Tafuta

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, achaguliwa kuwa Rais mpya na Mheshimiwa Padre Andrew Kaufa kuwa Katibu mkuu mpya wa AMECEA kwa kipindi cha Miaka minne. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, achaguliwa kuwa Rais mpya na Mheshimiwa Padre Andrew Kaufa kuwa Katibu mkuu mpya wa AMECEA kwa kipindi cha Miaka minne. 

Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA: Ibada ya Misa na Viongozi Wapya! Askofu Mkuu Nyaisonga

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, achaguliwa kuwa Rais mpya na Mheshimiwa Padre Andrew Kaufa kuwa Katibu mkuu mpya wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Baada ya kutangazwa rasmi, Dominika tarehe 26 Julai 2026 Askofu mkuu Nyaisonga ameongoza Adhimisho la Ibada yaMisa Takatifu ya Kilele cha Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 21 wa AMECEA : Kanisa chanzo cha matumaini, umoja na ushirika.

Na Fredy William - Nairobi, Kenya

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, achaguliwa kuwa Rais mpya na Mheshimiwa Padre Andrew Kaufa kuwa Katibu mkuu mpya wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Baada ya kutangazwa rasmi, Dominika tarehe 26 Julai 2026 Askofu mkuu Nyaisonga ameongoza Adhimisho la Ibada yaMisa Takatifu ya Kilele cha Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 21 wa AMECEA ambapo katika mahubiri yake yake, ametoa wito kwa Kanisa kuendelea kuwa chanzo cha matumaini kwa vijana na kutembea nao kama familia moja ya Mungu. Amelitaka Kanisa la Afrika Mashariki na Kati kuendelea kujenga sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazo mizizi yake kama chemchemi ya matumaini, umoja na ushiriki wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa, akisisitiza kuwa lengo kuu la AMECEA ni kuwaongoza waamini wote kuufikia Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika: Kweli na uzima, huu ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Huu ni mwaliko kwa waamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kujenga na kudumisha upendo, unaoweza kuzaa matunda na kwamba, upendo huu unahitaji kuzingatia mambo makuu matatu: kujitenga, kupoteza, mambo yanayosimikwa katika ukarimu.

Askofu mkuu Gervas Nyaisonga Rais wa AMECEA
Askofu mkuu Gervas Nyaisonga Rais wa AMECEA

Akiadhimisha Misa Takatifu ya kilele cha Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA), Askofu mkuu Nyaisonga alianza kwa kumshukuru Mungu kwa huduma ya Askofu Charles Sampa Kasonde, aliyeliongoza Baraza hilo kwa mafanikio katika kipindi cha miaka minane iliyopita. "Si maajabu tu bali ni mstuko kuchukua nafasi ya Askofu Charles Sampa Kasonde ambaye ameiongoza AMECEA kwa mafanikio makubwa kwa zaidi ya miaka minane. Tunamshukuru Mungu kwa makuu aliyotutendea kupitia uongozi wake," alisema. Akitafakari kaulimbiu ya Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA, Askofu mkuu Nyaisonga amesema washiriki wa mkutano huo wamealikwa kutembea pamoja na vijana kama familia moja ya Mungu inayowajibika na kusikilizana, wakitafuta kwa pamoja njia bora za kujibu changamoto za kizazi kipya katika nyanja za uchumi, maendeleo ya jamii, teknolojia na maisha ya kiroho, maadili na utu wema. Alisisitiza kuwa maamuzi yote yanayofanywa ndani ya AMECEA yanapaswa kuelekezwa katika kuwasaidia watu kuishi maisha yanayowastahilisha kuurithi Ufalme wa Mungu. "Tunataka kufanya maamuzi sahihi si kwa ajili ya vijana pekee bali kwa ajili ya watu wote wa Mungu. Pale tunaposhindwa kuona na kufanya maamuzi yanayofaa ndipo tunapopotea, na huo si mpango wa Mungu kwetu. Kila jambo tunalofanya ndani ya AMECEA linapaswa kutuelekeza katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu," alifafanua. Akirejea Somo la kwanza, Askofu mkuu Nyaisonga alisema mfano wa Mfalme Solomoni unawakumbusha viongozi wote wa Kanisa umuhimu wa kumtegemea Mwenyezi Mungu katika uongozi wao. Alibainisha kuwa hekima ya kweli ya uongozi hutokana na moyo unaomsikiliza na kumcha Mungu; na kutafuta kutenda yaliyo mema mbele zake. Aidha, amewaomba waamini kuwaombea viongozi wapya wa AMECEA pamoja na Maaskofu wote wanaobeba dhamana ya kuliongoza Kanisa katika eneo la Afrika Mashariki na Kati ili watende vyema utume wao wa kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha vyema watu wa Mungu ili waweze kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Shirikisho la Mabaraza ya Maskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati
Shirikisho la Mabaraza ya Maskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati

