Tafuta

AMECEA 21 Nairobi Kenya: Vijana wasisitiza Kanisa liwaone kama washirika wa leo katika uinjilishaji, uongozi na ujenzi wa jamii yenye matumaini. AMECEA 21 Nairobi Kenya: Vijana wasisitiza Kanisa liwaone kama washirika wa leo katika uinjilishaji, uongozi na ujenzi wa jamii yenye matumaini. 

Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA: Wito Kutoka Kwa Vijana wa AMECEA

Vijana kutoka nchi mbalimbali za Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA wamewaomba Maaskofu kuendelea kuwashirikisha kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, wakisisitiza kuwa wao si Kanisa la kesho pekee, bali ni Kanisa la leo linalostahili kusikilizwa, kuaminiwa na kupewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao na mustakabali wa Kanisa katika ujumla wake. Changamoto, Matarajio na Mtazamo!

Na Fredy William - Nairobi, Kenya

Kaulimbiu inayonogesha Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, “Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa” AMECEA kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 26 Julai 2026, kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128 ni: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu unafanyikia kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Jijini Nairobi, nchini Kenya. Sifa na utukufu apewe Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, kwani ni katika mukadha huu, AMECEA inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 65 ya umoja, ushirika na mshikamano wa shughuli za kichungaji na huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni umoja ulioanzishwa kunako mwaka 1961na unasimikwa na kufumbatwa katika tofauti mbalimbali kutoka katika nchi tisa wanachama ambazo ni: Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan Kongwe, Sudan ya Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia. Itakumbukwa kwamba, Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji.

AMECEA kwa Miaka 4 Kipaumbele ni kwa vijana wa kizazi kipya
AMECEA kwa Miaka 4 Kipaumbele ni kwa vijana wa kizazi kipya

Vijana kutoka nchi mbalimbali za Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA wamewaomba Maaskofu kuendelea kuwashirikisha kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, wakisisitiza kuwa wao si Kanisa la kesho pekee, bali ni Kanisa la leo linalostahili kusikilizwa, kuaminiwa na kupewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao na mustakabali wa Kanisa katika ujumla wake. Wito huo umetolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA unaoendelea katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA), Nairobi, Kenya, ambapo vijana waliwasilisha ujumbe wao rasmi mbele ya Maaskofu kutoka nchi wanachama wa AMECEA. Katika ujumbe wao, vijana waliwashukuru Maaskofu kwa kuwapa nafasi ya kushiriki mkutano huo mkubwa wa Kanisa, wakieleza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya kuwajumuisha vijana katika safari ya Kisinodi na ujenzi wa Kanisa la Kimisionari kwa kusikilizana na kutembea pamoja.

Vijana wametaja fursa, matatizo na changamoto za maisha
Vijana wametaja fursa, matatizo na changamoto za maisha

"Tunawaomba mtuone kama Kanisa la sasa, si Kanisa la baadaye. Tupokeeni, tusikilizeni na tuaminini kwamba hata sisi tuna mchango wa kujenga Kanisa na jamii," walisema vijana hao. Vijana walieleza kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Kanisa kupitia mapadri, watawa na walezi wa vijana, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji ushirikiano wa karibu zaidi kati ya viongozi wa Kanisa na vijana wenyewe. Walitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa ajira, ukata na ugumu wa maisha; changamoto za afya ya akili, migogoro ya kifamilia na kijamii; matumizi yasiyo salama ya mitandao ya kijamii, pamoja na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia ya kidijitali ambayo yanahitaji Kanisa kuwekeza zaidi katika uinjilishaji wa kidijitali (Digital Evangelization.) Aidha, vijana walibainisha kuwa kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo kupitia semina za uongozi, malezi ya kikristo, elimu ya ndoa na familia, pamoja na mafunzo ya stadi mbalimbali za maisha zitakazo wasaidia kukua kiimani, kiutu, kimaadili na kiuchumi. Walisisitiza kuwa uwekezaji kwa vijana ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa Kanisa na jamii.

Maaskofu wa AMECEA wameahidi kuwasikiliza, kuwathamini na kuwashirikisha
Maaskofu wa AMECEA wameahidi kuwasikiliza, kuwathamini na kuwashirikisha

Mapendekezo vya Vijana wa Kizazi Kipya Kwa AMECEA: Katika mapendekezo yao, vijana waliomba Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA, kuimarisha huduma kwa vijana kupitia hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzisha madawati ya vijana katika maeneo yote ya AMECEA, kuongeza mafunzo ya uongozi na uinjilishaji, kuandaa mijadala ya mara kwa mara kati ya Maaskofu, mapadri na vijana, pamoja na kuwekeza katika elimu ya maisha, ndoa, afya ya akili na maendeleo ya kiuchumi kwa vijana. Vilevile walisisitiza umuhimu wa kuwapa vijana vifaa na maarifa ya kidijitali ili waweze kutumia teknolojia kama chombo cha kueneza Injili, kujijengea ajira na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Mapendekezo ya vijana yamepokelewa kwa mikono miwili
Mapendekezo ya vijana yamepokelewa kwa mikono miwili

