Kardinali Rugambwa Atabaruku Kanisa Kuu la Jimbo kuu Arusha
Na Fredy William, Arusha na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. -Vatican.
Kanisa ni Jumuiya ya watu wa Mungu inayoongozwa na nguvu ya Mungu. Ni watu wenye imani moja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi. Wao wanaofungamanishwa na nguvu ya Kristo Yesu inayowatakasa na kuwaokomboa. Kanisa pia ni jengo maalum lililotengwa kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Kwa namna ya pekee kabisa, Kanisa kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Jimbo kuu la Arusha, Tanzania limetabarukiwa tarehe 7 Agosti 2026 na kwamba, uzito wake unafumbatwa katika maisha ya waamini wenyewe wanaoliwezesha Kanisa kuwa kweli ni Kanisa. Kanisa hili sasa limewekwa wafu kwa ajili ya kumtolea Mungu: sifa, shukrani na sala, ili waamini waweze kutakatifuzwa. Kanisa hili kwa sasa ni nyumba ya Sala, Nyumba ya Mungu na Nyumba ya Ibada. Ni mahali ambapo waamini wanalishwa kwa Neno la Mungu na kushibishwa kwa Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Altare imetabarukiwa na hivyo kuwekwa wakfu, inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa sababu Altare ni kielelezo cha Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayejisadaka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Ni mahali ambapo waamini wanatolea sala na sadaka zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Kanisa pawe ni mahali pa: amani, usalama na utulivu wa ndani. Waamini wajifunze kutumia vyema nyumba ya Mungu na wala si mahali pa kwenda kupiga picha au kuperuzi kwenye mitandao wakiwa Kanisani.
Kuta za Kanisa zimetabarukiwa kwa kupakwa Mafuta ya Krisma ya Wokovu yanayobarikiwa Siku ya Alhamisi Kuu. Haya ni mafuta matakatifu yanayotumika kwa ajili ya Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu. Mapadre wanapakwa Krisma ya wokovu viganjani mwao kama alama ya baraka na huduma kwa watu wa Mungu. Askofu anamiminiwa Krisma ya wokovu utosini kama kielelezo cha ukamilifu wa Daraja Takatifu na hivyo kufanywa kuwa ni mrithi na mwandamizi wa Mitume wa Kristo Yesu. Altare ni mahali patakatifu sana ndani ya Kanisa paheshimiwe na kuthaminiwa kwa ajili ya kuadhimisha Mambo Matakatifu, mahali pa kutolea sadaka ya haki na kulishwa kwa Neno la Mungu. Kumezikwa Masalia ya watakatifu ndani ya Kanisa kama kielelezo cha ushirika wa watakatifu unaosimikwa katika mema ndani ya Kanisa ambayo kimsingi ni amana na hazina ya pamoja. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu kwa ajili ya watakatifu. Kimsingi huu ni ushirika wa imani, Sakramenti za Kanisa, Karama na mapendo. Maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ndani ya Kanisa yananogeshwa na Neno la Mungu anayejifunua kwako, ili kuwatakatifuza na kuwatuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kama ilivyokuwa kwa Nabii Isaya, Mwenyezi Mungu anapenda kuonesha wema, huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Kristo Yesu Mfufuka bado anaendelea kukutana na wafuasi wake, kila mmoja katika Galilaya yake. Hapa ni mahali pa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo; Imani, Shukrani na Ibada katika kweli na roho. Ni katika muktadha huu, Galilaya ni eneo la kijiografia lakini pia ni mahali pa kukutana na Kristo Mfufuka. Kumbe, Galilaya ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Arusha ni katika familia zao, jumuiya ndogondogo za Kikristo, vigangoni, parokiani, jimboni na Kanisa la Kiulimwengu. Kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu, waamini wajitahidi kumtambulisha Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili aweze kufahamika, kupendwa na kutumikiwa na wengi!
