Tafuta

kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre kwa Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama; Mapadre na Watawa! kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre kwa Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama; Mapadre na Watawa! 

Maadhimisho ya Jubilei Jimbo Katoliki Kahama, Tanzania

Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre kwa Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama, Mapadri wafuatao: Padri Diego Cano, Padri Rogatus Malulu, Padri Salvatore Guerrera, na Padri Paulo Maziku, sanjari na Sr. Emmaculate Emily na Sr. Maria. Mama Kanisa anamshukuru Mungu kwa kuwakirimia watumishi wake neema na baraka ya kuweza kuwatumikia watu wa Mungu kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita. Amina

Na Pascal Mwanache, - Kahama, Shinyanga, Tanzania

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema, upendo na ukarimu wake wa ajabu. Ni kipindi cha kuwashukuru wale wote walijiojisadaka bila ya kujibakiza, kiasi cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya huduma kwa Habari Njema ya Wokovu na leo hii wamekuwa hivi jinsi walivyo. Hawa ni viongozi wa Kanisa wanaobeba madonda ya watu wa Mungu; wakachangia kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: Kweli na uzima, ni Ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani na kwamba, mateso na mahangaiko ni kielelezo cha uaminifu wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi.

Kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre na Utawa, Jimbo la Kahama
Kilele cha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre na Utawa, Jimbo la Kahama

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora katika mahubiri yake kwenye kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre kwa Askofu Christopher Ndizeye Nkoronko wa Jimbo Katoliki la Kahama, Mapadri wafuatao: Padri Diego Cano, Padri Rogatus Malulu, Padri Salvatore Guerrera, na Padri Paulo Maziku, sanjari na Sr. Emmaculate Emily na Sr. Maria, amesema kwamba, Mama Kanisa anamshukuru Mungu kwa kuwakirimia watumishi wake neema na baraka ya kuweza kuwatumikia watu wa Mungu kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita. Ametoa mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuungana pamoja kuwashukuru wanajubilei waliosikia na hatimaye, wakaitikia wito na baadaye wakadumu katika wito wao kwa miaka 25. Wamelihudumia Taifa la Mungu kwa upendo, sadaka na majitoleo yao katika maeneo mbalimbali. Kumbe, Kanisa halina budi kumshukuru Mungu kwa yote haya. Huu ni mwaliko wa kuendelea kuwaombea bila kuchoka, kwani utume wao bado unaendelea, wasichoke wala kukata tamaa katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Waamini wawe tayari kumuunga mkono Askofu Christopher Ndizeye na wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kanisa katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi. Mwenyezi Mungu azidi kuwaimarisha katika maisha na utume wao wanapoendelea kulitumikia Kanisa na kwamba, yote haya yafanyike katika umoja, ushirika na mapendo.

Utoto Mtakatifu katika ubora wao
Utoto Mtakatifu katika ubora wao

Kwa upande wake, Askofu Eusebius Nzigilwa, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda amewataka wanajubilei wa miaka 25 ya Upadri na Utawa katika Jimbo Katoliki Kahama, Tanzania kuendelea kuwa sababu ya furaha na matumaini kwa waamini na watu wote kupitia maisha na huduma zao. Akitoa salamu za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika maadhimisho hayo ya jubilei yaliyofanyika katika Viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Karoli Lwanga Jimbo Katoliki Kahama, Askofu Nzigilwa amesema kuwa kupitia Jubilei hiyo, Kanisa linafurahi, mbingu zinashangilia kwa sababu ya wanaoadhimisha Jubilei za utume wao. “Tunawaomba mwendelee kuwa sababu ya furaha na matumaini mbinguni na duniani kwa njia ya maisha na huduma zenu. Furaha hii isiishie leo bali nendeni mkaguse maisha ya watu, mkarudishe furaha na matumaini kupitia maisha, huduma, faraja na sala mtakazowapatia” amesema Askofu Nzigilwa. Pia amepongeza umoja na mshikamano walioonesha wanajubilei hao ambapo miongoni mwao yumo Askofu Christopher Ndizeye wa Jimbo Katoliki Kahama, Mapadri: Padri Diego Cano, Padri Rogatus Malulu, Padri Salvatore Guerrera, na Padri Paulo Maziku, sanjari na Sr. Emmaculate Emily na Sr. Maria, akisema kuwa ushirikiano huo hauna budi uendelee daima. “Leo mmesherehekea kwa pamoja, askofu, mapadri na watawa. Huu ni mshikamano na ushirikiano unaopaswa kuendelezwa na kusifiwa. Mshikamano huu ndio chimbuko la hakika la huduma zilizokuwa bora katika Taifa la Mungu. Mkishikamana waamini wataneemeka kwa huduma zenu, mtawapeleka watu wengi katika ufalme wa Mbinguni unoasimikwa katika: Kweli, Uzima, Utakatifu, Neema, Haki, Amani na Mapendo na ninyi wenyewe mtapata tuzo. Endeleeni kushikamana si tu katika sherehe bali zaidi sana katika utumishi wa Taifa la Mungu” ameeleza Askofu Nzigilwa.