Maaskofu wa AMECEA wahakikishia ushirikiano: Akijibu ujumbe huo kwa niaba ya Maaskofu wa AMECEA, Askofu Charles Sampa Kasonde, wa Jimbo Katoliki Solwezi, Zambia ambaye ni Mwenyekiti wa AMECEA anasema, Mkutano huu unakuwa ni chemchemi halisi ya matumaini na wakati wa neema kubwa kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati. Hii ni fursa ya kupembua kwa kina na mapana: Matatizo, changamoto na fursa katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, Kanisa linaendelea kutembea bega kwa bega na vijana na kuthamini mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa. Ameeleza kuwa tayari AMECEA ina Idara ya Vijana inayoratibu huduma kwa vijana katika nchi wanachama, huku akiahidi kuwa mapendekezo yote yaliyowasilishwa yatafanyiwa kazi katika: Sera, mipango na shughuli za kichungaji za AMECEA. "Tunawashukuru kwa mawazo yenu. Tumeyapokea na tunawahakikishia kuwa tutaendelea kutembea pamoja nanyi. Vijana ni sehemu muhimu ya Kanisa letu, na tuna wajibu wa kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa," alisema Charles Sampa Kasonde.

Maaskofu wa AMECEA wataendelea kutembea bega kwa bega na vijana
Maaskofu wa AMECEA wataendelea kutembea bega kwa bega na vijana

Aliongeza kuwa AMECEA itaendelea kuimarisha ushiriki wa vijana katika ngazi mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa ili wawe mabalozi wa Injili, haki, amani na matumaini katika Bara la Afrika. Uwasilishaji wa ujumbe huo umeakisi kwa vitendo mwelekeo wa Safari ya Kisinodi unaosisitiza Kanisa linalosikiliza, kushirikisha na kutembea pamoja na waamini wote. Kupitia sauti zao, vijana wa AMECEA wameonesha kuwa wanatamani Kanisa linalowaamini, linalowawezesha na linalowapa nafasi ya kutumia vipaji na karama zao katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Askofu Charles Sampa Kasonde amekaza kusema, vijana kwa kipindi cha miaka minne kuanzia sasa wanapewa kipaumbe cha kwanza katika nchi za AMECEA katika kuwaenzi, kuwashirikisha, kuwarithisha imani sanjari na ushiriki wao katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, kama sehemu muhimu sana ya uinjilishaji. AMECEA inakazia kwa namna ya pekee: umoja, ushiriki, haki, amani, Injili ya matumaini sanjari na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kwamba azma hii sasa inapaswa kutafsiriwa kwa vitendo. Katika Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA, ujumbe wao umebeba mwaliko kwa Kanisa kuendelea kuwa karibu na vijana, ili kwa pamoja wajenge madaraja ya umoja, tumaini, haki na utawala bora, kwa ajili ya mustakabali wa Kanisa na Bara la Afrika.

Maaskofu wamesikiliza maoni, changamoto na fursa za vijana
Maaskofu wamesikiliza maoni, changamoto na fursa za vijana

Kwa upande wake Askofu mkuu Maurice Muhatia Makumba wa Jimbo kuu la Kisumu na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, ameonya kwamba kupuuza mahitaji, changamoto na mchango wa vijana wa kizazi kipya si tu ni uzembe bali ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha sana na kwamba, hizi ni dalili za kutowajibika kikamilifu. Kanisa linakusudia kuwasikiliza kwa makini vijana wa kizazi kipya, ili kutambua kile ambacho Roho Mtakatifu anasema kupitia kwa maisha, vipaji, karama na shauku yao. Hii ni changamoto kwa wazazi kuhakikisha kwamba, wanawekeza katika nidhamu, hekima na akili, ili hatimaye, vijana waweze kuwa na utaratibu katika maisha.

Vijana washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa
Vijana washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa

Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2026 yalinogeshwa na kauli mbiu “Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu.” Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia mintarafu matumizi ya teknolojia ya akili unde “Artificial Intelligence” anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika kukuza na kudumisha mawasiliano yanayoheshimu, kulinda na kudumisha: Utu, heshima, haki msingi za binadamu na ukweli ambao kimsingi ni kanuni elekezi ya kila uvumbuzi wa kiteknolojia unaofanywa na mwanadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, uvumbuzi wa teknolojia, hasa matumizi ya teknolojia ya akili unde, inamhudumia binadamu badala ya kuchukua nafasi au kupunguza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anasema, nyuso na sauti za binadamu ni za kipekee, sifa bainifu za kila mtu; zinafichua utambulisho wa mtu mwenyewe usioweza kurudiwa na ni vipengele vinavyobainisha vya kila kukutana na wengine.

Changamoto; maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano
Changamoto; maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anataadharisha kuhusu athari za matumizi ya teknolojia ya kidigitali na akili unde kwa kukazia wajibu wa watoto, vijana, wazazi na walezi kwa kujizoesha kutumia kwa kiasi na kwa nidhamu vyombo vya upashanaji habari, wakiwa na lengo lakufahamu sawasawa kila wakionacho, wakisikiacho na kile wanachosoma. Haya ni mambo wanayopaswa kujadili pamoja na walezi na wataalam wa mambo haya. Waraka wa kwanza wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” umezinduliwa rasmi tarehe 25 Mei 2026.

Ujumbe wa Vijana wa AMECEA
22 Julai 2026, 10:40