Congo DRC:M23 yabeba tani 10 za madini ya kimkakati kutoka eneo la Kivu Kusini
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Zaidi ya tani 10 za madini ya kimkakati zilinaswa na wanamgambo wa M23 kutoka kituo cha Kivu Kusini. Haya yamesemwa katika barua iliyotumwa kwa Shirika la Habari za Kimisionari Fides na "Kikundi Kazi cha Mada kuhusu Migodi na Hidrokaboni za Mashirika ya Kiraia huko Kivu Kusini." Mkoa huu ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pamoja na Kivu Kaskazini, hatua kwa hatua unashindwa na wanamgambo wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.
Kupora kampuni ya madini ya CJX
Kulingana na dokezo hi "usiku kati ya tarehe 19 na 20 Februari 2025, kiwanda cha kuchakata madini cha kampuni ya CJX kiliporwa na watu wenye silaha wa M23". Wanamgambo hao walizima kamera za uchunguzi na "kuteka nyara na kutoweka maafisa wa usalama" katika kituo hicho. Kulingana na taarifa zilizokusanywa na kikundi cha mashirika ya kiraia ya Congo, "wanamgambo walikamata shehena ya takriban tani 10 za madini ya 3T ambayo tayari yalikuwa yameandikwa na tayari kuuzwa nje ya nchi.
Madini ya Kimkakati yanayosafirishwa kutoka Congo kwenda nchi za Nje
Madini ya (3T) Cassiterite (bati) wolframite(tungsten ),coltan (tantalum), ni madini matatu ya kimkakati kwa tasnia ya kielektroniki, anga na kijeshi ulimwenguni kote, ambayo ndiyo kitovu cha vita mashariki mwa DRC. Na CJX Minerals ni kampuni ya Madini ya kibinafsi chini ya sheria ya Congo, iliyoundwa mwaka wa 2014 na ndiyo msafirishaji mkuu wa madini haya (3T), katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.