Tafakari Dominika 16 Mwaka A wa Kanisa: Uvumilivu, Huruma na Ukuu wa Mungu
Na Padre Octavian O. Hinju-Jordan University College, Morogoro, Tanzania
Masomo ya Dominika hii ya 16 ya Mwaka A wa Kanisa yanalenga zaidi katika kutoa fundisho kuhusu uvumilivu, huruma, na ukuu wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya mwanadamu sanjari na kuonesha jinsi Mungu asivyo na haraka ya kuwaadhibu wanadamu, badala yake anatoa nafasi ya kutubu na kumwongokea kupitia mifano kama ule wa magugu na ngano (Mt. 13: 24-43) na mbegu ya haradali. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo, (1 Sam 16:7). Zamani katika moja ya mafundisho yake Mwanataalimungu Karl Rahner aliyepata kuwa Mwana taalimungu maarufu sana, aliitaja huruma kuwa ndiyo sifa kuu ya Mwenyezi Mungu. Pengine hii ni kwa sababu ya anguko la wazazi wetu wa mwanzo yaani Adamu na Eva anguko ambalo lilipelekea mahusiano kati ya Mungu na mwandamu yaharibike na kuchukua sura mpya. Mababa wa Kanisa wanaeleza kuwa uhusiano wa Mungu na mwanadamu ulitafsiriwa katika mtazamo wa huruma na upendo. Huruma hii ya Mwenyezi Mungu inaelezwa kwa namna mbalimbali ili mwanadamu aweze kuilewa, kuipokea, kuifurahia na kuiishi. Upole, uvumilivu na unyenyekevu ni moja kati ya fadhila za kikristu zinazo tumika kueleza namna huruma ya Mungu inavyo fanya kazi katika maisha ya watu wake. Uvumilivu humwonyesha Mungu mwenye huruma pale anapotupatia nafasi ya pili ili tujisahihishe hasa tunaposhindwa kuliamini neno lake. Wana wa Israeli walishindwa kuamini kuwa ni Mungu ndiye anaye waokoa nao wakamlalamikia mtumishi wake Musa (Kut. 14:11-12).
Malalamiko yao makuu yalijikita katika mambo yafuatayo: ukosefu wa chakula na maji (Kut. 17:3), walilalamika walipokosa chakula kwani walitamani nyama na vyakula vya Misri (Kut. 16:2-3) na walipokuta maji ni machungu. Hofu ya kuangamizwa (Kut.14:10-11), walimlaumu Musa pindi walipojikuta wamezingirwa, kama vile walipofika Bahari ya Shamu na jeshi la Farao likiwa nyuma yao. Uchovu wa Jangwani: Walichoka kutangatanga na mara kwa mara walitamani kurudi utumwani Misri badala ya kufa jangwani. Kutengwa na Viongozi wengine: Katika tukio jingine, Kora, Dathani, na Abiramu walimwasi Musa na Haruni wakidai wanajikweza zaidi ya wengine. Katika kila tukio, Musa aliikimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya sala ili kupata jawabu, na Mungu aliwajalia miujiza kama vile kuwanyeshea Mana na Kware ili wale, na maji kutoka kwenye mwamba ili wanywe. Kumbe katika hali hizi zote Mungu hakuwaonesha hasira bali huruma, wema na msamaha. Katika hali ya namna hii masomo ya Dominika hii ya 16 ya mwaka A yanaendelea kutufundisha ukuu wa huruma ya Mungu na inayojikita katika uvumilivu wake; kwani mwenyezi Mungu hana pupa wala haraka katika kumuadhibu yeyote anayekosea kwa kutenda dhambi. Mungu anatoa nafasi ya mtenda maovu kubadilika ndio maana anamuacha mtu aendelee kuishi pamoja na wale walio wema mpaka wakati wa hukumu ya mwisho. Uvumilivu huu wa Mungu unatupata nafasi kuifaidi huruma yake kwa kufanya toba kwa wakati ili hukumu ya mwisho isitutie hatiani; hivyo tuna himizwa sana kuto iipuuzia hata mara moja Sakramenti ya Kitubio.
Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek. 12:13, 16-19). Somo hili linelezea ukuu na uweza wa Mungu katika kuyatenda yote, tena anao uwezo wa kuadhibu mabaya na kulipa mema. Lakini ni kwa Hekima yake Mungu anawavumilia na kuwahurumia watu ijapo pengine binadamu sababu ya huruma yake Mungu hudhani kuwa hawezi kuwapitiliza. Kumbe hii ni nafasi nyingine ya kuonja uvumilivu wa Mungu unaotutaka kutubu dhambi zetu ili kufurahia utukufu wake. Ifahamike kuwa kwa kufanya hivi si kwamba Mungu anapunguza uwezo wake, la hasha. Ni katika upole na uvumilivu ndipo anapoonesha uwezo wake mkubwa alionao. Tunapolisikia somo hili na kulitafakari pamoja na ujumbe mbalimbali wa manabii, tunaona kuwa upole na uvumilivu wa Mungu una lengo moja tu, kumvuta mwanadamu mkosefu katika toba, abadili njia isiyofaa ili apate wokovu. Somo la pili linalotoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8: 26-27). Somo hili linaeleza udhaifu alio nao mwanadamu, udhaifu ambao una athiri pia sala zake mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini kwa sababu Roho wa Mungu yupo ndani mwetu, basi sala zetu zinapata maana na mastahili ya kusikilizwa na Mungu. Mtume Paulo anaeleza kuwa Mwenyezi Mungu hamwachi mwanadamu peke yake katika njia ya udhaifu. Humtuma Roho wake ili amsaidie kurudi kwake. Somo linasema “Roho hutusaidia katika udhaifu wetu”. Tena na hata pale ambapo hatujui namna ya kusali, namna ya kutafuta njia ya kurudi kwa Baba, ni Roho huyo ambaye husali ndani yetu kwa uchungu mkubwa usioelezeka ili kuifanya sala yetu ipokelewe kwa Mungu. Huu ndio ukuu wa huruma na upendo wake ambao Mzaburi alipo utafakari alisli akisema hivi, “tazama Mungu ndiye anayenisaidia, Bwana ndiye anayeitegemeza nafsi yangu. Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu Ee Bwana nitalishukuru jina lako maana ni jema. Ee Mungu uyasikie maombi yangu, uyasikilize maneno ya kinywa changu (Zab. 54:4,6).
Injili ni kama ilivyo andikwa na Mathayo (Mt. 13:24-43). Somo hili la Injili linatupa mifano mitatu ambayo Yesu mwenyewe ndiye anayeitoa. Mfano wa kwanza ndio huo wa magugu na ngano. Mfano wa pili ni wa punje ya haradali ambayo ni ndogo kabisa kama punje ya mchicha lakini ikipandwa inazaa mti mkubwa ambao ndege huja na kuweka viota. Mfano wa tatu na wa mwisho ni wa hamira ambapo kiasi kidogo tu kinatosha kuumua kiasi kikubwa cha unga uliokandwa. Kristu anatumia mifano hii ili kutueleza hali mbalimbali za Kanisa lake. Mwanzo wake ni duni na haujulikani sana; daima huambatana na matatizo. Lakini mwishowe litakuwa kubwa lenye ustawi na matunda yenye kuwafurahisha wote. Katika mifano mitatu, inayotolewa leo ni ule wa kwanza, yaani ule wa magugu na ngano unaobeba dhamira kuu ya tafakari yetu katika Dominika hii ya 16A. Katika mfano wa kwanza tunaelezwa kuhusu uvumilivu wa Mungu. Yeye amepanda mbegu njema ya ngano kondeni mwake, lakini kwa hila yake adui amekuja akapanda magugu ili kuharibu ngano. Hali hii pengine inaendelea hata leo kukua na kushamiri katika wanadamu walio wengi. Kwa kuendeshwa na chuki na hila wamepitia milango ya nyuma ili kuwaumiza wengine kwa siri. Punde wanapogundulika pengine malipo na stahili yao ni adhabu ili wajue uzito wa makosa yao. Ndiko huko kunako itwa kupalilia yaani kung’oa na kutupa motoni. Haya huenda ni maamuzi yenye hasira ndani mwake. Kinyume na desturi hii ya kuadhibu, katika mfano huu tunaweza kujihoji labda kwa nini mwenye shamba hafanyi mara moja palizi kuondoa magugu?
Kwa nini Mungu haangamizi mara moja waovu wote ili duniani wabaki wema tu? Tutambue kwamba palizi inayohitajika hapa maana yake ni maamuzi magumu ya kung’oa magugu katika shamba. Ni vema kutambua kuwa palizi ya namna hiyo inaweza ikaangamiza hata baadhi ya ngano ambazo ndio kusudio na tumaini la mkulima. Hapa tunajifunza subira na uvumilivu katika kutenda mambo. Mwenyezi Mungu anapenda kutufundisha kwamba katika subira na uvumilivu wetu kuna nafasi ndani yake wa mtu mwovu kuguswa na huruma ya Mungu na kutubu. Pili tukiangalia mifano ile miwili inayofuata, mifano inayoonesha kuwa kutoka mbegu ndogo ya haradali unazaliwa mti mkubwa na kwamba kiasi kidogo tu cha hamira kinaumua pishi kubwa, Mungu anaonesha matumaini kuwa hata katika mwovu kuna chembechembe ndogo ya wema inabaki ndani yake. Na hiyo chembechembe hata kama ni ndogo kiasi gani ina uwezo wa kumsukuma mtu afikie toba na wongofu. Uvumilivu wa Mungu ni kusubiri ili hiyo chembechembe ndogo kabisa ya wema iliyo ndani ya watu wake ikue iwafikishe wakosefu na wadhaifu katika wongofu. Tusali leo kuomba neema ya MUNGU ili itufae kufanya tathmini ya maisha yetu na pale penye kasoro tusikawie kumrudia Mwenyezi Mungu kwani anasema kuwa nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya (Yoeli 2:12-17).