Zoezi la Wakazi wa Ngorongoro Kuhamia Msomera, Handeni, Tanga. Yanaojiri Kwa Sasa
Na Ofisi ya Waziri Mkuu, -Arusha, Tanzania.
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewahakikishia wakazi wanaohama kwa hiari yao kutoka katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga kuwa hakuna shughuli zao zitakazosimama na kwamba wataendelea na ufugaji katika mazingira bora zaidi. Ameyasema hayo Alhamisi, Juni 23, 2022 wakati akiwaaga wakazi wa Ngorongoro wanaohama kwa hiari yao kwenda kijiji cha Msomera na kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo. Hii ni awamu ya pili ya wakazi wanaohama katika eneo hilo kuelekea Msomera. Mazungumzo hayo yamefanyika kwenye viwanja vya Ofisi Kuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), Ngorongoro mkoani Arusha. Waziri Mkuu ambaye ameshuhudia wakazi hao takribani 127 kutoka katika kaya 27 wakihama na kuelekea kijiji cha Msomera, amewapongeza kwa uamuzi huo na kuwahakikishia kwamba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwapa ushirikiano. Amesema uamuzi walioufanya wa kuhamia Msomera na kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Ngorongoro ni uamizi sahihi, hivyo ametumia fursa hiyo kuwahakikishia kwamba hakuna shughuli zao zozote zitakazisimama, wataendelea na ufugaji kwa kuwa Msomera kuna eneo kubwa na la kutosha. “Ninawaomba msafiri kwa amani kabisa na mioyo yenu ikunjuke. Isikilizeni Serikali yenu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Sasa hivi mko huru, nenda mkakae kwenye nchi yenu kwa uhuru,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dkt. Christopher Timbuka amesema awamu ya pili ya zoezi la kuwahamisha wakazi wa eneo la Ngorongoro kwa hiari lilianza Juni 20, 2022, ambapo inahusisha jumla ya kaya 27 zenye watu 127 na mifugo 488. Aidha kaya moja kati ya hizo itahamia Karatu. Dkt. Timbuka amesema hadi sasa kaya zilizohama kwa hiari katika eneo la Ngorongoro katika awamu ya kwanza na ya pili ni 48 zenye jumla ya watu 233 na mifugo 899. Amesema utaratibu wa kuwahamisha umefanyika kwa kufuata hatua mbalimbali ikiwemo kuhakiki idadi ya watu. Pia, hatua nyingine ni kusainisha vitabu vya fidia vya wakazi wanaohama kwa hiari awamu ya pili, kuhakiki idadi ya mifugo na kuiweka alama ili iweze kusafirishwa pamoja na kuhakiki na kutambua aina za nyumba za wakazi hao kwa ajili ya taratibu za ubomoaji. Dkt. Timbuka amesema mbali na kupewa nyumba, fidia na shamba kaya zote pia zitapewa magunia mawili ya mahindi kwa kwa kipindi cha miezi mitatu ili waweze kujikimu katika kipindi cha mpito wakati wakijiandaa na msimu wa kilimo.
Naye, mmoja wa wakazi hao wanaohama kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, Bw. Emmanuel Saitoti kutoka kijiji cha Nainokanona ameishukuru Serikali kwa upendeleo ilioutoa kwao kwa kuwa mbali ya kupewa nyumba pia Msomera wanakwenda kupata fursa zitakazowaongezea tija kiuchumi. “Serikali tunaishukuru imetupendelea sana, tumepata hati za nyumba na mashamba pamoja fidia ya fedha, naishauri iendelee kuwahamasisha na wakazi wengine nao wahame kule hakuna maendeleo. Msomera tunakwenda kufanya shughuli nyingi za maendeleo.” Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezipongeza taasisi zote zilizokuwa zinaratibu zoezi la uwekaji wa alama katika eneo la Pori tengefu la Loliondo kwa kukamilisha uwekaji wa vigingi 424 vilivyokusudiwa kuwekwa. Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo Alhamisi, Juni 23, 2022) alipotembelea eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500 kuona maendeleo ya uwekaji wa alama kuzunguka eneo la hifadhi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa eneo hilo lina umuhimu mkubwa kwa Watanzania na hata nchi jirani. “Hii ni tunu tuliyopewa na Mwenyezi Mungu, uwepo wa wanyama ni kivutio kikubwa kwa shughuli zetu za utalii, ni muhimu tuilinde.” “Ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini unatokana na kodi ambazo Serikali inakusanya kutoka maeneo tofauti ikiwemo sekta hii ya utalii,” amesema Waziri Mkuu. Amesema kuwa Watanzania hawana budi kuzingatia na kuzifuata sheria zilizowekwa. “Kila nchi ina utamaduni wake, hata wewe Mtanzania unapotoka kwenda nchi yoyote, fuata sheria za nchi hiyo.” Amesema kuwa zoezi lililofanyika ni uwekaji wa alama tu, na hakuna mtu yeyote atakayeondolewa katika vijiji vinavyozunguka eneo hilo. “Hili eneo liko umbali wa karibu kilomita 12 hadi 15 kutoka kwenye makazi ya watu.” Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa zoezi la ulinzi katika eneo hilo ni endelevu katika kipindi chote na si wakati huu wa uwekaji wa alama pekee, na akaelekeza ulinzi uendelee kuimarishwa katika eneo la kilomita za mraba 1,500 zilizowekewa alama.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana alisema kuwa eneo hilo ni muhimu katika sekta ya utalii na ni wajibu wa Wizara kuhakikisha eneo hilo linalindwa. “Tumeshapitisha GN, sasa itaitwa Pori tengefu la Pololeti la kilomita za mraba 1,500.” Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bw. Mashimba Ndaki amesema kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa lambo kubwa litakalotumika kunyweshea mifugo katika eneo la Loliondo. Alisema kuwa Serikali inajenga majosho 10 ya kuogeshea mifugo na tayari majosho mawili yameshakamilika huku mengine manane yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi. “Serikali inawajali na inawaangalia sana wafugaji,” alisisitiza. Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Bw. Jumaa Aweso alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kupeleka huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote nchini ikiwemo Loliondo.
