Tafuta

Sr. Bonifasia Sebastian Ngonyani OSB wa Shirika la Masista Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing, Ndanda, Mtwara Tanzania, tarehe 15 Agosti 2026 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Maisha ya kitawa. Sr. Bonifasia Sebastian Ngonyani OSB wa Shirika la Masista Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing, Ndanda, Mtwara Tanzania, tarehe 15 Agosti 2026 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Maisha ya kitawa. 

Sr. Bonifasia Sebastian Ngonyani, OSB: Jubilei ya Miaka 25 ya Maisha ya Kitawa

Ni Ibada iliyoadhimishwa kwa uchaji na heshima, alama ya neema na baraka kutoka kwa Mungu. Hii ni safari ya miaka 25 ya kukubali na kuitikia wito wa maisha ya kitawa, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyeanza hija ya utume wake tangu pale alipopashwa habari kwamba, angekuwa ni Mama wa Mungu, akathubutu kusimama chini ya Msalaba na kushuhudia mateso, kifo na hatimaye ufufuko wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, aliyemstahilisha utukufu mbinguni!

Na SR. Bonifasia Ngonyani OSB. – Roma.

Sr. Bonifasia Sebastian Ngonyani wa Shirika la Masista Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing, Ndanda, Mtwara Tanzania, tarehe 15 Agosti 2026 wakati wa Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, ameadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipoweka nadhari za kwanza za maisha ya kitawa, Ibada ya Misa takatifu imeongozwa na Padre Sakubita Lawrence Like, O.M.I. Ni Ibada iliyoadhimishwa kwa uchaji na heshima kubwa kadiri ya Mapokeo ya Wabenediktini, alama ya neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Hii ni safari ya miaka 25 ya kukubali na kuitikia wito wa maisha ya kitawa, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyeanza hija ya maisha na utume wake tangu pale alipopashwa habari kwamba, angekuwa ni Mama wa Mungu, akathubutu kusimama chini ya Msalaba na kushuhudia mateso, kifo na hatimaye ufufuko wa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, aliyemstahilisha kwa zawadi ya kupalizwa mbinguni mwili na roho. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mintarafu Maandiko Matakatifu, Jubilei ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema na baraka za kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Ni wakati murua sana wa mapumziko; muda wa kujichotea nguvu na neema pamoja na kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Ni wakati wa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Watawa Wamisionari wa Shirika la Wabenediktini wa Tutzing, Ndanda, TZ.
Watawa Wamisionari wa Shirika la Wabenediktini wa Tutzing, Ndanda, TZ.

Mimi naitwa SR. BONIFASIA NGONYANI OSB, wa Shirika la Wamissionari wa Benediktini wa Tutzing Ndanda Mtwara, Tanzania. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya huruma ya Mungu: Zaburi 145:8-13, Neno la Mungu linathibitisha kuwa yeye ni mwingi wa rehema, hakasiriki ovyo, na ni mwema kwa kila mtu. Safari ya maisha yangu ya wito miaka 25. kutoka mwaka 1989- 2026. Maisha yangu yanaongozwa na maneno haya: Kwa Huruma ya Mungu tuu.” kutoka  Zaburi 145:8-13,hapo juu yasemayo ‘‘Neno la Mungu linathibitisha kuwa yeye ni mwingi wa rehema, hakasiriki ovyo, na ni mwema kwa kila mtu.’’ Pia kutoka Tito 3:5: "Si kwa matendo ya haki tuliyoyatenda sisi, bali kwa rehema yake alituokoa..." Safari ya maisha yangu ya wito yalianzia katika Kijiji kidogo sana ambacho hakisikiki sana, nacho ni kijiji cha MAWA katika Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma (Songea).  Nimezaliwa kwa wazazi: Sebastian Ngonyani na Dionisia Fussi Mama yangu ambaye ametangulia mbinguni. Mimi ni mtoto wa tatu kati ya watoto tisa na sasa tumebaki watoto saba na baba yetu.