Katika sehemu nyingine ya mahubiri yake, Askofu mkuu Nyaisonga amezungumza kwa namna ya pekee kuhusu hali ya vijana, akisema wengi wao wanahisi kutengwa na kukosa nafasi katika jamii. Hata hivyo, aliwahimiza vijana wasikate tamaa bali wamtegemee Roho Mtakatifu ambaye huleta uzima, mwanga na uhuru katika maisha na utume wa Kanisa. Akirejea Injili Takatifu, amesema Kristo Yesu anaendelea kuwakaribisha waamini kumfuata kwa moyo wote, wakiamini kuwa anayemkabidhi maisha yake Kristo Yesu hataachwa kamwe. "Hatuna muda tena wa kuwaondolea watu matumaini. Vijana, mnapojisikia wanyonge, fungulieni vipaji na hamasa mlizopewa na Mungu. Mnaishi katika dunia ya teknolojia na mapinduzi ya kidijitali; vitumieni vipawa hivyo kwa ajili ya kumtukuza Mungu na kuijenga jamii," alisisitiza. Akihitimisha mahubiri yake, Askofu mkuu Nyaisonga alisema AMECEA itaendelea kuwa ishara ya umoja wa Kanisa Barani Afrika kwa kuimarisha ushirikiano kati ya Mabaraza ya Maaskofu na kuendeleza maisha na utume wa uinjilishaji unaoongozwa na Roho Mtakatifu. Alieleza matumaini yake kwamba kwa kuendelea kutembea pamoja kama familia moja ya Mungu, Kanisa litaweza kuwafikia vijana na kuwajengea mazingira ya kukua katika imani, matumaini na upendo, huku likiwaandaa kuwa mashuhuda wa Injili katika ulimwengu mamboleo.

Vijana kamwe wasikate tamaa katika safari ya maisha yao
Vijana kamwe wasikate tamaa katika safari ya maisha yao

Rais Mpya wa AMECEA:Kabla ya kuanza kwa Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ya Kilele cha Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA), Makamu Mwenyekiti wa AMECEA Askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Nyeri nchini Kenya, Mhashamu Anthony Muheria, alitangaza rasmi kuchaguliwa kwa Mhashamu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, kuwa Rais mpya wa AMECEA na kusimikwa rasmi na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora pamoja na Askofu Charles Sampa Kasonde. Uchaguzi huo umefanyika wakati wa Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA uliowakutanisha Maaskofu kutoka nchi wanachama wa Shirikisho hilo kwa ajili ya kutafakari na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za kichungaji, uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ushiriki wa vijana pamoja na maendeleo fungamani ya binadamu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Askofu mkuu Nyaisonga anachukua nafasi hiyo ya uongozi huku AMECEA kutoka kwa mtangulizi wake Mhashamu Charles Sampa Kasonde ambaye amemaliza muda wake, hivyo akiendelea kutekeleza dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano kati ya Mabaraza ya Maaskofu, kukuza uinjilishaji na kujenga Kanisa linalotembea pamoja na watu wa Mungu, hasa vijana, kwa misingi ya umoja, matumaini, haki na utawala bora. Kuchaguliwa kwake kunadhihirisha imani kubwa ambayo Maaskofu wa AMECEA wameweka katika uongozi wake, wakiamini ataendeleza dira ya Shirikisho hilo katika kuimarisha: maisha na utume wa Kanisa na hivyo kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii ya Afrika Mashariki na Kati kwa mwanga na tunu za Kiinjili.

Watu wa Mungu waendelee kuwaombea Maaskofu wa AMECEA
Watu wa Mungu waendelee kuwaombea Maaskofu wa AMECEA

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, alizaliwa kunako mwaka 1966, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1996. Mwaka 2011 Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa na hatimaye kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma. Kunako mwaka 2014, akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Huko akaendeleza utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Tarehe 21 Desemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu Katoliki la Mbeya na kusimikwa rasmi tarehe 28 Aprili 2019, wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu. Kati ya Mwaka 2018 hadi mwaka 2024 alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Kaulimbiu iliyonogesha Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, “Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa” AMECEA kuanzia tarehe 19 hadi tarehe Dominika tarehe 26 Julai 2026, kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128 ni: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu unafanyikia kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Jijini Nairobi, nchini Kenya. Sifa na utukufu apewe Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, kwani ni katika mukadha huu, AMECEA inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 65 ya umoja, ushirika na mshikamano wa shughuli za kichungaji na huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni umoja ulioanzishwa kunako mwaka 1961 na unasimikwa na kufumbatwa katika tofauti mbalimbali kutoka katika nchi tisa wanachama ambazo ni: Eritrea, Ethiopia, Kenya, Malawi, Sudan Kongwe, Sudan ya Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia. Itakumbukwa kwamba, Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji.

Rais wa AMECEA 2026
26 Julai 2026, 16:18