Tafakari Dominika ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Siku ya 6 ya Babu, Bibi na Wazee Duniani
Na Padre Octavian O. Hinju, Jordan University College Morogoro, Tanzania.
Tungali bado katika muktadha wa jamii ya wakulima, masomo ya Dominika ya 17 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa yanatoa na kukazia kuhusu ufalme wa Mungu kama tunu yenye thamani, mwaliko kwa waamini kuwa tayari kuacha vyote ili kupata kile kilicho bora zaidi yaani ufalme wa Mungu. Yesu anafananisha ufalme wa Mungu na hazina iliyofichwa kondeni na lulu ya thamani kubwa; anayeipata huuza vyote alivyo navyo ili kuinunua. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Babu, Bibi na Wazee duniani tarehe 26 Julai 2026 unanogeshwa na kaulimbiu: "Sitakusahau kamwe." Rej. Isa 49:15. Hii ni siku maalum ya kuwakumbuka, kuwashukuru na kuwapongeza wazee kwa hekima na upendo wao, mwaliko kwa jamii kushikamana kwa dhati na wazee. Mwenyezi Mungu anaahidi kwamba, kamwe hatamsahau mja wake kwani amechora sura yake kwenye kiganja cha mikono yake na kwamba, upendo wake ni mkuu kuliko upendo kwa mama kwa mtoto wake. Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake kama rafiki, na kila mtu binafsi na kwa watu wote katika ujumla wao na hata leo hii maneno yake yanawahusu hata watu katika ulimwengu mamboleo: "Sitakusahau kamwe" yakisemwa moja kwa moja kwa kila mtu. Haya ni maneno yanayowajaza watu faraja na matumaini. Ni jibu kwa hisia chungu inayousumbua moyo: "Bwana ameniacha; Bwana wangu amenisahau" (Isa 49:14).
Mara ngapi katika Maandiko Matakatifu, hasa katika Zaburi, sala hutokana na kukata tamaa kwa wale wanaohisi kuwa maisha yao hayana thamani kwa mtu yeyote na kwamba wanapuuzwa! Kwa bahati mbaya, hisia chungu ya kusahaulika inashikiriwa na watu wengi, na miongoni mwao wamo wazee wengi. Upendo wa Mungu, ambao humkumbuka kila mtu, unajitokeza kama tendo la haki na jibu kwa hali ya kutoonekana au kusahaulika ambamo maisha ya binadamu mara nyingi hupotea. Maisha ya wazee wengi, hasa, yanaonekana kufunikwa na pazia linaloficha sura zao na kuwatumbukiza katika kusahaulika. Hivi ndivyo inavyotokea katika nyumba ambazo upweke hutawala, na pia katika vituo vya kutunzia wazee ambapo upekee wa kila mtu unaweza kupoteza thamani yake na kubaki kuwa namba ya kitanda au ugonjwa tu. Tuko ukingoni mwa Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, “Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa” AMECEA kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 26 Julai 2026 kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128. Kaulimbiu inayonogesha maadhimisho ya Mkutano huu ni “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu unafanyikia kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Jijini Nairobi, nchini Kenya.
Kama mfalme Sulemani aliyesali kuomba Hekima, basi Vijana wa Afrika Mashariki na Kati wanaitwa kwa Hekima ya kimungu kuwa kweli mabalozi wa amani, umoja na maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuhakikisha kwamba wanatumia kikamilifu: karama na vipaji vyao; elimu na teknolojia kwa manufaa ya jamii badala ya kuruhusu migawanyiko ya kisiasa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii inayoweza kukwamisha mustakabali wao. Vijana wanatakiwa kuwa ni vyombo na wajumbe wa Habari Njema ya Wokovu kwa kueneza ujumbe wa: Haki, amani, matumaini, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Dhamira kuu inayo bebwa na masomo ya dominika hii ni ufalme wa Mungu kama tunu yenye thamani, tunu ambayo hakuna anayeweza kuifananisha na kitu kingine chochote kile. Ufalme wa mbinguni ni zawadi inayohitaji hekima na busara ili kuweza kuipata. Katika moja ya mafundisho yao, Mababa wa Kanisa walifundisha kuwa hekima ya kimungu ni zaidi ya maarifa tu; ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli” (Yoh.1:14) ndiye Yesu Kristo, ambaye anarejesha sura na mfano wa Mungu ndani ya mwanadamu aliye asi kwa dhambi.
