Tafakari Dominika ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa: Huruma, Upendo na Ukarimu Mkuu
Na Padre Octavian O. Hinju, Jordan University College Morogoro, Tanzania.
Ujumbe wa masomo ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa unalenga kusisitiza juu ya ukarimu, upendo na huruma ya Mungu kwa wanadamu. Kwa nyakati tofauti tofauti, Mababa wa Kanisa wameendelea kufundisha kwamba ukarimu ni kielelezo halisi cha imani na upendo kwa Kristo Yesu unaoonekana kupitia kuwapokea maskini, kuwajali wahitaji na kufungua milango kwa wageni. Kutoka karne ya kwanza, Mababa wa Kanisa wanatambua ndani ya maskini namna ya upendeleo wa kipekee wa kumfikia Mungu. Ukarimu unaotolewa kwa wenye shida haukutazamwa kama fadhila ya kimaadili, bali ulikuwa ni kielelezo wazi cha imani juu ya Neno aliyefanyika mwili. Masomo ya dominika hii yanatuasa na kutukumbusha kuhusu ukarimu, upendo na huruma ya Mungu kwa wanadamu. Katika Waraka wake wa Kitume Dilexi Te unaotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kama “Nimekupenda” uliosainiwa mnamo Oktoba 4, 2025, na kuchapishwa tarehe 9 Oktoba 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV akinukuu mafundisho ya Mababa wa Kanisa kuhusu ukarimu, upendo na huruma ya Mungu kwa wanadamu hasa masikini anafundisha akisema kwamba, ukarimu ni kielelezo halisi cha imani na upendo kwa Kristo unaoonekana kupitia kuwapokea maskini, kuwajali wahitaji na kufungua milango kwa wageni. Mababa wa Kanisa walihusiana kwa karibu sana na maskini.
Kutoka karne ya kwanza, Mababa wa Kanisa wanatambua ndani ya maskini namna ya upendeleo wa kipekee wa kumfikia Mungu. Ukarimu unaotolewa kwa wenye shida haukutazamwa kama fadhila ya kimaadili, bali ulikuwa ni kielelezo wazi cha imani juu ya Neno aliyefanyika mwili. Historia ya Maandiko Matakatifu licha ya mafunzo yake mengi na mazuri bado haiachi kuibainisha fadhila hii ya ukarimu kama mwelekeo wa huruma na upendo wa kimungu. Katika Kitabu cha Kwanza cha Wafalme 1 Fal 17:8-16, tunasimuliwa kuhusu mjane wa Sarepta ambaye kwa tendo moja la ukarimu yeye na nyumba yake walibarikiwa. Ni ukarimu ndio uliomfanya Abrahamu baba wa Imani ahakikishiwe kuwa atapata mrithi kutoka katika tumbo la mkewe Sarah, “Mmoja wao akasema, “Hakika nitakurudia wakati kama huu mwakani, na mkeo Sara atakuwa na mtoto wa kiume.” Sara alikuwa huko nyuma mlangoni mwa hema, akisikiliza (Mwz. 18:10). Naye mwanamke Mshunemi (2 Fal 4:1-37), alibarikiwa kwa ukarimu wake kwa Nabii Elisha naye alijaliwa mtoto aliyefanyika furaha kwa familia nzima. Ukarimu ni matokeo ya upendo unao hurumia na kujali. Bwana wetu Yesu Kristu ni mfano na kielelezo Thabiti cha huo ukarimu kwani Yeye pasi na kipimo alitupenda hata akatuhurumia hivyo kutukarimu kwa Zawadi ya ajabu ya mwili na damu yake azizi ndiyo Ekaristi Takatifu, “Alikuwa amewapenda sana wafuasi wake hapa duniani, akawapenda hadi mwisho (Yoh. 13:1), “Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu (Mt. 26:26).
