Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 21 ya Mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 21 ya Mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida.   (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 21 Mwaka A wa Kanisa: Kiri Kuu ya Imani ya Mtume Petro

Masomo ya Dominika hii ya 21 ya mwaka A wa Kanisa yanatilia mkazo kuhusu umasiha wa Kristo na mamlaka aliyompa Petro ili apate kuliongoza Kanisa lake. Mababa wa Kanisa wanafundisha kuwa Yesu Kristo ni Masiha wa kweli, Mungu Mwana, na Mwokozi wa ulimwengu. Walithibitisha kwamba umasiha wake haukuwa wa kisiasa au wa kidunia, bali ulikuwa wa kiroho kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu kutoka kwenye dhambi kupitia mateso, kifo, na ufufuko wake.

Na Padre Octavian Onesmo Hinju, JUCo, Morogoro, Tanzania.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 21 ya Mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya Dominika hii ya 21 ya mwaka A wa Kanisa yanatilia mkazo kuhusu umasiha wa Kristo na mamlaka aliyompa Mtume Petro ili apate kuliongoza Kanisa lake. Mababa wa Kanisa wanafundisha kuwa Yesu Kristo ni Masiha wa kweli, Mungu Mwana, na Mwokozi wa ulimwengu. Walithibitisha kwamba Umasiha wake haukuwa wa kisiasa au wa kidunia, bali ulikuwa wa kiroho kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu kutoka kwenye dhambi kupitia mateso, kifo, na ufufuko wake. Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 22 Agosti 2026 amefanya hija ya kichungaji Jamhuri ya San Marino na kuhudhuria Kongamano la Urafiki kati ya Watu: “Meeting per l'amicizia fra i popoli” na hatimaye, majira ya jioni, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Bandari ya Rimini, nchini Italia kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Ninyi ni nuru ya ulimwengu.” Mt 5:14. Itakumbukwa kwamba, Jamhuri ya San Marino ni nchi iliyoanzishwa na Mtakatifu Marino tarehe 3 Septemba 301 BK na Mwezi Aprili 1926 ikaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican, uhusiano ulioimarishwa kunako mwaka 1989 kwa njia ya Mkataba kamili “Concordato” na kupyaishwa tena mwaka 1992 kwa kusoma alama za nyakati. Kumbe, hija hii ya kichungaji nchini San Marino ni sehemu ya kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 100 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Jamhuri ya San Marino.

Wewe ndiwe Petro na juu ya Mwamba huu nitalijenga Kanisa langu
Wewe ndiwe Petro na juu ya Mwamba huu nitalijenga Kanisa langu   (@Vatican Media)

Kwa imani leo tunamshuhudia Mtume Petro akitambua na kukiri nguvu ya Mungu itendayo kazi ndani mwake kiasi cha kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Masiha wa Bwana. Umasiha wa kristu lilikuwa ni fumbo ambalo bado halikuwa limefunuliwa wazi kwa wanafunzi na wafuasi wa Yesu. Kumbe leo tunaona namna ambavyo imani inamsaidia Petro kupata ujasiri na kumkiri Kristu kuwa ni Mungu. Ni kwa sababu hii mafumbo ya kimungu mtu hapaswi kuyaendea kwa kutanguliza maarifa pekee au kwa kutafuta hoja kwa vipimo vya elimu zetu au ufahamu. Mafumbo ya kimungu, pamoja na akili na ufahamu, mtu hualikwa kuyaendea kwa imani. Ni imani inayoweza kufika pale ambapo akili na ufahamu wa kibinadamu haiwezi kufika. Tena ni imani inayoweza kuiangazia akili kupata hoja ya kuyapokea. Imani na ufahamu vinapaswa kwenda pamoja. Kuhusu Imani, Mwadhama Robert Kardinali Sarah anafundisha kuwa “imani ni ‘ndio ya mwanadamu’ kwa Mwenyezi Mungu. Ndio hiyo humtaka mtu kuacha miungu yake, utamaduni wake wa kale, hakika zote za kibinadamu, utajiri na fahari zote ili kuweza kuiingia nchi, utamaduni mpya na urithi wa kimungu. Imani ni kujiachia ili kuongozwa na umoja wa Mungu. Imani inaashiria na inahitaji uaminifu, kwa sauti ya Mungu inayosema ‘Nenda mbele yangu na ukawe mkamilifu’ (Mwz. 17:1). Itakumbukwa kuwa katika kiri kuu ya imani yetu tunasali na kusadiki kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la Mitume. Nalo kanisa ni la kitume kwa sababu limejengwa juu ya msingi imara wa mitume: tena kanisa limejengwa na linabakia katika msingi wa mitume. Kwa nyakati zote kanisa linahifadhi na kuendeleza kwa msaada wa Roho Mtakatifu, mwangaza wa mafundisho na mapokeo. Na mwishowe linaendelea kufundishwa, kutakatifuzwa na kuongozwa na mitume hadi mwisho.