Mababa wa Kanisa waliona hekima kuwa zawadi ya Roho Mtakatifu inayomwezesha mtu kushinda dhambi na kutenda mema. Katika mafundisho yao ya msingi, walisisitiza mambo makuu yafuatayo: Mosi, Kristo ndiye hekima halisi ya Mungu. Mababa kama Mtakatifu Augustino wa Hippo na Mtakatifu Athanasius kwa pamoja walieleza kuwa Yesu ndiye Neno na hekima ya milele ya Mungu, iliyoshuka kutoka mbinguni ili kuwaokoa wanadamu na kuwafundisha siri za uzima wa milele. “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma (Yn 17:3).” Tunapo tafakari na kumwomba Mungu atujalie hekima basi tutambue kuwa hekima inapatikana kwa kuiishi vema fadhila ya unyenyekevu. Mababa wa Kanisa wanafundisha kuwa kiburi ni kikwazo kikubwa cha hekima, kwani kiburi kilimfanya Malaika akawa Shetani na unyenyekevu humbadili mwovu kuwa mtakatifu. Kumbe, ili mtu awe na hekima ya kiroho, lazima awe mnyenyekevu, atubu dhambi zake, na kuishi maisha matakatifu; kwa kufanya hivyo mtu hujizolea matunda ya hekima. Hekima ya kimungu huzaa matunda yanayoonekana kama vile amani, upole, huruma, na haki tofauti na hekima ya kidunia. Leo tunaonywa vikali dhidi ya hekima ya ulimwengu huu inayotegemea akili tupu au faida za kibinafsi, mababa wa kanisa wanasisitiza kuwa hekima ya kweli inamweka Mungu kwanza na inasimama katika kweli na upendo. Hekima ni karama inayomwezesha mtu kutambua kwa furaha mpango wa Mungu katika mambo yote. Hekima ni ya msingi sana katika maisha ya mwanadamu kwani hutusaidia kung’amua lililo jema na kulifuata.
Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Kwanza cha Wafalme (1 Wafal. 3: 5, 7-12). Somo hili linaelezea namna ambavyo Mfalme Sulemani alitumia hekima kuomba moyo wa utambuzi na wenye hekima badala ya mali au maisha marefu. Mungu anajibu maombi yake kwa kumpa hekima kuu. Itakumbukwa kuwa sura 10 za mwanzo za kitabu hiki cha kwanza cha Wafalme zinaeleza kuhusu hekima na mafanikio ya Sulemani kama Mfalme na mtawala wa taifa teule la Mungu. Katika somo la kwanza siku ya leo linazungumza kuhusu kuanza kwa utawala wake, ambapo Sulemani anatambua kipi kinapaswa kupewa uzito katika jukumu hili la kuwaongoza watu wa Mungu na kipi hakina maana katika maisha yake kama kiongozi na ndipo alisali kuomba akisema “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, umeniweka mimi mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, ijapokuwa ningali mtoto mdogo na sijui namna ya kutekeleza wajibu huu. Na hapa umeniweka kati ya watu wako ambao umewachagua; nao ni wengi hata hawawezi kuhesabika kwa wingi wao. Kwa hiyo, nakuomba unipe mimi mtumishi wako moyo wa kusikia ili kuamua watu wako, niweze kutambua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuhukumu watu wako walio wengi hivi? (1 Wafal. 