Tanzania:Maamuzi ya EAC na SADC katika mkutano kuhusu mzozo DRC!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) walifanya maamuzi yatakayosaidia kurejesha amani katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), iliyogubikwa na mzozo wa muda mrefu sana. Mkutano huo wa pamoja uliofanyika jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania, kwa kukaribishwa sana na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, Jumamosi tarehe 8 Februari 2025 na ambao ulihudhuriwa na wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa wanachama wa EAC na SADC, ambao uliongozwa na Mwenyekiti wa EAC, Rais William Ruto, wa Jamhuri ya Kenya na Mwenyekiti wa SADC, Rais Emmerson Mnangagwa wa Jamhuri ya Zimbabwe, japokuwa hapakuwapo Rais wa Congo DRC, Bwana Felix Tshisekedi ambaye alishiriki kwa njia ya Mtandao.
Njia ya misaada ya kibinaadamu kazima ifunguliwe haraka
Baada ya majadiliano ya kina, Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), walikubaliana kuwa mgogoro wa mashariki mwa DRC unaweza kutatuliwa kwa njia ya kisiasa, kidiplomasia,na hatua za kiusalama. Akisoma maazimio ya Mkutano huo Katibu Mkuu wa EAC, Bi Veronica Nduva alisema kuwa mkutano umeamua kuwa pande zote zinazozozana katika mgogoro huo zisitishe mapigano mara moja na kuweka silaha chini bila masharti yoyote. Viongozi walisisitiza kuwa njia za misaada ya kibinadamu lazima zifunguliwe haraka ili kuruhusu upatikanaji wa chakula, dawa, na huduma nyingine muhimu kwa wananchi walioathiriwa na mapigano. Ili kuhakikisha hali ya usalama inarejea, wakuu wa majeshi wa EAC na SADC wamepewa siku tano kuandaa mpango wa Ulinzi wa Goma na maeneo yanayozunguka jiji hilo. Hatua hii inalenga kuzuia mashambulizi zaidi na kuwalinda wananchi walio katika hatari ya kushambuliwa na waasi.
Serikali ya DRC irejee katika meza ya mazungumzo na makundi ya waasi
Hata hivyo kwa upande wa Katibu Mkuu huyo alisema kwamba kwa upande wa mazungumzo ya amani, viongozi wa EAC na SADC waliamua kuwa serikali ya DRC irejee kwenye meza ya mazungumzo na makundi yote, yakiwemo ya kijeshi na yasiyo ya kijeshi, chini ya mwavuli wa mchakato wa Nairobi na Luanda. Kwa hiyo walikubaliana pia kuwa juhudi zote za amani zinazofanyika ziunganishwe kuwa mpango mmoja ili kuharakisha upatikanaji wa suluhisho la kudumu. Viongozi wa mkutano huo wameagiza kuondolewa kwa vikosi vyote vya kigeni visivyoalikwa kutoka ardhi ya DRC. Ili kuhakikisha utekelezaji wa hatua hiyo, wameagiza kufanyika kwa kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Ulinzi wa EAC na SADC ndani ya siku 30 zijazo ili kuweka mkakati madhubuti wa utekelezaji.
Jumuiya ya Kimataifa iunge mkono juhudi za kuleta amani
Katika maamuzi pamoja na hayo, viongozi hao walisisitiza kuwa suluhisho la kudumu kwa ajili ya mgogoro huo wa DRC lazima lijikite katika ushirikiano wa kisiasa na kidiplomasia. Kwa hiyo walisisitizia “Jumuiya ya kimataifa kuwa inapaswa kuunga mkono juhudi zakuleta amani, hasa kwa kusaidia juhudi za kidiplomasia na kuzuia uungwaji mkono wa makundi ya waasi.” Hatimaye Mkutano huo wa Vingozi wa EAC na SADC pia uliazimia “kuwa vikao vya aina hiyo viwe vinafanyika angalau mara moja kwa mwaka ili kujadili maendeleo ya utekelezaji wa maazimio yaliyowekwa na kuhakikisha kuwa mchakato wa kurejesha amani nchini Jamhuri ya Congo (DRC )unaendelea kwa kasi inayotakiwa.”