Hotuba ya Kwanza ya Rais Samia Suluhu Hassan Kwa Watanzania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Familia ya Mungu nchini Tanzania, tarehe 19 Machi 2021, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, aliyekuwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu wa Vikosi vya ulinzi na usalama nchini Tanzania. Sherehe hii fupi imeongozwa na Jaji Ibrahim Juma na kufanyika Ikulu, Dar Es Salaam. Baadaye, Rais Samia Suluhu Hassan amelihutubia Taifa la Tanzania kwa kujieleleza zaidi katika ratiba ya mazishi ya Hayati Dr. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021. Katika hotuba yake fupi, ameelezea sifa za Dr. John Pombe Magufuli, ari na mwelekeo wake wa kutaka kuwaendeleza watanzania.
Ameongoza Kikao cha kwanza cha Baraza la Mawaziri na kama Amri Jeshi mkuu amepigiwa mizinga ishirini na moja pamoja na kukagua gwaride la heshima! Katika hotuba yake iliyosheheni majonzi na simanzi kubwa, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amezungumzia kuhusu taarifa ya ugonjwa uliopelekea hata mauti ya Dr. John Pombe Magufuli hapo tarehe 17 Machi 2021. Ameelezea kwa kina mipango ya maombolezo ya kitaifa na mazishi yatakayofanyika hapo tarehe 25 Machi 2021. Tarehe 22 machi 2021, Hayati Dr. Magufuli ataagwa rasmi na watu wa Mungu Jijini Dodoma na itakuwa ni siku ya mapumziko kitaifa. Baada ya taarifa kuhusu maombolezo ya kifaifa, Rais Samia Suluhu Hassan amezungumza machache baada ya kula kiapo cha Urais kama Rais wa sita katika kipindi cha awamu ya tano.
Amegusia sifa za Hayati Dr. Magufuli, ari na moyo wake wa uzalendo katika kuwahudumia watanzania ili kuwaletea maendeleo mapana zaidi. Amesema, hiki ni kipindi cha kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa, kwa kupeana faraja na upendo. Ni muda muafaka wa kujenga na kuimarisha udugu wa kitanzania, amani, utu, uzalendo na utanzania wao. Rais Samia Suluhu Hassan amekazia umuhimu wa watanzania kuyaangalia ya mbeleni kwa kujiamini na kwa kuwa na matumaini. Ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Hiki ni kipindi cha kufutana machozi na kushikamana katika mchakato wa ujenzi wa Tanzania mpya aliyoitamani Dr. John Pombe Magufuli.