Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC: Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS ameendelea kuwa mfano wa mchungaji anayejenga Kanisa kupitia maisha ya sala, ibada na huduma ya kujitoa kwa watu wa Mungu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC: Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS ameendelea kuwa mfano wa mchungaji anayejenga Kanisa kupitia maisha ya sala, ibada na huduma ya kujitoa kwa watu wa Mungu 

Jubilei ya Miaka 25 ya Askofu Ludovick Joseph Minde: Sala, Huduma na Moyo wa Upendo

Askofu Wolfgang Pisa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), amesema Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS ameendelea kuwa mfano wa mchungaji anayejenga Kanisa kupitia maisha ya sala, ibada na huduma ya kujitoa kwa watu wa Mungu, sifa ambazo zimeendelea kuimarisha utume wake katika kipindi cha miaka 25 ya Uaskofu na Miaka 40 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Ni Jembe kweli kweli katika: Sala, Ibada, Huduma na Upendo!

Na Fredy William - Moshi

Askofu Anthony Lagwen wa Jimbo Katoliki Mbulu, Tanzania, amesema Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Mhashamu Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki Moshi ni wakati wa kumshukuru Mungu na Kanisa kwa zawadi ya mchungaji aliyejitolea kwa uaminifu katika kulitumikia Taifa la Mungu kupitia huduma ya kichungaji, malezi ya imani na uongozi wenye maono. Akihubiri katika Misa Takatifu ya Kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Ludovick Minde iliyofanyika katika Kanisa kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki Moshi, Askofu Lagwen alisema maisha ya Askofu Minde ni ushuhuda wa namna Mungu anavyomwandaa na kumkuza mtumishi wake hatua kwa hatua kwa ajili ya kulijenga Kanisa. "Mungu amemjalia Baba Askofu Minde zawadi nyingi; zawadi ya uhai, ya imani, ya wito wa kipadri na hatimaye ya huduma ya uaskofu. Leo tunamshukuru Mungu kwa namna alivyoitikia wito huo kwa uaminifu na kuendelea kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wake," alisema Askofu Lagwen. Alieleza kuwa Jubilei hiyo si ya Askofu Minde peke yake, bali ni Sherehe ya Jimbo Katoliki Moshi, Kanisa Katoliki Tanzania na waamini wote waliofaidika na huduma yake kwa kipindi cha miaka 25 ya uaskofu na miaka 40 ya upadri. Huduma yenye matunda ya kiroho na maendeleo. Akirejea Somo la Kwanza kutoka Kitabu cha Hekima ya Yosua Bin Sira, Askofu Lagwen aliwataka waamini kumhimidi Mungu kwa matunda yaliyoonekana katika utume wa Askofu Minde tangu alipokuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kahama hadi sasa akiwa Jimbo Katoliki Moshi. Alisema huduma yake imejengwa juu ya mshikamano, ushirikiano wa kisinodi na kimisionari na kujitoa kwa dhati katika kuimarisha maisha ya sala, ibada, malezi ya waamini pamoja na maendeleo endelevu ya taasisi za Kanisa. Aidha, alieleza kuwa juhudi hizo zimeonekana katika miradi mbalimbali ya kichungaji na maendeleo, ikiwemo uzinduzi wa Nyumba ya Maaskofu uliofanyika kuelekea maadhimisho ya Jubilei hiyo.

Baadhi ya Maaskofu waliohudhuria Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Minde
Baadhi ya Maaskofu waliohudhuria Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Minde

