Tafuta

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Guatemala ulianzishwa rasmi tarehe 15 Machi 1936 na Papa Pio XI na mwaka 2026, uhusiano huu unatimiza miaka 90 Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Guatemala ulianzishwa rasmi tarehe 15 Machi 1936 na Papa Pio XI na mwaka 2026, uhusiano huu unatimiza miaka 90   (CRISTINA_CHIQUIN)

Kumbukizi ya Miaka 90 ya Uhusiano Kati ya Vatican na Guatemala: Diplomasia ya Majadiliano

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Guatemala ulianzishwa tarehe 15 Machi 1936 na Papa Pio XI na mwaka 2026, uhusiano huu unatimiza miaka 90 ya ushirikiano wa masuala ya maisha ya kiroho, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Guatemala. Kardinali Pietro Parolin kuanzia tarehe 1 hadi 4 Agosti 2026 amekuwa akifanya hija ya kitume nchini Guatemala, kama sehemu ya kumbukizi ya miaka 90 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, kimsingi inakazia kwa namna ya pekee kabisa: huduma makini ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mambo mengine msingi ni: amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani; elimu, afya, biashara, mawasiliano, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na haki miliki ya kiakili. Hizi ni kanuni msingi zinazofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa dira na mwongozo makini kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kukuza na kudumisha utamaduni wa amani, haki, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu. Hii ni sehemu muhimu sana ya utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa.

Kardinali Pietro Parolin akiwa nchini Guatemala 2026
Kardinali Pietro Parolin akiwa nchini Guatemala 2026   (AFP or licensors)

Vatican katika masuala ya diplomasia ya Kimataifa inafuata kwa makini sana: Sheria za Kimataifa, taratibu na kanuni za Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii inayojikita katika kanuni maadili, utu wema na ushirikiano unaosimamiwa na kuratibiwa na kanuni auni. Amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa kujengwa siku kwa siku. Amani ni matokeo ya haki inayomwilishwa katika upendo, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. GS 78. Amani ya kweli inakolezwa katika urafiki wa udugu wa kibinadamu na kwamba, upatanisho ni mchakato unaopania kuboresha maisha ya mbeleni na unafumbatwa katika toba, msamaha na wongofu wa ndani, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo, chemchemi ya amani ya kudumu. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia Januari 2026 Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 duniani kote. Mabalozi wakazi wanaoishi mjini Roma kwa sasa ni 89, wengine, ni mabalozi wanaowakilisha nchi zao wakiwa wanatoka nje ya Roma. Kuna Mashirika ya Kimataifa kama vile, Shirikisho la Nchi za Kiarabu pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR yote haya yanafanya idadi yake ifikie 93.

Kardinali Parolin akisalimiana na baadhi ya waamini
Kardinali Parolin akisalimiana na baadhi ya waamini   (AFP or licensors)

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Guatemala ulianzishwa rasmi tarehe 15 Machi 1936 na Papa Pio XI na mwaka 2026, uhusiano huu unatimiza miaka 90 ya ushirikiano wa masuala ya maisha ya kiroho, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Guatemala. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 1 hadi 4 Agosti 2026 amekuwa akifanya hija ya kitume nchini Guatemala, kama sehemu ya kumbukizi ya miaka 90 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Guatemala sanjari na kumbukizi ya Miaka 400 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Petro de San José de Bethencourt, hapo tarehe 21 Machi 1626 huko Vilaflor, Tenerife, na kufariki dunia tarehe 25 Aprili 1667 nchini Guatemala akiwa na umri wa miaka 41. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 30 Julai 2002 akamtangaza kuwa ni Mtakatifu wa kwanza kutoka nchini Guatemala. Kardinali Parolin, Dominika tarehe 2 Agosti 2026 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbukizi hii na katika mahubiri yake amesema kwamba, ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayeweza kuganga njaa na kiu ya ndani kabisa ya maisha ya mwanadamu inayokita mizizi yake katika hamu ya kupata upendo, matumaini na maisha ya uzima wa milele. Shauku ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu humwongoza mtu kujenga jamii inayosimikwa katika haki, udugu na mshikamano wa kibinadamu, huku akivunjilia mbali: dharau, hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zake; dhuluma, ukosefu wa usawa, ufisadi na rushwa mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za Guatemala.

Kumbukizi ya Miaka 90 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican & Guatemala
Kumbukizi ya Miaka 90 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican & Guatemala   (AFP or licensors)

Kardinali Parolin, ametumia fursa hii kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa watu wa Mungu nchini Guatemala. Amesema, Mwenyezi Mungu kamwe hajawahi kuwaacha waja wake katika shida na mahangaiko yao na kwamba, Kanisa lina wajibu wa kujikita katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuwakirimia watu wa Mungu Mkate wa uzima, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao na hivyo kuwa tayari kusikiliza na kujibu kilio chao cha ndani. Binadamu anapokabiliana na changamoto mamboleo kama vile: ujinga, umaskini, baa la njaa, magonjwa, upweke hasi, vita, ukosefu wa haki na amani pamoja na mateso, mambo ambayo kimsingi yanapata chimbuko lake kutokana na ufisadi, uchoyo na ubinafsi. Hata katika kidogo ambacho waamini wamebarikiwa kuwa nacho yaani: muda, karama, ukarimu na hata udhaifu wao, Kristo Yesu atawazidishia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Watu asilia nchini Guatemala
Watu asilia nchini Guatemala   (ANSA)

Kardinali Pietro Parolin, akizungumza na wanadiplomasia na wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa wanaoziwakilisha nchi zao, amekazia umuhimu wa diplomasia ya majadiliano badala ya diplomasia inayotilia mkazo nguvu za silaha; hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa na kuheshimiwa; Uhuru wa kidini na uhuru wa dhamiri ni msingi wa haki nyingine zote. Yote haya yasaidie kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika haki, udugu na mshikamano wa kibinadamu, ili kuondokana na utandawazi wa kutoguswa na mahangaiko ya jirani; uchu wa madaraka pamoja na rushwa mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kardinali Parolin ameonya kuhusu kuibuka kwa haki mpya za binadamu zinazokwenda kinyume cha utu wa binadamu. Diplomasia ya Vatican inachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na Mapokeo, ili kulinda na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu, haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Amesema, Kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali ya Guatemala katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu, ili kuhakikisha kwamba, jamii inasimama kidete kulinda na kutangaza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; uhuru na elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kardinali Pietro Parolin wakati wa hija yake ya kitume nchini Guatemala amepata nafasi ya kutembelea Kituo cha Mama Theresa wa Calcutta cha kutunzia Wazee, ametembelea Madhabahu ya Mtakatifu Petro de San José de Bethencourt na hatimaye, amekutana na kuzungumza na Maaaskofu, Mapadre na Watawa kutoka nchini Guatemala na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Madhabahu ya Kuabudia Ekaristi Takatifu.

Parolin Guatemala
04 Agosti 2026, 15:17