Uongozi ni fadhila inayosimikwa katika unyenyekevu
Uongozi ni fadhila inayosimikwa katika unyenyekevu   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Nabii (Isa. 22:19-23). Katika somo hili tunamwona Isaya akitoa unabii kwa mtu aliyeitwa Shebna. Huyu alikuwa ni mkuu wa nyumba ya mfalme. Isaya alimlaumu na kumhukumu Shebna kwa sababu ya kiburi chake kikubwa, kujitukuza na kutumia vibaya madaraka yake kujinufaisha mwenyewe badala ya kumtegemea Mungu wakati wa hatari kwa taifa la Yuda. Shebna alijichimbia kaburi la kifahari na la kudumu juu mwambani, jambo lililoonyesha kuwaza kuhusu urithi na utukufu wake binafsi badala ya kuwajali wananchi waliokuwa hatarini. Badala ya kuongoza taifa kwa unyenyekevu na kutegemea ulinzi wa Mungu wakati Yerusalemu ilipokuwa inatishiwa na maadui, yeye na wenzake walijihusisha na sherehe, kula na kunywa. Inatajwa kuwa alikuwa na mtazamo wa kujipendekeza kwa mataifa ya nje (kama Ashuru) badala ya kuwa mwaminifu kwa Mungu na taifa lake. Kinyume na ilivyozoeleka, ni katika somo hili tu ndio tunaletewa sehemu pekee ambayo Isaya anatoa unabii kwa mtu binafsi. Mara zote katika kazi zake za kinabii, Isaya na hata manabii wengine wote wa Agano la kale walitoa unabii wao kwa Israeli nzima au kwa mataifa mengine ya kigeni. Katika unabii huu, Isaya anatabiri kuwa Shebna ataondolewa katika nafasi yake na nafasi hiyo atapewa mtu mwingine. Anapotoa utabiri huo, Isaya anatumia lugha ya picha ya ufunguo pamoja na maneno ya kufunga na kufungua. Lugha hii ya picha ya ufunguo inamaanisha mamlaka ya kutawala na maneno “kufunga na kufungua” humaanisha mamlaka ya kuhukumu au kutoa hukumu. Na Mungu mwenyewe anapotamka kwa kinywa cha Nabii Isaya akisema nitaweka mabegani mwako funguo au nitakupatia funguo anajitambulisha kuwa ni yeye anayetoa mamlaka hayo katika himaya ya mfalme. Tendo hili linakuwa ni kielekezo cha Mungu mwenyewe kuamua kuamua kumpa mwanadamu mamlaka na uwezo wa kutenda kazi juu ya ndugu zake.

