Baada ya M23 kuingia Bukavu,mamia elfu ya watu wanakimbilia Burundi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Wakati mapigano yalipozidi kushika kasi katika Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), biashara mjini Bukavu bado zimefungwa, huku baada ya waasi wa M23 kuingia mjini, baadhi ya watu bado wanaonekana wakitembea barabarani, wakiwa wamegubikwa na ukimya wa viziwi. Hali katika mji mkuu wa Kivu Kusini inaelezewa na chanzo kutoka shirika la Habari za Kimisionari la Fides kulingana na ambao ufyatulianaji risasi ulikoma baada ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda kuingia jijini Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 mchana. Kuanguka kwa Bukavu kunafuatia mji ule wa Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, unaokaliwa sasa na M23 tangu mwishoni mwa mwezi Januari, wakati ilichukuliwa Kavumba na uwanja wake wa ndege.
Wakimbizi nchini Burundi
Kusonga mbele kwa waasi huko Kivu Kusini tayari kumesababisha maelfu ya watu waliokimbia makazi yao, wakati Vikosi vya Wanajeshi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimetelekeza Bukavu kwa haraka. Sehemu ya jiji iliachwa bila umeme, wakati shirika la Fides likiripoti uporaji hasa huko Kadutu, wilaya ya kihistoria ambayo soko kuu la ndani linapatikana. Wakimbizi hao walikimbia kutoka eneo la Kamanyola, kuvuka Mto Ruzisi, na kuweka kambi katika jimbo la kaskazini-magharibi la Burundi la Cibitoke. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Congo Martin Niteretse pia alithibitisha kwamba wakimbizi wengi wameingia Burundi, lakini serikali bado haijatoa idadi zinazohusiana na mtiririko huu wa wakimbizi. Waziri huyo aliongeza hivi: “Wakongo wengi walikimbia kwa sababu waliogopa walipojua kwamba jiji la Bukavu lilikuwa limetekwa.”
Mgogoro wa kibinadamu ambao unatia wasiwasi
Kwa tahadhari, kivuko muhimu cha mpaka kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi kilifungwa kwa muda mfupi tarehe 16 Februari ili kuzuia wimbi kubwa la wakimbizi. Kinshasa na Gitega zimekuwa na ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo kwa miaka mingi, na tangu mwaka 2023, jeshi la Burundi limetuma takriban wanajeshi 10,000 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusaidia mapambano dhidi ya zaidi ya makundi 100 yenye silaha ambayo yamekithiri katika eneo hilo. Wakati huo huo, mjini Kinshasa, Rais Felix Tshisekedi ameitisha mkutano wa usalama kujadili mabadiliko ya operesheni za kijeshi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, pamoja na hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea mashariki mwa nchi hiyo.