Askofu Eusebius Nzigilwa, Jimbo Katoliki la Mpanda
Askofu Eusebius Nzigilwa, Jimbo Katoliki la Mpanda

Aidha amesema kuwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawatambua, kuwaombea na kuwapongeza wanaoadhimisha jubilei zao za utume katika Kanisa ndani ya majimbo na mashirika mbalimbali wapo mapadri na watawa wengine wanaofanya jubilee zao. “Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania inatualika kumtolea Mungu shukrani, aliyewajalia ndugu zetu miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Wanajubiei tunamshukuru Mungu pamoja nanyi kwani miaka hii imekuwa na mchanganyiko wa vipindi vya furaha na magumu lakini neema na baraka za Mungu zilikuwa pamoja nanyi, zikiwaongoza na kuwapitisha kuyakabili magumu yote.” “Pongezi za dhati kwa wanajubilei kwa kudumu katika kuitikia na kuishi miito yao kitakatifu. Tunawashukuru na kuwapongeza kwa huduma na sadaka mlizotoa katika Taifa la Mungu, zimewaponya na kuwaongoza wengi katika wokovu na uzima wa milele” ameongeza.

Wanajubilei wakiwasha Mshumaa wa Jubilei
Wanajubilei wakiwasha Mshumaa wa Jubilei

Askofu Eusebius Nzigilwa, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ametumia pia fursa hiyo kutangaza Jubilei za Kibaraza ambazo ni Miaka 25 ya Upadri: kwa Askofu Christopher Ndizeye na Askofu Filbert Felician Mhasi wa Jimbo Katoliki Tunduru-Masasi, aliyepadrishwa tarehe 3 Julai 2001 kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Mahenge; tarehe 17 Februari 2019 akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi; Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu na 40 ya Upadri kwa Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS Jimbo Katoliki Moshi aliyepadrishwa tarehe 26 Juni 1986, akawekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 5 Agosti 2001 na tarehe 2 Desemba Papa Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi. Mwishoni ni Jubilei ya Miaka 25 ya Jimbo Katoliki la Mpanda lililoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 23 Oktoba 2000 na Hayati Askofu William Pascal Kikoti, akawa Askofu wake wa kwanza na hatimaye, kufariki dunia tarehe 28 Agosti 2012.

Kardinali Protase Rugambwa amewaalika waamini kuendelea kuwaombea
Kardinali Protase Rugambwa amewaalika waamini kuendelea kuwaombea

Wakati huo huo, Askofu Christopher Ndizeye wa Jimbo Katoliki Kahama ametoa shukrani kwa niaba ya wanajubilei wenzake akiomba sala zaidi kutoka kwa watu wote ili wazidi kumtumikia Mungu kwa uaminifu na uadilifu zaidi. "Mnavyotuona leo ni matokeo ya mchango wa wengi, tunatoa shukrani zetu kwa wote waliochangia tukawa hivi tulivyo, wakawa sababu ya furaha na mafanikio katika utume wetu. Shukrani kwenu ninyi nyote kwa kuwa pamoja nasi hapa Kahama mkisali na kutuombea, mkitokea mbali na karibu. Bado hatujafikia ukamilifu, tunahitaji kuombewa. Tunaomba sala na ushirikiano wenu, huenda tukahitaji ukaribu wenu kwa sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Mwendelee kuwa sababu ya furaha na amani katika maisha na utume wetu ili tuzidi kumtumikia Mungu na Taifa lake kwa ari na moyo mkuu” amesema Askofu Christopher Ndizeye wa Jimbo Katoliki Kahama.

Jubilei Miaka 25
13 Julai 2026, 17:04