Wokovu ni mpango wa Mungu kwa watu wote
Wokovu ni mpango wa Mungu kwa watu wote   (@Vatican Media)

Tendo hili linarudiwa tena na Kristo mwenyewe ambaye atalifanya kwa Petro anapomweka juu ya Kanisa lake. Naye atampa mamlaka ya kutawala na ya kutoa hukumu akimwambia anampatia funguo za kufunga na kufungua. Huu ukawa ni mwanzo wa utume mpya na endelevu wa kanisa chini ya Mtume Petro kama Khalifa wa Kristo Yesu. Somo hili linatoa ujumbe kwa viongozi na wenye mamlaka kutumia nafasi zao vema katika kuwahudumia watu wa Mungu. watambue kwamba uongozi ni huduma ambayo inapaswa kufumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu nao ni kama koti la kuazima tu basi wasilivae kwa mikogo. Uongozi ni sadaka ya utayari wa kukataa uhuru na matakwa binafsi ili kukidhi yale yamuhusuyo Mungu tu na maendeleo fungamani ya watu wa Mungu. Daima wenye mamlaka watambue kuwa Mungu siku moja anaweza kuondoa mamlaka hayo mabegani mwetu kama alivyofanya kwa Shebna na kumvika mtu mwingine mwenye kumstahili. Somo hili linaleta fundisho kwa viongozi kote ulimwenguni hasa wale wenye desturi ya kupenda kujilimbikizia mali, wala rushwa, tapeli na mafisadi wasio tanguliza mbele maslahi ya walio wengi bali kwa uchoyo na ubinafsi wamekuwa chanzo cha keki na matamu ya mataifa yao kushindwa kugawanywa na kufurahiwa na wengi. Wametengenza makundi na mipasuko ambapo kundi dogo tu la walio wachache ndio wanao nufaika na rasilimali za taifa kiasi cha wao kujiona ndio wamiliki halali wa nchi na walio wengi kusukumizwa pembeni. Uongozi wa kweli ni ule unao tafuta kuwaunganishwa wote kuwa kitu kimoja kwa upendo na mshikamano wa kidugu.

Kiri kuu ya imani ya Petro ni kazi ya Roho Mtakatifu
Kiri kuu ya imani ya Petro ni kazi ya Roho Mtakatifu   (@VATICAN MEDIA)

Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 11: 33-36). Katika somo hili, tunapewa tamati ya mafundisho ya Mtume Paulo kwa warumi kuhusu maana na namna ya kufikia wokovu. Mafundisho haya yalijikita kuelezea wokovu upatikanao kwa njia ya Kristo Yesu kwa ajili ya wayahudi na kwa wasio wayahudi. Kwa lugha yenye kufaa zaidi tungeliweza kusema kwamba, Paulo alifundisha wokovu kama Zawadi iliyowekwa tayari kwa watu wote. Kwa kweli ni lazima kukiri kuwa fundisho hilo ambalo Mtume Paulo alilitoa kwa Wayahaudi lilikuwa ni gumu. Ugumu uliletwa pia na ukweli kwamba tangu mwanzo Wayahudi walifahamu kuwa wao ni Taifa teule na hawakuwaza kuwa hata watu wa mataifa nao wangeliweza kuhesabiwa warithi wa wokovu; ndio maana iliwawia vigumu kumuelewa Mtume Paulo. Lilikuwa ni gumu kueleweka kwa watu kwa sababu ni kama lililenga kubomoa msingi wa mapokeo yaliyokuwapo lakini pia lilikuwa ni gumu kwake yeye mwenyewe Paulo kulielezea kwa ufasaha na hapa na pale ilimbidi kutumia namna nyingi na tofauti tofauti kuelezea kitu kile kile kimoja. Katika ufafanuzi wake Paulo Mtume anatoa sifa na kutukuza Hekima ya Mungu inayopita ufahamu wa kibinadamu. Hekima hiyo inajionyesha kwa kuwaokoa watu wote, yaani wayahudi waliomkataa Yesu na mataifa mengine waliohubiriwa Injili baada ya wayahudi kukataa. Kumbe hili ndilo pendo lake Baba ya kwamba wote waokoke kwa njia ya Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo.