Mbele ya Waziri mkuu Majaliwa Kassim Maliwa, mwananchi mpya wa kijiji cha msomera aliyehamia kwa hiyari kutoka Ngorongoro Richard Sali Tobiko Ole Mokolo ametoa ushuhuda wa wananchi hao kupewa upendeleo ambao hawakuutarajia kamwe kuupata kutoka kwa serikali na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwao aliouonesha. Ushuhuda huo, ulitolewa na mwananchi huyo ni pamoja na sasa kumiliki ardhi yenye jina lake na mkewe, ambapo hakuwahi kuiona au kuifahamu hati, kupewa nyumba yenye vyumba vitatu na sebure ikiwa katika eneo lenye ukubwa wa ekari mbili na nusu, kupewa shamba lenye ukubwa wa ekari tano, kupatiwa miundombinu yote ya huduma muhimu za jamii ikiwemo maji safi salama na ya uhakika, umeme, uangalizi wa wataalumu wa mifugo na madaktari wa kibinadamu.
Vitu hivyo, amevitaja kama moja ya mambo makubwa ya upendeleo waliofanyiwa watu hao waliohama kwa hiyari kutoka Ngorongoro na ametumia nafasi hiyo kumwomba Waziri Mkuu Majaliwa kuendelea kutoa elimu sahihi juu ya eneo hilo kwa kuwa kuna upotoshaji mkubwa unaofanyika kuwazuia watu wanaotaka kuhama kwa hiyari kuja Msomera. Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Majaliwa, mwananchi huyo bwana Ole Mokolo ambaye tayari amechangamkia fursa kwa kubadilisha moja ya chumba chake kuwa duka la bidhaa mbalimbali kuwauzia wananchi wenzake, alisema maisha ya eneo hilo ni salama na wameyapenda ndani ya muda mfupi kutokana na uwepo wa huduma zote muhimu za kijamii. ''Kwa kweli najisikia vizuri sana, mwanzo hatukujua kama itakuwa hivi, kwa fidia tulishapewa, tulipewa nyumba yenye eka mbili na mashamba eka tano, hali ya hewa ni nzuri na watoto hawaisumbui. Tunaishukuru sana serikali, Rais Samia na wewe pia Waziri Mkuu kwa kuwa nasi toka mwanzo na mama mmoja hivi simjui vizuri anatoka Mamlaka ya Ngorongoro anaitwa Joyce''. Aliongeza ''Kwa kweli niwashauri sana wenzetu ambao wamebaki kule, wakati tunaondoka walikuwa wanatulilia ni kama tunapotea, lakini tumefika huku tunasikitikika, tunawalilia wao kwa sababu bado hawajajua hatima yao.
Akizungumzia upotoshaji unaofanywa na baadhi ya wanaharakati, Ole Mokolo alisema ''Nikuambie tu Waziri Mkuu kwamba kuna upotoshaji mwingi sana, tulipokuja huku tumepiga simu wengine wanasema katika Kundi la kwanza tulilokuja tayari kuna watu tayari watatu wamegongwa na nyoka wamefariki na kuna ngombe wameliwa na wanyama wakali na wengine wamesema ngombe zangu zilifika makuyuni zimekufa, lakini ngombe wangu wazima wote wale pale na mbuzi wangu pia wapo pale''. Aidha, alipoulizwa na Waziri Mkuu kuhusiana na upatikanaji wa maji safi na salama, mwananchi huyo alisema kuna maji mengi ambapo kuna vituo vya maji kila baada ya mita 400, kuna maji mazuri na hata mifugo haipati shida ya kunywa maji kwa kuwa muda wote wanapata majisafi na salama tofauti na Ngorongoro.
''Kule Ngorongoro ilikuwa mifugo tukinywesha maji leo, kesho hatunyweshi kwa sababu hakuna maji lakini huku maji ni mengi, tunachagua tunyeshwe ya bombani au ya kwenye visimani, sasa tumepata uhuru na haki na maisha yetu na kufanya lolote bila bughuza katika ardhi yetu'' alisema. Akituma salamu kwa Rais Samia, Ole Mokolo alisema 'Kwanza nasema kwa majina naitwa Richard Sali Tobiko Ole Mokolo nipeleke sana salamu zangu kwa mheshimiwa rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanznaia, mama yetu samia suluhu hassan, nimuombe sana zoezi hili angalau hata likiwa limeendaenda na yeye aje tutoe shukrani zetu kwake. tunashukurani nyingi sana za kumpa, kwa kweli ni upendeleo wa kutosha, niseme ni upendeleo wa kutosha kwa sababu sidhani kama kwa fidia tulizopata sidhani kwa fidia ambayo mtu amepata angelalamika hata kama asingepewa hivi vitu. Nyumba, Shamba na maeneo ya malisho na kusafirisha wao, mifugo na mizigo yao). Tunamwomba Rais Samia aje Msomera, tunampenda sana na kura zetu hazina mashaka kwake''. Juni 23, 2022, Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara ya siku moja mkoa wa Arusha katika Wilaya ya Ngorongoro na kuwaaga wananchi wanaohama kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia Msomera kundi la watu 117 lenye kaya 27 ikiwa ni awamu ya pili ya wananchi wanaohamia katika kijiji hicho, aidha Waziri Mkuu pia alitembelea Loliondo kushuhudia eneo la kilometa za mraba 1500 linalowekewa vigingi.