3:7-9)”. Ombi hili halikuwa tu katika kutambua mema na mabaya. Itakumbukwa kuwa katika nahau za Kiebrania ombi hili lilimaanisha kujaliwa maamuzi mema na thabiti, hekima na maadili katika kuamua na uongozi makini wa watu wa Mungu. Kumbe jukumu la kwanza la Mfalme lilikuwa kuamua na Kutenda kwa haki. Sulemani ni mfano mwema kwa viongozi na wote wenye kushika mamlaka, kushukuru kwa nafasi wanazo pewa kuwatumikia watu. Nao watende kwa upole, huruma, upendo na unyenyekevu na pia watambue kwamba uongozi ni huduma kwa wale waliowekwa chini yao na si kitu cha kuonea ufahari na sifa zisizo na tija kwa watu wa Mungu. Uongozi bora wenye kuzaa matunda mema ni ule unao ongozwa kwa nguvu na hekima ya Mungu. Mfalme Sulemani alirithi kiti cha ufalme kutoka kwa baba yake yaani mfalme Daudi. Taifa alilokabidhiwa halikuwa dogo bali kubwa lenye utajiri mwingi. Kumbe uamuzi wa Sulemani kuomba hekima haukumletea mwangaza yeye kama mtu binafsi tu lakini pia Mungu anamjalia uwezo wa kuwaongoza watu wake kwa haki na ufahamu. Moyo wa Sulemani ulifungamana na mpango wa Mungu, ambao ulimwongoza kutafuta kile kilicho cha thamani.
Somo letu la kwanza siku ya leo linataka tufahamu kuwa wakati Mfalme Sulemani anaanza kuwaongoza watu wa Mungu, hekalu la Yerusalemu bado halikuwa limejengwa, Sanduku la Agano lilikuwa limehifadhiwa katika hema la muda huko Gibeoni nje kidogo ya mji mtakatifu wa Yerusalemu. Sulemani alikwenda kuhiji ili kumtolea Mungu sadaka na kuomba ulinzi kwa taifa lake. Ndipo Mungu alipo mtokea na kumpa nafasi ya pekee ya kuomba kitu toka kwake (1 Wafal. 3:5). Kwa imani Sulemani aliomba hekima ya kuwaongoza watu wa Mungu kwani aliamini katika kuzishika kanuni na miongozo ya Bwana. Huku ni kuyaishi mausia ya Mzaburi anayetukumbusha kwamba sheria ya Bwana ni hazina kubwa kuliko mali na utajiri, anaposali akisema hivi, “Naipenda sana sheria yako. Naitafakari mchana kutwa. Amri yako iko nami daima, yanipa hekima kuliko maadui zangu. Ninaelewa kuliko waalimu wangu wote, kwa kuwa nayatafakari maamuzi yako (Zab. 199:72-74). Haya ni maneno mazuri yenye kuitia roho nuru na furaha, ambapo mfalme Daudi anadhihirisha upendo na utii wake kwa neno la Mungu. Ni uamuzi mzuri wa kufuata sheria na maagizo ya Mungu kuliko utajiri wowote wa kidunia. Ni kupitia mang’amuzi haya ya kimungu na miongozo yake ndipo tunapata furaha na kusudi la kweli kwenye utume na maisha yetu. Kiitikizano cha zaburi yetu ya leo “sheria yako naipenda mno ajabu” (Zab. 199: 97), kadhalika kinatoa wito wa kutafuta furaha zetu si katika faraja za kidunia zipitazo bali katika ukweli wa kimungu. Mfalme Sulemani alidhirisha hekima kwa kuonyesha kwanza kuto kustahili kwake mbele za Mungu, uzoefu mdogo alionao katika uongozi na ukweli kwamba ni kwa wema na ukarimu wa Mungu tu ndio maana amepewa dhima hiyo tofauti na baba yake aliye amua kumteua yeye ashike wadhifa huo badala yake.
Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:28-30). Waraka huu unalenga kutukumbusha kwamba Mungu hutenda mambo yote kwa wema kwao wote wampendao. Uthibitisho huu unatoa faraja ya kweli kwetu hasa pale tunapopitia magumu na changamoto za maisha. Mungu ndiye anaye panga na kuzisimamia kazi na mipango yote katika maisha ya mwanadamu. Anatualika na sisi kuweka tumaini letu katika hekima yake kama alivyofanya Mfalme Sulemani. Mtume Paulo anaeleza kwamba Mungu alituchagua tangu milele, hivyo maisha yetu yamo katika umilele wake Mungu. Kwa ubatizo na maisha ya kisakramenti katika Kanisa tumeshirikishwa uzima huu kwa njia ya Kristu. Katika somo la Injili yetu ya leo kama ilivyo andikwa na Mathayo (Mt. 13:44-52) tunaelezwa kuhusu mfano wa hazina yenye thamani kubwa iliyofichwa. Yesu analinganisha Ufalme wa Mungu na kitu cha thamani kubwa, “lulu iliyo njema au hazina kubwa sana.” Ufalme wa Mungu unajitokeza katika maisha yetu ya kawaida. Historia inasema kuwa Waisraeli walikuwa na kawaida ya kuficha vitu vya thamani ardhini katika mashamba yao wakati wa misukosuko ya kivita, maisha yalipokuwa hatarini. Pia iliwawia wevi na wanyang’anyi vigumu kugundua mali imelala wapi. Mwenye mali alipokufa bila kumuonesha mrithi, au alipokaa mbali muda mrefu, mali ilidumu ardhini. Kama mtu aliigundua mali iliyofichwa katika shamba la mwingine, hakuwa na haki ya kuitwaa mali ile kama yake. Njia ya kuipata mali hiyo ilikuwa kulinunua shamba ili liwe mali yake. Baada ya kufanya hivyo hazina zote chini ya ardhi zinakuwa zake. Katika mfano huu mkulima aliyeiona hazina aliificha zaidi ili ibaki salama hadi hapo atakapokamilisha mipango ya kumiliki shamba.
Ni kwa kawaida mtu anakuwa na furaha sana pale anapopata kitu cha thamani kubwa na anaona kuwa mengine yote aliyonayo si kitu. Kwa urahisi furaha na hiari, mtu huvitoa vitu vya zamani ili avipate vipya. Kwa furaha anauza yote aliyonayo na ananunua lile shamba lenye hazina. Vivyo hivyo enzi zile lulu zilikuwa na thamani sana, hata kuzidi dhahabu, ziliuzwa kwa bei kubwa. Wafanyabiashara walisafiri mbali kuzisaka lulu. Mfanyabiashara alikuwa tayari kuuza yote aliyonayo ili kuipata lulu ya thamani. Kwa mfano huu tunakumbushwa kwamba ufalme wa mbinguni upo nasi, ingawa ufalme huo ni Zawadi kwetu lakini bado si jambo lenye kutujia kwa wepesi bali linatutaka kuuwajibikia ufalme huo. Ndio maana katika Injili tumesikia kuwa “ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile (Mt.13:44). Hazina iliyofichika shambani na lulu yenye thamani kubwa kwa pamoja vinaelezea thamani ya ufalme wa mbinguni wenye kuhitaji kila aina ya tone la sadaka tunayoweza kuitoa ili kuupata. Tunapo tambua thamani ya uhusiano wetu na Mungu, kama mfanyabiashara na yule kibarua basi tutoe kila tunu tuliyo jaliwa ili kuipata lulu na hazina tunayoitamani. Katika adhimisho la Ekaristi Takatifu siku ya leo, Bwana wetu Yesu Kristu anatuuliza kila mmoja wetu maswali haya; kitu gani ni cha thamani sana kwako? Yaani kile unacho dhani kwamba bila hicho huwezi kuishi? Je, tunajidhatiti kwa kiasi gani kuachana na fahari za dunia hii au bado tunajishkamanisha na Fahari hizo? Je tuna tafuta hekima ile itokayo kwa Mungu? Basi daima tumuombe Mwenyezi Mungu atujalie roho ya hekima na busara ya kuweza kujua kuwa ufalme wake ni wa thamani kuliko malimwengu yote. Tuutafute kwa nguvu na juhudi zote nasi tukiisha kuupata tufurahi milele kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.