Kaulimbiu iliyommwilishwa katika matendo: Askofu Lagwen alisema kaulimbiu ya Uaskofu ya Askofu Minde isemayo, "Ndipo nilipokuja kuyafanya mapenzi yake," imejidhihirisha wazi katika maisha na huduma yake. Alibainisha sifa tano zilizomtambulisha Askofu Minde katika kipindi chake cha utume ambazo ni utayari wa kuitikia mapenzi ya Mungu, uvumilivu na unyenyekevu katika kubeba majukumu ya kichungaji, moyo wa sala na ibada wenye upendo mkubwa kwa Ekaristi Takatifu na Bikira Maria, moyo wa kujitoa kwa Kanisa bila ubinafsi pamoja na uwazi na unyoofu katika uongozi wake. Kwa mujibu wa Askofu Lagwen, hata wakati wa changamoto za kiafya, Askofu Minde ameendelea kuonyesha ujasiri, matumaini na uaminifu katika kutekeleza wajibu wake wa kichungaji. "Ni mchungaji anayependa ubora katika kila jambo. Anapojenga, anataka ubora; anapolea watumishi wa Kanisa, anatamani ubora; na hata katika utendaji wake ameonyesha kujitoa bila kujibakiza kwa ajili ya watu wa Mungu," alisema. Kanisa liendelee kumtazama Kristo Yesu: Akihitimisha homilia yake, Askofu Lagwen aliwakumbusha waamini kuwa Kanisa linafananishwa na chombo kinachovuka bahari, ambacho wakati mwingine hukumbana na mawimbi na dhoruba, lakini Kristo Yesu ndiye anayelikalia na kuliongoza salama salimini. Aliwahimiza waamini kuendelea kumwangalia Kristo, kumtii na kuyafuata mafundisho yake, akieleza kuwa huo ndio msingi uliomwezesha Askofu Minde kubaki imara katika utume wake kwa kipindi cha miaka 25 ya uaskofu. Pia aliwataka waamini kuendelea kumuombea Askofu Minde ili Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, nguvu na hekima ya kuendelea kuliongoza Jimbo Katoliki Moshi, huku akiwaomba waamini waendelee kumpa ushirikiano katika kutekeleza utume wake wa kichungaji. Tumaini la kuendelea kujenga Kanisa: Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Mhashamu Ludovick Minde, ALCP/OSS, yamewakutanisha Maaskofu, mapadre, watawa na maelfu ya waamini kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakimshukuru Mungu kwa neema ya maisha na huduma ya Askofu huyo ambaye ameendelea kuwa mfano wa uongozi wa sala, unyenyekevu, uwazi na huduma yenye kujitoa kwa ajili ya Kanisa na jamii.

Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS
Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC: Askofu Minde amekuwa mfano wa Askofu anayeishi maisha ya sala na huduma: Askofu Wolfgang Pisa, OFMCap, wa Jimbo Katoliki Lindi na ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), amesema Mhashamu Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS ameendelea kuwa mfano wa mchungaji anayejenga Kanisa kupitia maisha ya sala, ibada na huduma ya kujitoa kwa watu wa Mungu, sifa ambazo zimeendelea kuimarisha utume wake katika kipindi cha miaka 25 ya Uaskofu. Akitoa salamu za pongezi kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa Misa Takatifu ya Kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Ludovick Minde katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki Moshi, Askofu Pisa alisema Jubilei hiyo ni tukio la kumshukuru Mungu kwa neema ya maisha, wito na huduma ya Askofu Minde, ambaye pia ametimiza miaka 40 ya Upadre. "Miaka ishirini na mitano ya kuhudumu kama Askofu si jambo dogo. Leo, kama Maaskofu wenzako, tumekuja kumshukuru Mungu kwa maisha yako, kwa utume wako na kwa huduma unayoendelea kulitoa kwa Kanisa kwa moyo wa sala, upendo na kujitoa," alisema Askofu Pisa. Sala ndiyo msingi wa utume wa Askofu: Katika salamu zake, Askofu Pisa alisema moja ya mambo makubwa yanayomtambulisha Askofu Minde ni msisitizo wake katika maisha ya sala, akieleza kuwa jukumu kuu la Askofu si kusimamia maendeleo ya miundombinu pekee, bali kuwaongoza waamini kuelekea utakatifu. Alisema mfano wa Askofu Minde unawakumbusha Maaskofu na watumishi wote wa Kanisa umuhimu wa kutenga muda wa kuwa karibu na Mungu kwa njia ya sala, akimrejea Yesu Kristo ambaye mara nyingi alijitenga na umati ili kusali. "Kazi ya mchungaji mkuu ni kuwafikisha watu katika utakatifu.