Ni katika muktadha huu, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Tanzania, amesema kuwa Kanisa si jengo la mawe pekee bali ni jumuiya ya waamini wanaounganishwa na Kristo Yesu, hivyo kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu kunapaswa kuambatana na kutabarukiwa kwa mioyo ya waamini ili waishi maisha ya umoja, utakatifu na utume. Kardinali Rugambwa aliyasema hayo wakati wa mahubiri yake katika Ibada ya Misa Takatifu ya Kutabaruku Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Jimbo Kuu Katoliki Arusha, akieleza kuwa Kanisa Kuu ni kitovu cha maisha ya kiimani na kiliturujia cha Jimbo, mahali ambapo waamini hukutana kumsifu na kumwabudu Mungu, kuadhimisha Sakramenti na kutumwa kwenda kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Awali ya homilia yake, Kardinali Rugambwa aliwashukuru viongozi wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha pamoja na waamini wote walioshiriki kwa hali na mali kuhakikisha ujenzi wa Kanisa Kuu unakamilika, akisema mafanikio hayo ni ushuhuda wa imani, mshikamano na sadaka ya watu wa Mungu. Alifafanua kuwa kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu si tukio la kawaida, bali ni mwanzo wa safari mpya ya kiroho inayowaalika waamini kuimarisha maisha yao katika nguzo kuu nne ambazo ni umoja, maisha ya Sakramenti, utakatifu na utume wa kimisionari. "Tunatabaruku Kanisa Kuu la Jimbo, si Parokia wala kanisa la kawaida. Hapa ndipo tutakapomsifu Mungu, kuadhimisha Sakramenti na kutoka tukiwa wamisionari wa Kristo. Lakini tusisahau kuwa Kanisa si mawe bali ni watu wanaounganishwa na Kristo Yesu."
Akirejea Somo la Kwanza kutoka Kitabu cha Nabii Yeremia, Kardinali Rugambwa alisema Kanisa lililotabarukiwa litakuwa mahali pa kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu, ambalo lina nguvu ya kuwabadilisha waamini na kuwapa uwezo wa kuishi maisha mapya yenye haki, upendo na ukweli. Alisisitiza kuwa kila Mkristo aliyebatizwa ni "jiwe hai" katika ujenzi wa Kanisa la Kristo, hivyo kila mmoja ana nafasi muhimu katika mwili wa Kristo na anapaswa kushiriki kikamilifu katika kulijenga Kanisa kwa roho ya ushirika na ushirikishwaji. Katika muktadha huo, Kardinali Rugambwa aliwahimiza waamini kuendelea kuijenga roho ya Kanisa la Kimisionari na Kisinodi kwa kutembea pamoja, kuwajibika pamoja na kushirikiana katika kutimiza utume wa Kanisa. Akizungumzia Injili, Kardinali Rugambwa alikumbusha umuhimu wa upatanisho kabla ya kushiriki ibada, akisema maisha ya Sakramenti yanapaswa kuzaa matunda ya msamaha, haki, umoja na upendo ndani ya familia, jumuiya na parokia. Alieleza kuwa Sakramenti zinazoadhimishwa katika Kanisa ndizo zinazowaunganisha waamini na Kristo na kuwapa nguvu ya kwenda kuwahudumia wengine kwa matendo ya huruma na Injili ya kweli. Aidha, aliwataka waamini kutambua kuwa zawadi ya imani haipaswi kubaki ndani ya Kanisa pekee bali iwafanye kuwa mashuhuda wa Kristo katika jamii kwa kueneza Neno la Mungu kupitia maisha yao ya kila siku.