Mwenyezi Mungu anataka watu wote waokoke
Mwenyezi Mungu anataka watu wote waokoke   (ANSA)

Injili ya dominika hii ni kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo (Mt. 16:13-20).  Katika Injili ya leo Petro anamkiri Yesu kuwa ndiye “Kristo mwana wa Mungu aliye hai”. Itakumbukwa kuwa tukio hili la kweli kihistoria na kiimani lilitokea kando ya mji wa Kaisaria Filipi, uliopo kaskazini mwa Israeli karibu na mlima Hermoni (Mt. 16:13-16; Mk. 8:27-29), ambapo Petro alikiri imani yake kwamba Yesu ndiye Masiha au Kristo. Historia inasimulia kuwa katika mji huu palikuwa na miungu mingi ya wagiriki na wa Syria. Katika mji huu Herode Mkuu alijenga hekalu akaweka sanamu ya Kaisari wa Roma aliyepaswa kuabudiwa kama mungu ishara ya shukrani kwake kwa kupewa eneo hilo alitawale. Filipo mtoto wake Herode aliongezea jina lake pakawa panaitwa Kaisaria-Filipo. Yesu akiwa katika eneo hili anawauliza wanafunzi wake swali la kutaka kujua watu wanasema yeye ni nani na wanafunzi wake wenyewe wanamchukulia kuwa ni nini? Swali hili ni la maana sana hata kwetu katika kumpenda, kumfuasa na kumwamini Kristo Yesu. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema; “Basi watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena watamwaminije kama hawajapata kumsikia wala kumjua?” (Rom. 10:14). Petro anafanya ungamo hili la imani pale Yesu anapowageukia wanafunzi na kuwauliza “na ninyi mwanisema mimi kuwa ni nani”? Ilikuwa ni muhimu kabisa kuwa baada ya kumwelezea Yesu mtazamo wa watu juu yake, wao nao waoneshe mwono wao juu yake.

Imani inasimikwa katika fadhila ya unyenyekevu
Imani inasimikwa katika fadhila ya unyenyekevu   (@Vatican Media)

Ungamo hili la imani kwa Yesu ambalo Petro analifanya, Yesu anamwambia si matokeo ya ubinadamu wake bali ni matokeo ya ufunuo kutoka kwa Mungu. Ni kwa utii huu wa Imani tunapata matunda ya utii huo kama Yesu alivyompa Petro mamlaka ya kuliongoza Taifa Jipya teule la Mungu yaani Kanisa na kumkabidhi funguo kama alama ya ukuu, mamlaka na utumishi wake, baada ya kuungama kuwa Yesu ni Masiya, Mwana wa Mungu aliye hai. Mamalaka haya ndiyo anayokuwanayo kila Baba mtakatifu anayechagualiwa kuliongoza Kanisa kwani ni halifa wa Mtume Petro. Leo tutambue kuwa Kiri hii ya imani ni ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu na sio kwamba Petro aliitambua kwa akili na uweza wake mwenyewe. Hili linatuonesha kuwa imani ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ni paji linalotoka juu ambalo ni Mungu pekee anaweza kuwajalia watu wake kwa ufunuo yaani fides quae creditur. Mwanadamu yeye huipokea tu zawadi hii pale anapofungua moyo wake na kuifungua akili yake kuangazwa na ufunuo huu yaani fides qua creditur. Tukumbuke daima kuwa kumfahamu Kristo kunahitaji unyenyekevu wa roho na kweli itokayo ndani ya mtima wetu, Kwa unyenyekevu Mungu kupitia kwa Kristo aendelee kutufunulia siri za mbingu ili tuweze kutambua nguvu zake katika maisha yetu na hivyo kuwa imara hata katika mateso. Basi tujitahidi siku zote kutafakari ukuu wa matendo ya Mungu katika maisha yetu. Tuwe watu wa sala na kumkabidhi Mungu njia zetu ili ajifunue yeye ni nani kwetu na atuongoze katika kila jambo tuweze kumpendeze Yeye siku zote za maisha yetu hata tufike kwake mbinguni. Amina.

Liturujia D 21 Mwaka A
22 Agosti 2026, 19:27