UNICEF:Watoto Mashariki mwa Congo ni waathirika wa kutekwa nyara na kubakwa!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell katika taarifa yake anabainisha kuwa:"Nimesikitishwa sana na ghasia zinazoongezeka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na athari zake kwa watoto na familia. Katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, tunapokea ripoti za kutisha za ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto unaofanywa na wahusika katika mzozo, ikiwa ni pamoja na ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia katika viwango vinavyozidi chochote ambacho tumeona katika miaka ya hivi karibuni. Katika Juma la Januari 27 hadi tarehe 2 Februari 2025, washirika wa UNICEF waliripoti kwamba idadi ya kesi za ubakaji zilizotibiwa katika vituo 42 vya afya iliongezeka mara tano katika Juma moja. 30% ya wale waliotibiwa watoto wanahusika. Takwimu halisi zina uwezekano mkubwa zaidi, kwa sababu waathirika wengi wanasitasita kujitokeza. Washirika wetu wanakosa dawa zinazotumika kupunguza hatari ya kuambukizwa (VVU) baada ya kushambuliwa kingono.
Mama mmoja aliwaambia wafanyakazi wetu jinsi ambavyo binti zake sita, ambaye mdogo wao alikuwa na umri wa miaka 12 tu, walivyobakwa na watu wenye silaha walipokuwa wakitafuta chakula. Watoto na familia katika sehemu kubwa ya mashariki mwa DRC wanaendelea kukabiliwa na milio ya risasi. Katika miezi ya hivi karibuni, maelfu ya watoto walio katika mazingira magumu katika kambi za wakimbizi wamelazimika kukimbia mara kadhaa ili kutoroka mapigano. Katika machafuko hayo, mamia ya watoto wametenganishwa na familia zao, na kuwaweka katika hatari kubwa ya kutekwa nyara, kuandikishwa na kutumiwa na makundi yenye silaha, na unyanyasaji wa kijinsia.
Katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita zaidi ya watoto 1,100 wasio na walezi wametambuliwa katika Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, na idadi yao inaendelea kuongezeka. Timu za UNICEF zinafanya kazi kwa haraka kusajili watoto wasio na wasindikizaji na waliotenganishwa, kuwaweka kwenye familia za muda za malezi na kuhakikisha wanapata huduma muhimu za kimatibabu na kisaikolojia. Hata kabla ya kuongezeka kwa mzozo wa hivi majuzi, uandikishaji watoto katika vikundi vyenye silaha tayari ulikuwa unaongezeka katika eneo hilo. Sasa, huku pande zinazopigana zikitaka kuhamasishwa kwa wapiganaji vijana sana, viwango vya uandikishaji vitaweza kuongezeka. Ripoti zinaonesha kuwa watoto walio na umri wa miaka 12 wanaandikishwa au kulazimishwa kujiunga na makundi yenye silaha.
Pande kwenye mzozo lazima zisitishe mara moja na kuzuia ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto. Lazima pia wachukue hatua madhubuti za kulinda raia na miundombinu muhimu kwa maisha yao, kulingana na majukumu yao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu. Washirika wa kibinadamu lazima wawe na ufikiaji salama na usiozuiliwa ili kufikia watoto na familia zote zinazohitaji, popote walipo. UNICEF inaendelea kutoa wito wa kuongezwa kwa juhudi za kidiplomasia kukomesha ongezeko la kijeshi na kutafuta suluhu la kudumu la kisiasa kwa ghasia, ili watoto wa nchi hiyo waishi kwa amani.