Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni 2027: Wimbo na Sala Rasmi

Wimbo rasmi umetungwa na Francis Jiyoon Kim kutoka Korea unaochota amana na utajiri wake kutoka katika kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni: “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33. Ni wimbo ambao umetungwa katika mandhari ya utamaduni wa watu wa Mungu kutoka Korea, lakini unaweza kuimba na vijana wote katika lugha mbalimbali. Kuna Watakatifu watano waombezi na wasimamizi wa Maadhimisho haya.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Mara baada ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana yaliyonogeshwa na kauli mbiu: “Vijana mahujaji wa matumaini” Baba Mtakatifu Leo XIV alitangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2027 Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini, yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 3 hadi 8 Agosti 2027 na kwamba, maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu; “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33. Matumaini yaliyomo ndani ya nyoyo za waamini ndiyo yanayowapatia nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya dhambi na mauti. Kwa hakika anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa matumaini hadi miisho ya dunia. Alitumia fursa hii kuwakaribisha vijana wengi zaidi huko Seoul, Korea ya Kusini, ili kwa pamoja waweze kuendeleza ndoto na matumaini. Kumbe, vijana pamoja na wachungaji wao watakaohudhuria maadhimisho haya wanazidi kuwa ni kiini cha maandalizi ya tukio hili muhimu la Kikanisa. Wimbo Maalum wa tukio hili pamoja na Sala rasmi na ushuhuda wa watakatifu watano walioteuliwa kuwa ni wasimamizi na walinzi wa kiroho kwa ajili ya Maadhimisho haya ni nyenzo msingi za kichungaji zinazowasaidia vijana wa kizazi kipya kujiandaa kikamilifu kiroho kwa ajili ya maadhimisho haya na kwamba, maadhimisho haya yamezidi kutajirishwa kutokana na imani, shauku na ushiriki hai wa vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni mwaliko kwa Maaskofu na viongozi wa Kanisa watakao ambatana na vijana kwenda Seoul kutumia vyema amana, utajiri na rasilimali hizi katika maandalizi yao, ili hatimaye, waweze kuiishi siku hii kama tajiriba halisi ya imani, umoja na mshikamano wa Kanisa sanjari na vijana kukutana binafsi na Kristo Yesu Mfufuka.

Jipeni Moyo Mimi nimeushinda Ulimwengu Yn 16:33
Jipeni Moyo Mimi nimeushinda Ulimwengu Yn 16:33   (sito web GMG)

Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni nchini Korea ya Kusini inasema, inaendelea kukamilisha maandalizi ya maadhimisho haya kwa kujikita katika ushirikiano wa kimataifa, huduma kwa ajili ya mahujaji, malazi, usafiri, usalama, huduma za afya na mawasiliano. Vijana wote wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya maisha yao ya kiroho. Wimbo rasmi wa maadhimisho haya hivi karibuni ulizinduliwa rasmi na umetungwa na Francis Jiyoon Kim kutoka Korea unaochota amana na utajiri wake kutoka katika kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni: “Jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” Yn 16:33 na kwa lugha ya Kilatini unasomeka hivi: “Confidite, Ego Vici Mundum.” Ni wimbo ambao umetungwa katika mandhari ya utamaduni wa watu wa Mungu kutoka Korea, lakini unaweza kuimba na vijana wote katika lugha mbalimbali. Mtunzi wa wimbo huu Francis Jiyoon Kim ameonesha moyo wake wa shukrani kwa Mungu na upendo wake kwa Mama Kanisa, kumbe wimbo huu ni matunda ya shukrani kwa karama na upendo ambao ameupokea katika safari ya maisha na taaluma yake. Kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho haya, vijana katika maeneo yao, wanahimizwa kushiriki kampeni ya kupanda miti kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika kampeni ambayo imepewa jina: “Breath of life” yaani “Pumzi ya Uhai” ni sehemu ya utekelezaji kwa vitendo Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote.” Waraka huu pamoja na mambo mengine unazungumzia kuhusu: Mambo yanayoendelea kujiri katika mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii. Njia za kupanga na kutenda na umuhimu wa elimu ya ikolojia inayojikita katika wongofu wa ndani, furaha na amani.

Askofu mkuu Peter Chung Soon-taick, Jimbo kuu la Seoul , Korea ya Kusini
Askofu mkuu Peter Chung Soon-taick, Jimbo kuu la Seoul , Korea ya Kusini

Wakati huo huo, Askofu mkuu Peter Chung Soon-taick, O.C.D. wa Jimbo kuu la Seoul ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea “The Catholic Bishops' Conference of Korea, CBCK” anasema, Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni ni tukio la matumaini, ushuhuda wa upendo, ukarimu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Vijana nchini Korea kuanzia tarehe 29 Julai hadi tarehe 2 Agosti 2027 watashiriki Maadhimisho ya Siku ya Vijana katika ngazi ya kijimbo, kama sehemu muhimu sana ya ushuhuda wa vijana na watu wa Mungu katika majimbo yao, ili hatimaye waweze kuitamadunisha Injili ambao kimsingi ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu wa Mungu nchini Korea.

Korea inakuwa ni mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, nchi ambayo mchakato wake wa Uinjilishaji ni kazi na matunda ya waamini walei. Watakatifu na waombezi wa Maadhimisho ya Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni ni: Mtakatifu Yohane Paulo II; Muasisi wa Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni; Mtakatifu Andrea Kim Taegon, Padre wa kwanza Mkatoliki kutoka Korea, alama ya imani na ujasiri. Mtakatifu Francesca Saverio Cabrini, Msimamizi na Mwombezi wa Wakimbizi na Wahamiaji; Mtakatifu Josepine Bakhita, Mtumwa aliyekombolewa, akabahitika kuwa ni Mtawa wa Shirika la Mabinti wa Upendo wa Mtakatifu Magdalena wa Canossa (Canossian Daughters of Charity). Bakhita ni shuhuda wa imani kupitia mateso, nyanyaso na dhuluma mambo yamayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Na hatimaye ni Mtakatifu Carlo Acutis anayejulikana kuwa na Ibada ya kina kwa Ekaristi Takatifu, na matumizi yake ya mtandao wa intaneti katika kueneza imani yake, alivutiwa na kuongozwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Hata alikwenda kuhiji kwa ajili ya kumwona. Carlo aliyatoa mateso yake ya kuugua saratani ya damu kwa nia za Baba Mtakatifu Benedikto XIV. Carlo alitangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mwenyeheri kunako Mwezi Oktoba 2020, na hatimaye Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 7 Septemba 2025 akamtangaza kuwa ni Mtakatifu na kumbukumbu yake ni tarehe 12 Oktoba ya kila mwaka. Ni kijana aliyetumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuwainjilisha vijana wenzake. Usajili wa washiriki wa maadhimisho haya utazinduliwa hivi karibuni kwa kutumia kiunganishi kifuatacho: website www.wydseoul.org.

Siku ya 42 ya Vijana Ulimwenguni
07 Agosti 2026, 15:16