Ukarimu wa Mungu kama Baba na Bwana wa historia, mwingi wa huruma na upendo kwa mwanadamu unafumbatwa katika upendo wake wa kumtoa Mwanae wa pekee ili kila amwaminiye na kumfuata apate uzima wa milele (Yoh.3:16; 17:3, Flp. 2:6-11). Anayemtendea mwenzake kwa ukarimu, Mungu pia atamtendea kwa ukarimu kwa sababu kipimo tupimacho ndicho tutakachopimiwa. Ukarimu, upendo na huruma kuu ya Mungu ndio hasa mwelekeo wa masomo yanayoongoza tafakari yetu katika Dominika hii ya 18 ya Mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 55:1-3). Katika somo hili tunapewa mwaliko wa kuingia katika Ufalme wa Mungu unaofananishwa na karamu nono pasipo malipo. Hili tendo la pekee lenye kusheheni upendeleo mkubwa kwani Mwenyezi Mungu pasi na mastahili yetu kutoka na hali zetu za dhambi bado anaona tunastahili kujumuika naye katika ufalme wake wenye raha zisizo na mwisho. Mwaliko wa kuingia ili kufurahi katika karama yenye vinono, ni ujumbe wa matumaini kwao wote walio kata tamaa na kupondeka moyo kutokana na changamoto za maisha. Hali hii iliwakumba na kuwahangaisha sana wana wa Israeli walipo kuwa utumwani. Walijiona kuwa ni kundi lisilo na maana tena na thamani yao imepotea machoni pa Mungu.
Katika hali hiyo Mungu anawapelekea ujumbe wa faraja. Kwa kinywa cha Nabii Isaya anawafariji watu wake akiwalika wajongee katika karamu ya meza ya Bwana ambayo kuna vyakula na vinywaji tele vilivyoandaliwa kwa ajili yao akisema: “Kila aonaye kiu, njooni majini, naye asiye na fedha; nunueni mle; naam, njoni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila thamani. Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema. Na kujifurahisha nafsi zenu, kwa unono, tegeni masikio yenu, na kunijia. Sikieni, na nafsi zenu zitaishi, nami nitafanya nanyi agano la milele, naam, rehema za Daudi zilizo imara.” Baadaye Wayahudi waliruhusiwa kurudi Yerusalemu na utabiri wa Nabii Isaya ulitimia hekalu lilipojengwa nao wakaanza kumwabudu Mungu wa kweli.Pengine hata sisi nyakati fulani katika safari ya maisha tumejikuta katika hali ya sintofahamu kiasi cha kukata tamaa. Tupokee kwa moyo wa shukrani na ibada mwaliko huu wa kuingia katika karamu yenye vinono ambayo Mungu mwenyewe kwa njia ya Kristu Bwana wetu ameiandaa na kuitimiza kwa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu ambaye kwa upendo wake kwetu anatoa maisha yake kulipia gharama ya adhabu ya dhambi zetu na kujitoa mwenyewe kuwa chakula chetu cha kiroho yaani Ekaristi Takatifu. Yesu mwenyewe anasema; “Mimi ni mkate wa uzima ulioshuka kutoka mbinguni” (Yoh. 6:51) na maji ya uzima wa milele naye anayenywa hatasikia kiu kamwe tena (Yoh. 4:10,14). ili pamoja na Malaika na Watakatifu wote tuweze kuingia na kufurahi pasi na mwisho.
Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8: 35, 37-39). Katika somo hili Mtume Paulo anasisitiza jinsi pendo la Mungu lilivyodhihirishwa kwetu katika Kristo Yesu. Kumbe tukikubali kushikamana na pendo hili, basi hakuna hatari wala matatizo yanayoweza kututenganisha na Kristo aliye upendo halisi. Hapa Mtume Paulo anaorodhosha matatizo yanayoweza kutupata endapo tuta tengana na pendo la Kristu. Mtume Paulo anataja akisema “wala dhiki, wala shida, wala adha, wala njaa, wala uchi, wala hatari, wala upanga, wala mauti, wala uzima wala malaika, wala wenye mamlaka wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Kinyume na hapo tutaendelea kuwa wahanga wa hayo yote kwani Kristu hakai tena ndani mwetu nasi tumemwacha mbali na roho zetu. Tumwombe Kristu ashinde nasi ili tuweze kujihakikishia ulinzi na usalama utokao kwake.