Sala, tafakari na Sakramenti ni mihimili mikuu ya maisha ya kitawa
Sala, tafakari na Sakramenti ni mihimili mikuu ya maisha ya kitawa

MAISHA YA WITO; Safari ya wito wangu ulianza kuchipuka moyoni mwangu nikiwa msichana mdogo, pole pole ulikua kwa kupaliliwa na watawa wa Hanga Monasteri ambao ni jirani zetu kule kijijini. Nilipo maliza shule ya msingi wakati ule wa miaka ya 1984 haikuwa rahisi sana kufaulu na Kwenda secondari nilibahatika Kwenda domestic au maarifa ya nyumbani.  Wakati ule mashirika yalikuwa yanatafuta mabinti kuingia utawani mara moja masista wengi wa mashirika mbali mbali walitembelea domestic yetu iliyo kuwa inaongozwa na mtawa wa Hanga monasteri. Basi nami nilisikia mvuto zaidi na sharika la wamisionari Wabenediktini wa Tutzing Ndanda. hatimaye mwaka 1989. mimi na wenzangu wanne tulianza safari ya kwenda Ndanda Misioni.  Rasmi kwa kuanza maisha ya kitawa. Tulipokelewa katika chuo cha Uunguzi kwa muda, tulikaa hapo maana Masista walikuwa wanasimamia chuo hicho. Na baada ya muda tuliweza kupata mahali pa kuishi. Katika nyumba ya Ndanda bado hapakuwa na nyumba ya malezi, bali nyumba ya malezi ilikuwa Nairobi. Mara moja tulitembelewa na Baba Askofu wa jimbo kuu la Songea, Yakobo Yofunani Komba. Alipo ongea na sisi mabinti, alisema: ‘‘ninyi mabinti wote mpo hapa lakini kila mtu ana njia yake Mumgu amemwandikia wengine watachukua muda mrefu wengine wataenda haraka.’’  Maneno haya yalikuja kutimia katika maisha yangu, mwendo wa maisha ukaanza kwa kadiri ya uwezo wetu wa kuelewa, kipaki, na afya. Katika kuendelea na majiundo ya utawa wengine waliweza kuonyesha vipaji tofauti na kupelekwa shule mbali mbali. 

Ibada imeemdeshwa kwa unyenyekevu na uchaji
Ibada imeemdeshwa kwa unyenyekevu na uchaji

Mimi ni kati ya wale waliokwenda na mwendo wa taratibu, hatimaye kwaka 1990 nilipelekwa Nachingwea mkoa wa Lindi kusomea uuguzi wakati ule waliita MCH, (Mother and Child Health Care) kwa miaka miwili na mwaka 1993 nikawa kati ya miongoni mwa Waaspiranti ambao walichaguliwa kwenda kuanza maisha ya kitawa huko Nairobi Novisiate. Wakati tumefika kule baada ya muda mfupitu, afya yangu ikaaza kuteteleka, na mwaka1994 nilirudishwa Ndanda Shirikani kwa tatizo la kiafya, nilikaa Ndanda baadaye wakubwa wakaona kuwa siwezi kwenda tena Nairobi kwa ajili ya kuendelea na malezi. Mungu kwa huruma yake hakutaka wanirudishe nyumbani. Na nilikuwa na afya dhaifu hawakuona kuwa ni sahihi niendelee na malezi pale shirikani Ndanda wakaona kuwa niende kusoma secondari maana kule nyumbni nilisoma tu Maarifa ya Nyumbani basi nikajiunga na kidato cha pili maana nilikwa na umri mkubwa.  Baada ya miaka miwili nilifanya mtihani wa kidato cha nne na kupata cheti mwaka 1998. Wakati ule kulikuwa na Kundi linajiandaa kuingia unovisi pale shirikani Ndanda.  hivyo Mungu kwa huruma yake baada ya kuona maisha ya mtoto wake, wakubwa wakanikubalia niingie katika Kundi lile la wapostulanti ambao walikuwa wawili na mimi wa tatu. Kwa kweli ni siku ambayo niliisubiri kwa hamu kubwa sana. Nilikuwa naumwa shingo, mgongo, baada ya Habari ile njema, baada ya muda nilipona, ugonjwa ukapotea. Tulipo kuwa mwaka wa kwanza wa unovisi mwenzetu mmoja aliona maisha ya kitawa hayakuwa yake. Aliamua kurudi nyumbani. Tukabaki wawili. Mwaka 2001 kwa huruma ya Mungu tulifunga nadhiri za kitawa. Kusherekea Jubilei tunahesabu kutoka pale tulipofunga nadhiri za muda. Hivyo kwa neema na huruma ya Mungu leo tarehe 11 Agosti 2026 nasherekea Jubilee ya Huruma ya Mungu kwangu, kwa kunikirimia mema mengi sana nisiyo stahili. Nina neno moja tu kubwa kwangu namwambia: ‘‘Mwenyezi Mungu Asante sana.’’

