Umwagaji damu zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Na Valerio Palombaro na Angella Rwezaula – Vatican.
Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani kutoka Shirika la Kipapa la Makanisa Hitaji,(ACS), linabainisha kuwa: “Zaidi ya miili 70 imepatikana katika Kanisa la Kiprotestanti huko Maiba,Kivu Kaskazini, iliyosambaratishwa na ghasia kutokana na makundi ya waasi.” Mauaji hayo yalifanyika kati ya tarehe 12 na 15 Februari 2025 mikononi mwa waasi wa Allied Democratic Forces (ADF), kundi la kigaidi la Kiislamu lenye asili ya Uganda, ambao waliingia kijijini hapo na kuwateka takriban watu 100.
"Wengi wao walikuwa wamefungwa na wengine kukatwa vichwa. Miongoni mwa wahanga hao ni wanawake, watoto na wazee,” ilisema chanzo hicho ambacho kitambulisho chake kinahifadhiwa kwa sababu za kiusalama. Kuhusu nia ya mauaji hayo na mwenendo wa kundi hilo, chanzo hicho kiliongeza: "Inawezekana kwamba waathrika hawa hawakuweza kupinga au kustahimili maandamano ya kulazimishwa, kwa sababu wakati waasi wanachukua mateka huwafanya wasafiri nao, ama kama nyongeza kwa kikundi chao au kama vibarua vya kulazimishwa kuunga mkono juhudi za vita.
Wakati kuna utekaji nyara, wanahitaji watu wa kubeba. Ukichoka njiani, umemalizika. Nadhani ndivyo ilivyotokea kwa watu hawo 70." Chanzo kiliendelea: "Makundi ya Kiislamu, yamezidisha mashambulizi yao na uvamizi kwenye vijiji vya mbali, na kuua maelfu ya raia wa Congo. Kabla walikuwa katika maeneo mengine, lakini sasa ni huko Lubero ndiyo inashambuliwa. Magaidi hao wanaaminika kuwa na washirika wa ndani ambao hurahisisha shughuli zao; na hiyo ndiyo inatisha sana."
Mauaji haya yanakuja katika wakati mgumu sana kwa eneo lote la Kivu, ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono Rwanda, wanaendelea na mapigano makali na watu kukimbia. Kundi la M23 limeteka miji muhimu, kama vile Goma na Bukavu, huku likisonga mbele kaskazini na kusini katika hali ambayo wanajeshi wa Congo hawawezi kulikabili.
Mbali na wasiwasi kuhusu shughuli za ADF, chanzo cha ndani cha ACS kilieleza hofu kwamba katika siku zijazo M23 wanaweza kuiteka Butembo, jiji la pili kwa ukubwa katika Kivu Kaskazini, kama ilivyofanya kwa Goma na Bukavu, "Tunatarajia waasi kuingia mjini wakati wowote, ikizingatiwa kwamba wako kilomita 70 tu kutoka hapa. Kuna mateso mengi ya kisaikolojia huko Butembo, kwa sababu vita viko kwenye mlango wetu. Tumeona jinsi mikoa mingine ilivyogubikwa na machafuko, na sasa inaonekana ni zamu yetu."