Askofu Rogatus Kimaryo wa Jimbo Katoliki Same
Askofu Rogatus Kimaryo wa Jimbo Katoliki Same

Baba Askofu Minde ametukumbusha kwamba hata katikati ya majukumu mengi, Askofu anapaswa kutafuta muda wa kusali na kuimarisha uhusiano wake na Mungu," alisema. Aidha, alimnukuu Mtakatifu Yohane Maria Vianney, akisema sala ndiyo inayomuunganisha mwanadamu na Mungu na kumwezesha kubaki mwaminifu katika wito wake. Huduma ya kujitoa na unyenyekevu: Askofu Pisa pia alimpongeza Askofu Minde kwa mchango wake katika shughuli mbalimbali za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akisema ameonyesha uaminifu, uwazi na moyo wa kujitolea katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kuzitumikia. Alieleza kuwa pamoja na bidii yake katika kazi, Askofu Minde amejulikana kwa unyoofu, unyenyekevu na ukarimu wake, akisema hata katika mazingira ya kawaida amekuwa tayari kuwahudumia wengine kwa upendo. "Tunamshukuru Mungu kwa huduma yako katika Baraza la Maaskofu. Umeonyesha mfano wa uongozi unaojengwa katika kujitoa, unyenyekevu na utayari wa kuwahudumia wengine," alisema. Katika hatua nyingine, Askofu Pisa amewapongeza waamini wa Jimbo Katoliki Moshi kwa kuendelea kuishi imani yao kwa vitendo na kwa mchango wao katika kutoa watumishi wengi wanaohudumu katika taasisi mbalimbali za Kanisa nchini. Alibainisha kuwa mapadre kutoka Jimbo Katoliki Moshi wanaohudumu katika taasisi za Baraza la Maaskofu ni ishara ya ukomavu wa imani na moyo wa kimisionari unaoendelea kuimarisha utume wa Kanisa Tanzania. Akihitimisha salamu zake, Askofu Pisa alimtakia Askofu Minde afya njema, nguvu na neema ya kuendelea kutimiza mapenzi ya Mungu katika huduma yake ya kichungaji.

Waamini wakishiriki Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Minde
Waamini wakishiriki Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Minde

Askofu Rogatus Kimaryo wa Jimbo Katoliki Same, amesema Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Mhashamu Ludovick Minde ALCP/OSS ni tukio la neema na shukrani si kwa Jimbo Katoliki la Moshi pekee, bali pia kwa Majimbo ya Kahama na Kanisa lote Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika uinjilishaji wa kina na uongozi makini wa shughuli za kichungaji. Askofu Kimaryo alitoa kauli hiyo tarehe 4 Agosti 2026 wakati wa Ibada ya Masifu ya Jioni kuelekea kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Mhashamu Ludovick Minde ALCP/OSS tarehe 5 Agosti 2026 iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki Moshi. Mwanzoni mwa homilia yake, Askofu Kimaryo aliwapongeza waamini wa Jimbo Katoliki Moshi kwa kuadhimisha Jubilei ya Askofu wao, akisisitiza kuwa jubilei ya mchungaji ni furaha ya Jimbo zima. Pia aliwapongeza waamini wa Jimbo Katoliki Kahama, Askofu Mhashamu Christopher Ndizeye pamoja na viongozi na waamini wote wa jimbo hilo, akibainisha kuwa ndiko Askofu Ludovick Minde aliposimikwa kuwa Askofu na kuanza safari yake ya huduma ya kichungaji. Akirejea masomo ya siku, Askofu Kimaryo alisema Neno la Mungu linamkumbusha Mkristo ukweli kuhusu dhambi na neema ya Mungu. Alinukuu mafundisho ya Mtume Yohane kwamba anayesema hana dhambi anajidanganya, lakini neema ya Mungu ina nguvu kuliko dhambi zote za mwanadamu. Alieleza kuwa kwa mtazamo wa kitaalimungu, ushindi wa Mkristo haupatikani kwa nguvu zake mwenyewe bali kwa msamaha na huruma ya Mungu. "Tunasafishwa kwa msamaha wa Mungu, si kwa nguvu zetu wenyewe.