Watawa Wakishuhudia Sr Bonifasia akirudia tena nadhiri zake
Watawa Wakishuhudia Sr Bonifasia akirudia tena nadhiri zake

Katika safari ya maisha yangu nimejifunza mambo mengi sana nitayataja machache. Mosi: Njia za Mungu kwangu hazichunguziki: kama mtume Paulo kwa Warumi 11:33-34 asemavyo: Mtume Paulo anashangaa na kusema, "Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!" nami leo na sema njia za Mungu kwangu ni za ajabu siwezi kamwe kueleza wala kuelewa. Ila leo na sema tu Mungu asante sana! Maana siku zote amenitunza, ameniongoza na kunilinda, mara nyingi nilijikwaa na kuanguka lakini Mungu kwa wema wake ameniinua na kuniongoza nipo hadi leo. Pili. Nimejifunza sana kuwa MVUMILIVU. Mwinjili LUKA 21:19. anasema “Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu". Kwa hakika hili nadhibitisha sana katika maisha yangu. Ni uvumilivu tu umenifanya leo nimtukuze Mungu, nimshuru Mungu. Uvumilivu ni kama Silaha: Mwinjili Luka Anatuhakikishia kuwa imani thabiti na subira katika nyakati za dhiki ndio itakayowasaidia kushinda na kulinda wokovu na uzima wa milele wa roho zao. Pia kupata Ushindi wa Kiroho: Kusimama imara katikati ya majaribu huleta wokovu wa mwisho. Tatu: Kumtumainia Mungu: mara nyingi niliona Barabara ya maisha yangu ilikuwa haisomeki wala haieleweki. lakini kitu kimoja ambacho sikutaka kinipoteee katika maisha yangu ni kuwa na tumaini kwa Mungu. Kama maandiko matakatifu yanasema kwamba kumtumaini Mungu huleta amani na nguvu. Mungu ametuahidi wakati ujao mzuri na wa matumaini, na anatutia moyo kumtegemea Yeye hasa nyakati za shida ili nafsi zetu zisifadhaike hayo maneno leo mimi nayatolea shuda kuwa ni kweli. Na Zaburi ya 42:11: Inatukumbusha kujiuliza kwa nini tunasononeka na badala yake kuweka tumaini letu kwa Mungu, aliye mkombozi wetu. Kusononeka ni sehamu ya maisha hasa maisha yanapoenda namna si nipendaavyo inaleta uchungu, maumivu, wasiwasi n.k. lakini tujifunze kubaki na Mungu. Pia Zaburi ya 62:5-8: Inasisitiza kumngojea Mungu kwa utulivu, kwani Yeye ndiye mwamba na ngome yetu. Tafakari ya maneno haya yamenitia nguvu daima katika maisha yangu. Warumi 15:13: "Mungu wa tumaini" anijaze furaha na amani tele katika maisha yangu yote.

Maisha ya kitawa yanahitaji sadaka na kujitoa bila ya kujibakiza.
Maisha ya kitawa yanahitaji sadaka na kujitoa bila ya kujibakiza.

