Tafuta

Mababa wa Kanisa wanasema miujiza iliyotendwa na Kristo Yesu ililenga kuwaimarisha Mitume na wafuasi wake katika imani, matumaini na mapendo. Mababa wa Kanisa wanasema miujiza iliyotendwa na Kristo Yesu ililenga kuwaimarisha Mitume na wafuasi wake katika imani, matumaini na mapendo.  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika ya 19 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukuu, Nguvu na Uweza wa Mungu

Mababa wa Kanisa wanasema miujiza iliyotendwa na Kristo Yesu ililenga kuwaimarisha Mitume na wafuasi wake katika imani, matumaini na mapendo; kuonesha uwezo wake wa Kimungu, na hatimaye, kufunua upendo na huruma kwa wenye shida. Miujiza hii ilithibitisha mamlaka yake juu ya asili, magonjwa, na hata kifo, ikawasaidia wanafunzi wake kumwamini yeye kama Mwana wa Mungu. Muujiza wale Petro anaonekana kuwa ni imani haba kama kiatu cha "raba."

Na Padre Octavian O. Hinju - Jordan University College, Morogoro (Tz).

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 19 ya mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Mababa wa Kanisa wanasema miujiza iliyotendwa na Kristo Yesu ililenga kuwaimarisha Mitume na wafuasi wake katika imani, matumaini na mapendo; kuonesha uwezo wake wa Kimungu, na hatimaye, kufunua upendo na huruma kwa wenye shida. Miujiza hii ilithibitisha mamlaka yake juu ya asili, magonjwa, na hata kifo, ikawasaidia wanafunzi wake kumwamini yeye kama Mwana wa Mungu. Masomo ya dominika hii yanatuasa na kutukumbusha kuhusu ukuu, nguvu na uweza wa kimungu katika kushughulikia shida na mahangaiko ya roho za wanadamu na umuhimu wa kumtegemea Yeye peke yake ili aweze kuwaokoa. Mababa wa Kanisa wanafundisha kwamba muujiza wa Bwana wetu Yesu Kristo na Mtume Petro kutembea juu ya maji unaashiria umungu wa Kristo, mfano wa maisha ya kiroho na umuhimu wa imani pasipo mashaka. Msisitizo mkubwa unaoletwa kwetu siku ya leo ni kuhusu ustahimilivu wa Mungu katika kujidhihisha na kujitoa kwake kwa mwanadamu mwenye mahangaiko lukuki. Hakika mahangaiko yamekuwa ni moja ya sehemu ya vikwazo vinavyo mtatiza sana mwanadamu. Hili linajidhihirisha jinsi Mungu alivyomtokea mtumishi wake Nabii Eliya na kuongea naye katika upepo na hali ya utulivu huko mlimani Horebu na jinsi mwanae mpenzi Bwana wetu Yesu Kristu alivyotuliza dhoruba kwa nguvu na uweza wa neno lake katika ziwa Galilaya na kuwaokoa wanafunzi wake. Mtume Petro kama mwakilishi wa wanadamu wenye shauku ya kumfuata Kristu katika njia yake ya wokovu lakini bado hofu na mashaka vinawasonga anaomba naye aweze kutembea juu ya maji, lakini kwa sababu ya pupa na papara na kuona kwake mashaka baada ya Yesu kumruhusu kutembea juu ya maji alianza kuzama. Hili ni ashirio la uhaba wa imani na kushindwa kutambua ukuu na umungu wa Kristu. Pengine haya ni matokeo pia ya ile hali ilyomo ndani ya mwanadamu ya kumfuata Kristu na mioyo iliyogawanyika. Yaani kuwa pamoja na Yesu na wakati huo huo bado unatamani kukumbatia malimwengu.

Mtumbwi umkiteseka kwenye mawimbi mazito ya bahari
Mtumbwi umkiteseka kwenye mawimbi mazito ya bahari   (AFP or licensors)

Somo la kwanza ni kutoka kitabu cha kwanza cha Wafalme (1Fal 19:9a, 11-13a). Somo hili linaloelezea jitihada ya Nabii Elisha kushindwa kuwarudisha Waisraeli katika njia za Mungu. Nabii Elisha anakata tamaa na anakwenda kukutana na Mungu katika mlima wa Agano ulioitwa Horebu. Kinachojiri katika simulizi hili ni kwamba Nabii Eliya alikuwa amemaliza kupambana na manabii wa miungu ya kipagani yaani miungu ya Baali na kuwashinda katika mlima Karmeli. Tukio hilo lilimjengea uadui mkubwa hadi akatishiwa kuuwawa. Akakimbia kuinusuru nafsi yake lakini pia kukimbia kwake huku kuliashiria pia kukata tamaa. Nabii Eliya hakuelewa ni kwa nini baada ya kumtolea Mungu ushuhuda mkubwa namna hii, Mungu hamhakikishii ulinzi wala usalama na tena badala ya kupongezwa na kumwagiwa sifa kedekede machoni pa watu yeye anaambulia kejeli na vitisho vya kutaka kuuwawa. Nabii Eliya alifika katika mlima wa Mungu ulioitwa Horebu akamsubiri Mungu atokee kama alivyokuwa amemwahidi. Ukapita upepo mkali unaopasua milima na miamba lakini Bwana hakuwamo katika upepo huo, likapita tetemeko, ukaja na moto lakini Bwana hakuwapo katika vyote hivyo. Hatimaye ikaja sauti ndogo na ya utulivu, upepo wa kisulisuli, na humo ndimo alimokuwamo Bwana. Kumbe tunalopaswa kujifunza hapa ni kuwa Mungu hajionyeshi katika kelele na tetemeko kama alivyofikiri Nabii Eliya naye si Mungu mwenye kutisha na kuogofya sana, bali wakati utimiapo Mungu atawakomboa watu wake Kadiri ya mpango na mapenzi yake. Somo hili linatuonesha namna Mungu anavyotenda kazi zake na namna ambavyo Mungu anajidhihirisha kwetu. Ni utendaji wa utulivu, Subira na unyenyekevu, usiotafuta kujionesha au kama tunavyoweza pia kusema, ni utendaji usio wa kelele na maneno mengi.

