Tafuta

Kauli mbiu inayonogesha mkuutano wa kwanza:  “Majadiliano kati ya Wakristo na wafuasi wa “Confucion” kwa ajili ya kujenga jamii bora” Kauli mbiu inayonogesha mkuutano wa kwanza: “Majadiliano kati ya Wakristo na wafuasi wa “Confucion” kwa ajili ya kujenga jamii bora”  

Majadiliano ya Kidini Kati ya Wakatoliki na Waamini wa Dini ya "Confucion"

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Korea, Chuo Kikuu cha Sogang na Taasisi ya dini ya “Confucion”, kwa mara ya kwanza, wameandaa mkutano wa kwanza utakaofanyika Chuo Kikuu cha Sogang kilichoko mjini Seoul, nchini Korea kuanzia tarehe 4 hadi 5 Agosti 2026 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Majadiliano kati ya Wakristo na wafuasi wa “Confucion” kwa ajili ya kujenga jamii bora”: Mbingu, Dunia Mpya na Datong, Amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 60 iliyopita walitoa tamko kuhusu majadiliano ya kidini kwa watu wa nyakati hizi linalojulikana kama “Nostra Aetate." Hili ni tamko linalokazia pamoja na mambo mengine: Dhamana ya Kanisa katika kuhamasisha umoja na upendo kati ya watu wa Mataifa; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kusimama kidete kutangaza na kushuhudia pamoja utu na heshima ya binadamu. Kanisa Katoliki linatambua mambo ya kweli na matakatifu katika dini mbalimbali, lina heshimu na kuthamini namna yao ya kutenda na kuishi; sheria na mafundisho yao. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Kanisa litaendelea kutangaza kwamba: Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima na ambaye ndani mwake mwanadamu anapata utimilifu wa maisha ya utauwa na upatanisho kati yake na Mwenyezi Mungu.

Majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na waamini wa dini ya "Confucion"
Majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na waamini wa dini ya "Confucion"   (ANSA)

Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi. Kanisa linatambua kwamba, bado kuna changamoto nyingi na vikwazo vya kufanyiwa kazi, lakini hadi hapa linapenda kumshukuru Mungu kwa jiitihada zilizokwisha kufikiwa katika medani mbalimbali za maisha. Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Mama Kanisa anaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kufahamiana, kuheshimiana na kushirikiana kwa dhati katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji, linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani.

Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa
Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Waamini wanaweza kujenga na kudumisha umoja, udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii kwa kusaidiana katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mama Kanisa anakazia: Umuhimu wa watu kuishi katika umoja, upendo na mshikamano kwa sababu majadiliano ya kidini, udugu wa kibinadamu, haki na amani ni mambo msingi ya maisha ya watu wa Mungu. Kwa njia ya majadiliano ya kidini, watu wanakutana, wanazungumza, wanafahamiana na hivyo kuanzisha mchakato wa kutembea bega kwa bega kama ndugu wamoja. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuwa ni shuhuda na chombo cha amani, kwa kufyekelea mbali yale yote yanayosababisha: chuki, kinzani na mipasuko ya kidini na kiimani. Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Korea, Chuo Kikuu cha Sogang na Taasisi ya dini ya “Confucion”, kwa mara ya kwanza, wameandaa mkutano wa kwanza utakaofanyika Chuo Kikuu cha Sogang kilichoko mjini Seoul, nchini Korea kuanzia tarehe 4 hadi 5 Agosti 2026 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Majadiliano kati ya Wakristo na wafuasi wa “Confucion” kwa ajili ya kujenga jamii bora” kama dira na mwongozo wa tema ya majadiliano: “Mbingu mpya, Dunia Mpya na Datong yaani, Utulivu na Umoja. Majadiliano haya yanawakusanya viongozi maarufu wa dini, wanazuoni na wawakilishi wa dini hizi mbili ili kupembua kwa kina na mapana mchango wa dini hizi mbili katika mchakato wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika haki, amani na utu wema.

Ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa haki, amani, utu na maadili
Ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa haki, amani, utu na maadili   (AFP or licensors)

Dini hizi mbili zinashirikishana maono yao ya pamoja mintarafu utu, heshima, kanuni maadili, uwajibikaji wa viongozi na kwamba, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni uwanja maalum kwa ajili ya majadiliano haya ya kina. Majadiliano haya yanatarajiwa kugusia changamoto mambo leo, mintarafu mipasuko ya kijamii, utepetevu wa kanuni maadili na utu wema, uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote pamoja na mambo yanayotishia amani sehemu mbalimbali za dunia. Mkutano huu unatarajiwa kuhitimishwa kwa mwaliko wa dini hizi mbili kushirikiana kwa karibu zaidi katika sekta ya elimu, majiundo ya maadili; ujenzi wa haki na amani na huu unakuwa ni mwanzo wa ujenzi wa msingi wa majadiliano kati ya Mapokeo ya dini hizi mbili.

Majadiliano ya kidini

 

 

01 Agosti 2026, 14:53