Maghala ya chakula Mashariki mwa DRC ya WFP yameporwa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (WFP) tarehe 17 Februari 2025 limelaani vikali uporaji wa maghala yake ya chakula mjini Bukavu, Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC.) Katika taarifa yake fupi ilyotolewa mjini Geneva shirika hilo limesema “Chakula kilichoibwa kilikuwa kimekusudiwa kusaidia familia zilizo hatarini zaidi wakati ghasia zinaendelea kuenea na upatikanaji wa chakula ukiwa mgumu zaidi.”
Uporaji utasababisha hali mbaya ya kibinadamu
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani limeonya kuwa uporaji huu utazidisha hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo la Mashariki ambako hali inazidi kuwa tete. Licha ya changamoto hii, WFP imesisitiza kuwa iko tayari kuanza tena ugawaji wa msaada wa chakula mara tu hali ya usalama itakapokuwa imerejea. Shirika hilo limehimiza hitaji la dharura la kurejesha utulivu katika maeneo yaliyoathirika ili wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu waweze kuwafikia wahitaji kwa usalama. Hata hivyo, ghasia zinazoendelea limesema shirika hilo zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa juhudi za usambazaji wa misaada ya kibinadamu. WFP imetoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro unaoendelea DRC kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu. “Hii inajumuisha ulinzi wa raia, wahudumu wa misaada ya kibinadamu, na mali za kibinadamu ili kuhakikisha msaada wa kuokoa maisha unawafikia wanaouhitaji.”
Mashambulizi dhidi ya misaada ya kibinadamu ni moja ya hatari kwa mamilioni ya watu
Shirika hilo pia limeeleza kuwa mashambulizi dhidi ya misaada ya kibinadamu yanahatarisha moja kwa moja maisha ya mamilioni wanaotegemea msaada huo ili kuendelea kuishi. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani(WFP),tukio hili la uporaji linajiri wakati ambapo mgogoro wa chakula unazidi kuwa mbaya katika eneo la mashariki mwa DRC, ambako ghasia zinazoendelea zimewalazimu maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kuathiri vibaya minyororo ya usambazaji wa chakula. Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani(WFP) inatoa wito wa msaada wa haraka kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kurejesha operesheni za kibinadamu na kuzuia mateso zaidi katika moja ya maeneo yaliyo hatarini zaidi kwa ukosefu wa chakula duniani.