Kuzama kwa Mtume Petro ni kielelezo cha imani haba
Kuzama kwa Mtume Petro ni kielelezo cha imani haba   (ANSA)

Utendaji wa Mungu haujipambanui katika kupasua miamba, kuleta mabadiliko ya haraka kwa njia za miujiza yenye kutisha na kuvutia halaiki, bali una njia na namna yake ya pekee na ya ajabu. Kumbe nasi kwa kufuata mfano wa Nabii Eliya kama inavyo elezwa katika somo la kwanza; tutambue kuwa tutakataliwa, kudharauliwa na kuudhiwa hata kupelekea kuuwawa kwa sababu ya ukweli tunao usimamia. Pili, tusikate tamaa hata mara moja hasa pale inapoonekana kuwa jitihada, bidii na shauku zetu za kuleta mabadiliko ya kweli zinagonga mwamba na kupuuzwa na jamii tunayoitumikia. Tufahamu kwamba uongo hata usemwe na watu wengi bado haubadiliki kuwa ukweli na ukweli hata ukisemwa na mmoja bado hauwezi kugeuka kuwa uwongo. Hivyo wingi si hoja. Katika kupuuzwa tutambue kuwa bado yupo Mungu naye hakawii kujibu bali anao muda muafaka  wa kuhidhirisha ukuu na uweza wake. Tusimpime Mwenyezi Mungu kwa hisia na msukumo wa watu bali kwa Imani Thabiti tumruhusu ajifunue kwetu.  Ni kweli kuwa zipo nyakati tunafadhaishwa na karaha za watu tunaotumwa kwao na Mungu kuwahudumia kiasi cha kujibu kama Eliya “Naona uchungu na wivu, ewe Mungu wa majeshi, kwasababu watu wa Israeli wamevunja agano lako, wakazibomoa madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga; ni mimi tu niliyebaki, nami pia wananiwinda, waniue!” (1Waf. 19:10); tufahamu kuwa Mungu ni mpole na mvumilivu naye kwa upendo anatutuliza nafsi zetu kwa kututia nguvu. Kama ambavyo Mungu aliongea na Nabii Eliya kirafiki; kwa sauti ya upole na utulivu na kumuhakikishia kuwa yupo pamoja naye hata kama yuko kimya basi vivyo hivyo kwetu Mungu ni Baba anaye safiri nasi ili kutuchunga kutulinda na kutuongoza. Mungu alimwonyesha Eliya kuwa hawakomboi watu kwa kuwapatisha kwenye tanuru la moto, tetemeko, upepo mkali, au kwa njia ya kuwatesa au kuwauwa. Yeye si Mungu wa kisasi bali ni Mungu wa msamaha na amani. Katika hali hii, imani ya nabii Eliya kwa Mungu iliimarika, akawa na ujasiri wa kusimama mbele zake na kumshuhudia kuwa Yeye ni Mungu wa kweli ndiyo maana anakumbukwa kama nabii mkubwa zaidi baada ya Musa. Huyu ndiye Nabii Eliya ambaye Pamoja na Musa walitokea na kuongea na Yesu kuhusu kifo chake katika tukio la kugeuka sura kwa Yesu mlimani Tabor (Mt. 17:3). Kumbe basi kama ambavyo imani ya Eliya kwa Mungu ilimfanya awe mwaminifu katika kazi aliyopewa nasi tumwombe Bwana atupe Imani kama hivyo ili katika kuishi kwetu tumjue Mungu, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake mbinguni.

