Beijing, China kuhusu masuala ya hali za Wanawake, ili kupitisha kile kinachoendelea kufahamika kama: “Azimio la Beijing,” kwa lengo la kuleta usawa wa kijinsia, kuwainua wanawake katika nyanja mbalimbali baada ya kundi hilo kuwa limekandamizwa kwa miaka mingi duniani kote.
Kama tulivyosikia katika makala iliyopita wakati Bi Mongella akizungumza kwenye Radio ya Umoja wa Mataifa, (UN)kuhusu Mkutano wa 69 (CSW69) leo hii ninawaletea kwa ufupi aliyozungumza katika fursa ya Toleo la tano la Tuzo kwa wanawake waliojipambanua katika biashara ambapo pia alirudia kuwasimulia uzoefu alioshi majuma mawili au matatu akiwa katika Mkutano waa Umoja wa Mataifa kuhusu Kamisheni ya Hali ya Wanawake kwa ujumla. Katika mazungumzo yake kwa umati katika ukumbi huo Balozi Mongella alisema: “Ndugu zangu nikianza kufanya protokali tutakesha, ninaomba heshima kwa mgeni rasmi na wageni wote waliomo humu. Mimi nimefurahishwa sana kuwa hapa. Nimerudi kutoka New York juzi ambapo nilikuwa huko kama wiki mbili / tatu tukiangalia tumefanikiwa nini, tufanye nini zaidi ili tufikie lengo lile tulilotamania, tulipokuwa Beijing mwaka 1995, ya kwamba mwanamke na mwanaume ni binadamu walioumbwa na Mungu na wana haki sawa na katika haki hizo ni pamoja na haki ya kuelimika, haki za kushiriki katika maamuzi mbali mbali na haki za kulinda utu wao. Zilifika kama haki 12 ambazo tuliorodhesha huko Beijing.” Bi Mongella aliongeza kusema kuwa “ Tumetazama juzi tulipokuwa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN ) katika Nchi mbali mbali, mengi yametekelezwa. Na katika Tanzania, nadhani tumetekeleza zaidi ninaomba tupige makofi….” Na ningependa nisema hapa jioni ya leo, nimefurahi kwamba niko miongoni mwa baadhi ya watu ambao kila siku nimefanya kazi nao, lakini wana siri kubwa ya kuwa mabilionea…Na leo nimewatambua na mtanitambua na mimi tutakapokutana huko nje…”
Kwa kufanya kumbukizi ya hekima, Bi Mongella alisema “Hiyo ni moja. Na hili linanikumbusha msemo wa Ndugu yetu, aliye kwisha tutangulia mbele ya haki: rais Magufuli,(John Pombe). Yeye alisema kwamba alitaka kuona mabilionea mia moja, sijuhi kama mnamkumbuka?” Aliuliza swali Bi Mongella na kuongeza: “Na mimi nikapata nafasi, nikamwambia, mimi ninataka wale 50 wawe wanawake na 50 wawe wanaume. Sasa tumeanza mwendo na wakina Angelina na wote waliopata ubilionea hapa; tumeanza na tunaweza tukazidi 50. Kazi kwetu, hilo ni moja,” alisisitiza Bi Mongella. Aliendelea alisema “La pili: tumeona jinsi wanawake walivyo na bidii katika kukuza biashara katika nchi hii na kufanya uvumbuzi wa aina mbali mbali. Tunasonga mbele, lakini pia tulipokuwa juzi New York, watanzania wengi tulitembea kifua mbele kwa sababu ya kuwa na rais mwanamke, na wengine tulio wazee zaidi tulitembea kifua mbele.” Kadhali alisisitiza hilo kwa “Namibia yenyewe ilimwapisha rais mwanamke(tarehe 21 Machi 2025, Dk Netumbo Nandi Ndaitwah), aliyekulia Magomeni(Dar Es Salaam), akiwa mpigania uhuru; akiwa anasimamia(SWAPO). Na leo hii nimeona katika mtandao, Cabinet yake zaidi ya nusu ni wanawake. Hapo mpo...?
Wanawake wanasonga mbele: miiko imekwisha
Bi Mongella aliendela na mazungumzo akieleza jinsi ambavyo wanawake wanasonga mbele na kwamba: “Mimi humu nina ndugu zangu “Women contractors), ambapo Mimi ndiye mlezi. Kwa hiyo ninadhani kumbe ziwa langu zuri , na kwenyewe nimepata mabilionea na wengine wadogo kama Sara niko pamoja nao kwenye mitandao yetu. Mimi bado sijachimba dhahabu, lakini nasikia ardhi yangu huko Biharamulo ina dhahabu. Kwa hiyo na mimi kuna siku moja mtanitaja tena kama bilionea….” Balozi Mongella aliwageukia wanawake wengine zaidi: “wakina mama waliotoka mikoani, ninawaomba sana, miiko imefutwa. Zamani mwanamke kwenda kuwinda ilikuwa ni mwiko. Wanaume walisema mkienda kiwinda na wanawake, humwoni mnyama.” Katika hilo Balozi Mongella alitoa kichekesho: “sijuhi walikuwa wanaona nini? Labda walikuwa wakimkodolea mwanamke mpaka wanakuwa hawaoni wanyama?... Alafu kulikuwa ni mwiko kwa mwanamke kuchimba madini..., lakini sasa, kuna wanawake wachimba madini na vile vile wanawake walikuwa hawaruhusiwi kwenda ziwani kuvua samaki.” Kwa hiyo alisisitiza kwamba: "hivyo, hayo yote ya miiko yamekwisha, tunachokifanya sasa hivi tu, ni kuchanja mbuga, ili tuweze kutekekeza kazi za kujenga mataifa yetu.”