Nne: Kuwa mtu wa sala: Maisha ya wito ni maisha pekee sana, msingi wake ni sala. Wito unahitaji kupaliliwa, unahitaji uangaliwe na utuzwe na kitu kikubwa ambacho kinatunza wito ni kuwa na mahusiano na Mungu kujiunganisha na Mungu daima hili si tendo rahisi. Mara nyingi nimeonja maisha magumu sana lakini kamwe sikuacha kusali. Wakati mwingine sala za Pamoja yaani sala kwenye jumuiya zinasaidia sana. sisi watawa kuna wakati watawa wenzako wanakubeba na kukuombea, na kuna wakati nahisi hata sala zangu Mungu hasikilizi lakini kamwa sikuancha kusali, kama mtume Paulo asemavyo dumu katika maombi (sala): inahimiza "kusali bila kukoma" (1 Wathesalonike 5:17) na kudumu katika maombi kwa shukrani. Tano: Katika maisha nimejifunza na naendelea kujifunza kuwa mapenzi ya Mungu yatimizwe hii lugha wakati mwingine ni ngumu sana kuipokea hasa pale ambapo mimi nilitamani Mungu aharakishe mambo, lakini njia zangu si njia za Mungu kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya 55:8-9, ambapo Mungu anatueleza kwamba hekima, mipango, na asili yake viko juu sana kuliko ufahamu na uwezo wa kibinadamu. Mstari huu unasema mawazo ya mwanadamu ni tofauti sana na njia za Mungu. Hii mara nyingi nimejikuta nagombana na Mungu kwa nini hasikilizi sala zangu, maombi yangu, lakini Mungu ameniongoza na anaendelea kuniongoza kwa namna vile yeye anapenda, kwangu natakiwa mara zote nidumu na naendelea kudumu katika Imani. Imani kwa mwonekano wa nje ni kama kitu rahisi kuiishi lakini, kwangu kwenye mazingira mengine ni ngumu sana, kumtumainia Mungu hasa pale ambapo maisha ni magumu au hayaendi kulingana na mimi. Sasa nimewezaje? Kwa neema zake tuu. Na leo ninasema bila neema ya Mungu mimi nisingekuwa hapa nilipo. Imani kwangu ni kung’ang’ana na kumshikilia Mungu hata kama mambo hayaendi na haonekani kwa macho. Na katika Bibilia inasemwa imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo na uthibitisho wa mambo yasiyoonekana. Ni uamuzi thabiti wa kumtumaini Mungu na ahadi zake, hata pale ambapo hatuoni kwa macho ya kawaida Waebrania 11:1, ikisisitiza mtazamo wa kuamini pasipo shaka. Mara nyingi nashuhudia kupita katika giza la imani mara nyingi nilikuwa sioni mwelekeo mzuri wa maisha, sikukata tamaa. Leo nashuhudia kuwa Mungu alitaka ni komae katika Imani na naendelea kupambana ili nizidi kukomaa katika Imani, katika kumtumainia Mungu. Mara nyingi nimetamani yale ninayo penda mimi yatokee lakini mara chache tu yalitokea ila mara nyingi hayatokei ila yale yaliyo pangwa na Mungu katika njia ya wito wangu, hivyo tena na tena najifunza nikiomba si mapenzi yangu ya timie bali ya yule aliye niumba aliye nichagua, anaye niongoza daima mapenzi yake yatimizwe.

Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya baraka, neema na faraja
Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya baraka, neema na faraja

Sita: Katika maisha yangu ya wito nimejifunza kutokukata tamaa. Kukata tamaa ni dhambi, kukata tamaa ni kuto kuaminia nguvu za Mungu, uwezo wa Mungu, maongozi ya Mungu pia uwepo wa Mungu. Ila kuna kipindi katika maisha yangu nime mwuliza Mungu ‘‘kweli wewe upo’’?  Nilihisi nipo peke yangu. Lakini pamoja na mahangaiko yangu bado nilijua Mungu yupo. Tupate neno kutoka Zaburi ya   142:3. Mzaburi anatuhimiza kutoruhusu roho ya kukata tamaa. Tunapokumbana na changamoto, Mungu anatuahidi nguvu. ukumbuke kuwa Mungu anajua tunayopitia, tena Isaya 42:4 inathibitisha hatua zake za kutupa tumaini "Yeye hatafifia wala kufa moyo, hata atakapoimarisha haki duniani. Watu wa mbali wanangojea mwongozo wake." Tukimtuaminia Mungu kwa hakika hatufi moyo mara nyingi tunapata nguvu, tuna kuwa kama mti uliopatwa kando ya mto: Baraka ya Mtu Mwadilifu Zaburi (1:1-3): Mwandishi anasema mwenye heri (baraka) ni yule asiyefuata mashauri ya waovu, asiyesimama katika njia ya wenye dhambi, wala asiyeketi na wenye dharau. Badala yake, furaha yake inapatikana katika sheria ya Mwenyezi Mungu, akiitafakari mchana na usiku. Mtu huyu anafananishwa na mti uliopandwa kando ya vijito vya maji, unaotoa matunda kwa majira yake na majani yake hayanyauki. Pia Mtume Paulo kwa Wagalatia 6:9: anasema "Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho." Mstari huu unatukumbusha kwamba bidii yetu italeta matokeo mazuri tukiendelea kuvumilia nami naendelea kujitahidi, daima kujikabidhi kwa Mungu ili nisichoke wala kuzimia. Nilipo hisi nguvu zangu zinakwisha Mungu aliweza kutuma watu wema kwangu kunitia moyo kama Zaburi 142:3: isemavyo "Ninapokaribia kukata tamaa kabisa, yeye yupo, anajua mwenendo wangu." Mara nyingi amenipa kitulizo, alifuta machozi yangu. Hii inathibitisha kuwa Mungu anatujua hata tunapokuwa katika nyakati ngumu zaidi.