Mtumbwi ni alama ya Kanisa Sakramenti ya Wokovu
Mtumbwi ni alama ya Kanisa Sakramenti ya Wokovu

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 9:1-5). Katika somo hili Paulo anatoa onyo kuhusu ukaidi, kiburi na majivuno ya mwanadamu. Kwa kawaida kabisa kiburi huja kabla ya anguko. Akiwatolea mfano wayahaudi, Paulo anaeleza kwamba walikirimiwa kipekee sana na Mungu. tena kwa njia ya manabii walipewa Zawadi ya Neno la Mungu. Zawadi iliyo bora ni kwamba Masiha yaani Neno wa milele alizaliwa kwao, lakini Wayahudi walimkataa. Tendo hili lilimhuzunisha sana Mtume Paulo, kwani Yesu ndiye njia pekee ya wokovu. Yamkini hata sisi kwa nyakati tofauti tofauti kutokana na kukumbatia dhambi tumemkataa Yesu, leo ni nafasi nyingine ya kuchunguza mienendo ya maisha yetu kuona ni wapi na kwa namna gani tumemkataa Kristu na kwa sakramenti ya kitubio na maungamo tupatane naye.

Mtumbwi ni alama ya Kanisa, Sakramenti ya umoja na wokovu wa watu wote
Mtumbwi ni alama ya Kanisa, Sakramenti ya umoja na wokovu wa watu wote   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo (Mt. 14:22-33). Katika sehemu hii ya Injili ya leo, tunasimuliwa jinsi Yesu alivyotembea juu ya maji ili kudhihirisha umungu wake. Itakumbukwa kuwa masimulizi ya kibiblia katika Agano la Kale yanatanabaisha kwamba, watu walisadiki kuwa ni Mungu tu ndiye mwenye mamlaka yote juu ya maji kama alivyofanya kwenye bahari ya shamu alipowavusha Waisraeli pakavu ili kuwaokoa dhidi ya mkono wa Farao na majeshi yake yote, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kutembea juu yake bila kuzama. Katika tukio hili, wanafunzi wa Yesu wanapanda mashua na kuanza safari wakati yeye bado angali mlimani akisali kama ilivyokuwa desturi yake. Anapomaliza kusali anawafuata akitembea juu ya maji. Petro anapomtambua na kujihakikishia kuwa ni Yeye, anaomba naye atembee juu ya maji. Anaanza kweli kutembea lakini muda tu anazama kwa hofu. Petro alijawa na hofu kutokana na Imani iliyokuwepo miongoni wa wayahudi kuwa mizimu na majini ndio wanaotembea juu yam aji baharini, hvyo alidhania Yesu ni mzimu. Yesu analitafsiri tukio hili kama ukosefu wa imani na anamuuliza Petro, “ewe mwenye imani haba kwa nini ulitia shaka.?” Muujiza huu una mafunzo mengi yanayoweza kutusaidia kuelewa vema. Tuyaangalie maji kama alama ya nguvu za giza na nguvu za uharibifu. Kwa tendo la Yesu kutembea juu ya maji ni ishara kuwa Yesu ana nguvu kuliko nguvu hizo za uharibifu zinazowakilishwa na maji. Petro anapoomba na yeye kutembea juu ya maji Yesu anamwambia njoo. Na kwa neno hilo la Yesu Petro kweli anatembea juu ya maji. Yesu hapa anapenda kutuonesha kwa kuwa Neno lake hata sisi wanafunzi wake tutakuwa na uwezo wa kuzishinda nguvu za giza na za uharibifu.

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wote
Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wote   (@Vatican Media)

Kitendo cha Petro kuzama kwa hofu ni mwaliko wa wafuasi wa Yesu kuzishinda hofu za kiimani na hofu za kimaisha zinazoweza kuwapoteza kutoka katika kulishika Neno la Yesu na hivyo kuangamia. Mtumbwi ni alama ya kanisa lililo daima safarini. Yesu anapoingia mtumbwini, hapo hapo upepo mkali na mawimbi yanakoma. Ni mwaliko wa Kanisa kuendelea kuutunza utambulisho wa Kristo ndani yake ili kuyashinda mawimbi na misukosuko katika safari yake ya wokovu. Kumbe basi kutembea kwake Yesu juu ya maji kulikuwa ni hakikisho kwa wakristo wa mwanzo lakini hata kwetu sisi kwa zama zetu hizi kuwa Yesu ni Mungu. Naye Petro kwa tendo la kutembea juu ya maji na kuanza kuzama ni ashirio la uchanga katika imani, hofu na mashaka juu ya uweza wa Mungu. Tutambue pia sisi nasi tukikosa imani tutazama katika Bahari hii yaani ulimwengu mamboleo. Yesu anapotembea Juu ya Maji anataka kuonesha mamlaka na uwezo wake juu ya nguvu za asili, na tunafundishwa kuwa na imani thabiti badala ya kuzama kwa sababu ya mashaka na hofu. Tunapo endelea kuyatafakari hayo, tusali kumwomba Kristu atuongezee imani tukisema; Ee Mungu Mwenyezi wa milele, nijalie siku zote mimi mtumishi wako kuwa na imani thabiti, uniongezee zawadi hiyo ya imani ili nisiongozwe na mashaka. Imarishwa zawadi hiyo ya imani itokayo kwako ili niwezeshe daima kukutegemea wewe hata nisipokuona kwa macho yangu. Fukuza woga ndani mwangu na unipe siku zote moyo wa uchaji, subira na utulivu wa nafsi yangu. Amina. Tumsifu Yesu Kristo.

Liturujia D 19 Mwaka A

 

08 Agosti 2026, 15:53