Watawa wakishiriki katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Askofu Minde
Watawa wakishiriki katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Askofu Minde

Neema ya Mungu ina nguvu kuliko dhambi yoyote ile," alisema Askofu Kimaryo. Akimrejea Mtakatifu Yohane Maria Vianney, msimamizi wa mapadre ambaye Kanisa lilikuwa linamkumbuka siku hiyo, Askofu Kimaryo alisema licha ya kuwa mtu wa kawaida, alijulikana kwa unyenyekevu, kuwa muungamishi mahiri, mfariji wa wagonjwa na mchungaji aliyewatafuta kondoo waliopotea. Alisema anamuona Askofu Ludovick Minde akiwa na sifa nyingi zinazofanana na Mtakatifu huyo, hususan katika upendo wake kwa Kanisa, elimu yake ya Maandiko Matakatifu na juhudi zake za kuimarisha maisha ya kichungaji. Aidha, alimpongeza Askofu Minde kwa kuendeleza kwa vitendo dhamira ya Kanisa ya kutembea pamoja kwa njia ya Sinodi, akibainisha kuwa hata baada ya Sinodi ya Maaskofu, Jimbo Katoliki Moshi limeendelea kutafakari na kutekeleza maono hayo kupitia Sinodi ya Jimbo.Akikumbusha Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA uliofanyika jijini Nairobi, Kenya, Askofu Kimaryo alisema ajenda ya Kanisa Afrika inaendelea kuelekeza nguvu katika kujenga Kanisa la Kimisionari na Kisinodi linalotembea pamoja, hasa kwa kuwashirikisha vijana. Katika sehemu nyingine ya homilia yake, Askofu Kimaryo alisema matunda ya huduma ya Askofu Minde yanaonekana wazi katika maendeleo ya kichungaji na miundombinu ya Jimbo Katoliki Moshi. "Hata kama kuna anayekuwa na mtazamo tofauti kuhusu Askofu Minde, jambo moja haliwezi kupingwa kwamba kazi imefanyika. Alipokuwa Kahama alikuwa kijana, lakini amekuja Moshi akiwa mzee kijana. Miradi na mafanikio yanayoonekana ni ushuhuda wa uongozi wake. Huenda siri yake iko katika kutembea pamoja, kushauriana na kutenda pamoja," alisema. Ibada ya Masifu ya Jioni ilikuwa ni sehemu ya maandalizi ya kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Mhashamu Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS iliyokusanya Maaskofu, mapadre, watawa na waamini kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kumshukuru Mungu kwa robo karne ya huduma yake ya kichungaji. Kwa waamini, Jubilei hiyo imeendelea kuwa nafasi ya kutafakari wito wa uongozi unaojengwa katika: huduma, unyenyekevu, ushirikiano, msamaha na kutembea pamoja, tunu ambazo Kanisa linaendelea kuziishi katika safari yake ya uinjilishaji.

Picha ya Pamoja kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25
Picha ya Pamoja kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25

Itakumbukwa kwamba, Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS alizaliwa tarehe 9 Desemba 1952 kwenye Parokia ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. Ni mtoto wa mzee Joseph Ndasika Minde na Mama Maria Joseph Mukure. Baada ya masomo yake Seminari Ndogo ya Mtakatifu James, Jimbo Katoliki la Moshi kunako mwaka 1979 alijiunga na Shirika la Mapadre wa Maisha ya Kitume na Kazi ya Roho Mtakatifu ALCP/OSS. Akaendelea na masomo yake ya falsafa Seminari kuu ya Kibosho na kuhitimisha masomo ya taalimungu kwenye Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Tarehe 26 Juni 1986 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 24 Aprili 2001 akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 5 Agosti 2001 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, akisaidiana na Askofu Mathew Shija, Muasisi wa Jimbo Katoliki la Kahama pamoja na Hayati Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki la Moshi. Itakumbukwa kwamba, Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS ni kati ya Mapadre watano walioteuliwa kwenda Roma kwa masomo zaidi baada ya hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania kunako mwaka 1990. Mtakatifu Yohane Paulo II alitaka kuimarisha malezi na makuzi ya majandokasisi kutoka Tanzania. Tangu mwaka 1990 hadi mwaka 1995 alikuwa mjini Roma akijifunza Maandiko Matakatifu na hatimaye, akajipatia Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma. Ni kati ya wanafunzi waliofanya vizuri sana katika masomo yao kwa mwaka huo. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Jaalimu wa Maandiko Matakatifu, Mlezi na Baba wa maisha ya kiroho, Seminari kuu ya Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Itakumbukwa kwamba, Jimbo katoliki la Moshi lilikuwa wazi baada ya Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Desemba 2017 kumteua Askofu Isaac Amani Massawe wa Jimbo Katoliki Moshi, kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo Kuu la Arusha, nchini Tanzania.

Askofu Minde

 

 

07 Agosti 2026, 16:15