Kardinali Rugambwa amewahimiza pia kuwakumbuka na kuwaombea wale waliojitenga na Kanisa ili warejee katika ushirika wa waamini na kupata njia ya kuelekea uzima wa milele. Akihitimisha mahubiri yake, aliwakumbusha waamini kuwa wito wa kila Mkristo ni kuishi utakatifu, akisisitiza kwamba utakatifu haupatikani kwa kufanya mambo makubwa pekee, bali kwa kutekeleza mambo madogo kwa upendo mkubwa. "Kwa ubatizo kila mmoja wetu ameitiwa utakatifu. Tuombe neema ya kuufikia kwa kufanya mambo madogo kwa upendo mkubwa, ili siku moja tufike Yerusalemu ya Mbinguni." Kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu kunafungua ukurasa mpya katika historia ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha, ambapo Kanisa hilo litakuwa kitovu cha ibada, Sakramenti, malezi ya kiroho na utume wa uinjilishaji, huku waamini wakialikwa kuendelea kujenga Kanisa hai linalodhihirisha umoja, upendo na ushuhuda wa Kristo katika ulimwengu. Kanisa kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu ni ishara ya umoja na uwepo wa Mungu kati ya watu wake: ASKOFU wa Jimbo Katoliki Bariadi, Mhashamu Prosper Baltazar Lyimo, amesema kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu la Jimbo Kuu Katoliki Arusha ni ushuhuda wa baraka naneema ya Mungu, umoja wa waamini na matunda ya sala, sadaka na mshikamano wa Kanisa kwa kipindi cha zaidi ya miongo sita ya historia ya Jimbo hilo. Askofu Lyimo amesema hayo wakati wa Ibada ya Masifu ya Jioni iliyofanyika katika Parokia ya Tokeo la Bwana Burka, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kutabaruku na kuweka wakfu Kanisa Kuu jipya la Jimbo Kuu Katoliki Arusha. Akikumbusha historia ya Jimbo hilo, Askofu Lyimo alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963, Kanisa Kuu la zamani lilitosheleza mahitaji ya waamini kwa wakati huo. Hata hivyo, ukuaji wa idadi ya waamini ulisababisha kuibuka kwa hitaji la kujenga Kanisa Kuu kubwa zaidi litakalokidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Alieleza kuwa ndoto hiyo ilianza rasmi chini ya uongozi wa Hayati Mhashamu Fortunatus M. Lukanima ikaendelezwa kwa msukumo mkubwa na Askofu mkuu mstaafu Mhashamu Josaphat Louis Lebulu kuanzia mwaka 1997, na baadaye kukamilishwa katika kipindi cha Askofu Mkuu Mhashamu Isaac Amani Massawe. "Haya ni matunda ya kazi, sala na sadaka za watu wa Mungu. Wengi walioanza safari hii hawapo nasi leo, lakini mchango wao umebaki kuwa sehemu ya historia ya Jimbo letu. Tuendelee kuwaombea wote waliotutangulia mbele ya haki." Askofu Lyimo alisema mafanikio hayo hayakupatikana kwa nguvu za kibinadamu pekee, bali kwa msaada wa Mungu na maombezi ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu msimamizi wa Jimbo letu na watakatifu wengine ambao waliongoza safari hiyo ya imani. Aidha, aliwataka waamini kutambua kuwa pamoja na uzuri wa Kanisa Kuu linalotabarukiwa, kila Mkristo anapaswa pia kulitunza "hekalu la moyo" kwa kuishi maisha ya toba na wongofu wa ndani; msamaha, upendo na utakatifu. Alisisitiza kuwa tofauti za kikabila, kisiasa, kijamii au kiuchumi hazipaswi kugawa familia ya Mungu, bali Kristo ndiye anayewaunganisha waamini wote kuwa Kanisa moja. "Tusiliangalie Kanisa kama jengo pekee tukasahau kwamba kwa Ubatizo tumefanywa kuwa mahekalu ya Mungu. Kanisa hili ni kitovu cha maisha ya kiroho Jimboni kwetu, lakini pia linatukumbusha wajibu wa kutunza mioyo yetu ili iwe makao ya Mungu." Akihitimisha mahubiri yake, Askofu Lyimo aliwahimiza waamini kuingia katika Kanisa Kuu jipya wakiwa na mioyo iliyotakaswa kwa Sakramenti ya Upatanisho, ili waweze kupokea neema za Mungu na kuwa mashuhuda wa amani, umoja na upendo katika familia na jamii. Amewapongeza waamini wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha kwa hatua hiyo ya kihistoria, akiwataka waendelee kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Kanisa Kuu jipya ambalo litakuwa kitovu cha ibada, uinjilishaji na ukuaji wa imani kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.