Ni safari ya Miaka 25 za maisha, utume na majitoleo: Neema na huruma ya Mungu
Ni safari ya Miaka 25 za maisha, utume na majitoleo: Neema na huruma ya Mungu

Kutoka katika Injili kama ilivyoandikwa na Luka 18:1: Yesu anatoa mfano unaokazia "kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala musikate tamaa." Kwa hiyo daima najitahidi kudumu katika sala. Kusali kwa Mapenzi ya Mungu: Maombi yanayojibiwa ni yale yanayopatana na mpango Wake. Kusali kwa unyenyekevu: Kukiri ukuu wa Mungu na kutambua utegemezi wako Kwake. Ni kweli kabisa, katika Kitabu cha Nabii Isaya 55:8 Isaya 55:8, Mungu anathibitisha kwamba mawazo yake na njia zake ni tofauti na za mwanadamu. Hii inamaanisha kwamba hekima, haki, na huruma ya Mungu zinapita sana uelewa wetu wa kibinadamu. Kwa hiyo mimi daima najifunza kudumu katika sala, maombi yangu yasipojibiwa najitahidi kuwa mvumilivu. Maana wakati wa Mungu si wakati wangu, njia za Mungu si njia zangu, daima namtegemea Mungu.

Ni maisha kwa ajili ya Mungu na jirani
Ni maisha kwa ajili ya Mungu na jirani   (@VATICAN MEDIA)

Hitimisho: Naweza kusema kuwa katika safari yoyote ya maisha, nimejifunza kuto kutembea peke yangu bali Mungu ndiye anaye ongonza njia, mara zote nimejitahidi kumsikiliza na ninaendelea kumtegea Mungu sikio langu ili niweze kufuata maongozi yake.  Hivyo mara zote ni muhimu sana kufuata maongozi ya Mungu, hatuta kata tamaa.  Kusimama imara na msimamo wangu bila kuyumbishwa wakati mwingine na Mawazo yangu mwenyewe wala ya wengine, hapa sisemi kuwa tusi sikilize ushauri wa wengine hapana bali akili ya mwingine changanya na yako. Ni vyema kupokea ushauri ila lazima kuuchuja. hekima ya Mungu ituongoze daima. Katika maisha yangu ya wito nimejifunza kumshukuru Mungu kila wakati. kama mtume Paulo anasema kutoka kwa 1 Wathesalonike 5:18, linalosema: "Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu." Tendo hili linajenga uhusiano wa karibu na Mungu. Zaburi 107:1 inasema: "Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; maana fadhili zake ni zamilele. Kumshukuru Mungu ni kukiri kuwa peke yangu siwezi kitu, yeye ndiye anaye wazesha yote, nami nakiri hilo kuwa yeye ndiye aliye nifanya leo nisimame mbele yake na kumshuru. Kushukuru ni kuomba tena kwa sababu unapomshukuru Mungu kwa yale aliyotutendea, tunazidi kumkaribia na kuonyesha imani kwamba yuko tayari kuendelea kutubariki. Shukrani ni ufunguo wa kufungulia milango zaidi. Mtume Paulo kwa Wafilipi 4:6: Inatuhimiza tusiwe na wasiwasi, bali katika kila neno kwa kusali, kuomba, na kushukuru, haja zetu zijulikane na Mungu. Kwa ukweli Mungu ni wa kwanza kumtolea haja zetu, yeye baadae anatuelekeza tutende nini au tuende wapi au tupite njia gani. Daima macho yetu ni kwa Mungu. Napenda kumalizia safari ya maisha yangu ya wito wangu kwa kuwashukuru wazazi Wangu, ndugu zangu, mwanajubilei mwenzangu tunae tembea pamoja Sr Evangelista Namangaya OSB, wanashirika wenzangu, marafiki na wote wenye mapenzi mema kwangu, walio toa mchango wao wa hali na mali. nikaweza kufika hapa nilipo, nasema asanteni sana na Mungu awabariki wote. Kwa kuwa kushuru ni kuomba tena, Basi namwomba Mungu aendelee kufungua mioyo ya vijana wengi waisikie sauti ya Mungu ndani mwao ikiwaita kumtumikia Mungu katika maisha ya utawa.  Nao kamwa wasiipuuzie sauti ya Mungu bali kwa moyo wote waifuate. Mungu atubariki sisi sote. Amina.

Jubilei Miaka 25
18 Agosti 2026, 17:10