Injili inayoongoza tafakari yetu ya siku hii ya leo ni kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo (Mt.14:13-21). Mwinjili Mathayo anatueleza kuwa Kristo ni Masiha, mfano wa Musa aliyewalisha Waisraeli; tena inadokeza matayarisho ya karamu ya Ekaristi takatifu; na mwishowe inaonyesha upendo wa Mungu anayetualika wote kwenye karamu mbinguni. Kumbe ukarimu, upendo na huruma kuu ni matendo ya kiekaristi kwani karamu ya Ekaristi Takatifu ni ishara ya upendo wa Mungu kwetu unaojidhihirisha kwa njia ya Yesu anayetualika sote kwenye karamu ya mbinguni kwa kuibariki na kuimega mikate mitano na samaki wawili na watu wote wakala wakashiba. Kwa njia ya Yesu huruma ya Mungu inayofumbatwa katika upendo inajifunua kwa Yesu kuwaonea huruma kwa watu walio kama kondoo wasio na mchungaji hivyo anawalisha kwa neno lake kwa mafundisho yake, anawaponya magonjwa yao, anawashibisha njaa zao kwa kuwapa chakula kwa muujiza wa kuongezeka idadi ya mikate na samaki. Muujiza huu ni mwangwi wa kuwekwa kwa Ekaristi Takatifu katika karamu ya mwisho, kwa sababu matendo haya mawili yanafanana: “Kisha atachukua mikate mitano na samaki wawili, akainua macho yake mbinguni na kubariki, akaimega na kuwapa wafuasi wake nao wakawapa makutano” (Mt. 14:19). Wakati walipokuwa wanakula, Yesu alichukua mkate na baada ya kuubariki, aliumega na kuwapa wanafunzi wake akisema; “Twaeni, mle, huu ni mwili wangu” (Mt. 26:26).
Nasi ili tuweze kuguswa na kuonja hakika ya ukarimu wa Kristu basi tutambue kwamba Katika Ekaristi Takatifu fumbo la Ukombozi wetu linawekwa hai na kufikia kilele katika sadaka ya Bwana: “huu ndio Mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu na hii ndiyo Damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu”, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” (Luka 22:19-20). Sisi sote tunaalikwa kwenye karamu hii ili tuweze kushiriki katika uzima ule ule wa Kristo Yesu. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Pia huitwa Misa Takatifu, karamu ya Bwana, kumega mkate, kusanyiko la Kiekaristi, ukumbusho wa mateso kifo na ufufuko wa Bwana, Sadaka Takatifu ya Misa, Liturujia Takatifu, Sakramenti Takatifu sana ya Altare na Komunyo Takatifu. Ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo waamini humpokea Kristo na roho hujazwa neema na kupewa amana ya uzima wa milele (KKK 1322 – 1323, 1409). Ekaristi ni kitovu na kilele cha maisha ya Kanisa, kwa kuwa kwayo Kristo anachagamana na Kanisa lake na waamini wake wote na sadaka ya sifa na shukrani iliyotolewa mara moja Msalabani kwa Mungu Baba. Kwa sadaka hii anamimina neema za wokovu kwa mwili wake ambao ni Kanisa (KKK 1407). Papa Leo XIII anasema Ekaristi Takatifu ni roho ya Kanisa (Denz.3364). Ni Sakramenti ya umoja na upendo, kimsingi, Ekaristi ni kiini kamili katika Kanisa, na Kanisa haliwezi kitu pasipo hiyo. Kwa sababu ni Kristo mwenyewe anayejitoa kweli kama sadaka kwa ajili ya Kanisa katika Ekaristi Takatifu na ni katika Ekaristi Kanisa hufikia uhalisia wake wa juu wa asili yake, yaani, kuwa linaonekana, la daima, na alama wazi ya neema ya wokovu ya Mungu iliyopo duniani kupitia Kristo. Tumsifu Yesu Kristo.