Frt.Datius Prosper,OCD:"Bikira Maria tunamtazama kama mama na dada!"
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Siku kuu ya kiliturujia ya Mama Yetu wa Mlima Karmeli ilianzishwa ili kuadhimisha kutokewa kwa Mtakatifu Simon Stock mnamo tarehe 16 Julai 1251. Kitabu cha Kwanza cha Wafalme kinasimulia jinsi Nabii Eliya alivyokusanyika pamoja na baadhi ya watu kwenye Mlima Karmeli ili kutetea usafi wa imani, akiwashinda makuhani wa mungu Baali,(Wafalme 18). Kutokana na uzoefu huo, makundi ya watawa, yaliyoongozwa na Nabii Eliya, yalikaa hapo, yakifuata Utawala wa Mtakatifu Basil. Kuna ishara za hili katika karne ya 11, wakati Wapiganaji wa Msalaba walipofika mahali hapo. Karibu 1154, Mfalme wa Ufaransa Berthold, ambaye alikuwa amewasili Palestina na binamu yake Aimery wa Limoges, Patriaki wa Antiokia, alijificha mlimani, na ikaamuliwa kuwaunganisha tena watawa katika maisha ya kutafakari.
Watawa walijenga Kanisa dogo kati ya vyumba vyao vidogo , wakiliweka wakfu kwa Bikira Maria, na walichukua jina la Ndugu wa Mtakatifu Maria wa Mlima Karmeli. Kwa hivyo Karmeli ilipata vipengele viwili vyake vya kufafanua: marejeo yake kwa Nabii Eliya na uhusiano wake na Mwenyeheri Bikira Maria. Zaidi ya hayo, kulingana na mapokeo, Familia Takatifu ya Yesu Maria na Nazareth ilisimama hapo walipokuwa wakirudi kutoka Misri. Kila tarehe 16 Julai ya kila Mwaka, Mama Kanisa anaandimisha sikukuu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Vatican News, ilizungumza na mwanashirika Mkarmeli Datius Prosper ambaye anasisitiza mwongozo wao wa kumwinga Bikira Maria. Watawa wa Mlima Karmeli wamefanya hivyo na wanaendelea kufanya hivyo, lakini “kila Mkristo ameitwa kumtazama Maria ili kujifunza kutoka kwake, kujikabidhi kwa maombezi yake ili kulinda usafi wa imani dhidi ya kuabudu sanamu za Baali zilizopo ulimwenguni leo hii.”
Yafuatayo ni mahojiano na Ndugu Datius Prosper:
Mimi ninaitwa Frateli Datius Prosper ni ndugu wa shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Vikarieti ya Tanzania ambaye nipo hapa Roma, Italia, nikiwa nimehitimisha masomo yangu mwaka wa tatu masomo ya Taalimungu.
Bila shaka baada ya masomo utakuwa na majukumu mengine ya utume nchini Tanzania au unatarajia kubaki hapa?
Kwa sasa narejea Tanzania. Ratiba yangu yale yatakayofuata nitawasikiliza wakuu wangu wa shirika wananituma wapi na kipi kitakachoendelea.
Ukiwa hapa Roma, uzoefu wako katika masomo ni upi na vilevile hata katika ushirikiano na ndugu zako. Ni mambo gani ambayo yamekufurahisha ukiwa katika mji huu wanaouita mji wa milele?
Kwa kweli namshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ambayo wamenipatia, Shirika langu la Wakarmeli Tanzania, ni nafasi ambayo imenisaidia kuimarika kiimani. Uwepo hapa Roma baada ya kuona mambo mengi makubwa ya kiimani hasa imani yetu ya Kanisa Katoliki, ninaweza kusema kwamba safari yangu ya miaka mitatu hapa Roma imenisaidia kuimarika kiimani. Lakini pili imenisaidia kuweza kufahamiana na watu tofauti na kufahamu mambo mengi zaidi hasa kufahamu shirika kwa sababu hata makao yetu makuu ya Shirika yapo hapa Roma. Kwa hiyo nimepata nafasi pia ya kulifahamu shirika kwa undani zaidi, lakini kukua kiroho na kiimani katika shirika na katika Kanisa pia.
Shirika la Wakarmeli linajulikana ulimwenguni kote, hasa kwa ajili ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli na zaidi ninyi kama wakamermeli. Unaweza kutufafanulia kidogo kuhusiana na huyu Mama Maria wa Mlima Karmeli na ni kwa nini mmekuwa na roho hii ya Mama Maria wa Mlima Karmeli?
Kwa upekee sana sisi Wakarmeli, Bikira Maria tunamtazama kama mama na dada. Hii ni kutokana na utamaduni ambao upo katika shirika letu baada ya wale watawa wa mwanzo walipohama kutoka kule Israeli, Mlima Karmeli na kuja katika nchi za Ulaya, walipitia changamoto nyingi na mbalimbali. Na wakati huo aliyekuwa Mkuu wa Shirika alikuwa anaitwa Simon Stock. Kwa hiyo akiwa katika tafakari na sala, na kuwa na imani na kumwomba Mama Bikira Maria wa Mlima Karmeli, alimtokea na kama ishara ya ulinzi wake kwao alimpatia Skapulari. Kwa hiyo kwetu sisi Bikira Maria wa Mlima Karmeli tuna ibada hiyo. Na kwa Skapulari kama ulinzi kwa Shirika lakini kwa wale wote wanaovaa skapulari, kama yeye mwenyewe alivyosema “wote wanaovaa skapulari hii hawatauona moto wa milele maana yake watakombolewa.” Kwa hiyo tumekuwa na utamaduni huo na katika mavazi yetu ya shirika ipo skapulari tunayovaa lakini ili kuwashirikisha pia na waamini utajiri mkubwa huu wa kiroho nao wanaweza kupokea skapulari, na mara nyingi zinatolewa katika sherehe hii ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli tarehe 16 Julai katika Parokia na sehemu tunazofanya kazi.
Hii kweli na usione ajabu Mtakatifu Yohane Paulo wa II alikuwa na Skapulari hiyo hiyo ya Mtakatifu Maria wa Mlima Karmeli. Jambo jingine ambalo ni muhimu sana katika historia hii ya Mama Maria wa Karmeli?
Jambo jingine muhimu ambalo kwa sisi Wakarmeli tunaweza kusema ni utajiri ambao tuko nao. Tunasema ni Shirika la kwanza katika Kanisa kuwa chini ya jina na ulinzi wa Bikira Maria kwa sababu sisi Wakarmeli tunafahamika kama ndugu wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli, tofauti na mashirika mengi ambayo yana majina ya waanzilishi. Kwa hiyo ni utajiri na upekee ambao tunajivunia kuwa karibu na huyu mama, Mama Bikira Maria wa Mlima Karmeli.
Ni kwa jinsi gani utafanya hasa unaporudi mahali popote pale ambapo utatumwa, kuwafikia watu wengi waweze kumjua Mama Maria, kumsifu na kumshukuru na hasa kuwafundisha katika jamii na familia na isitoshe hata katika sehemu hizi ambazo unakuta Mama Maria anakuwa kama adui?
Kwanza ninaweza kusema kwamba, kwa sehemu ambazo Mungu atapenda kunituma itakavyokuwa baada ya kuhitimisha masomo yangu hapa Roma, kitu cha kwanza kwa sisi Wakarmeli kuwa, ibada ya skapulari sio kuivaa tu kama irizi au kitu kinginecho; lakini ni mwaliko wa kujipatanisha na kuwa karibu na Kristo! Kwa hiyo hilo ni la kwanza, na kwa sifa yetu sisi Wakarmeli tuna karama ya sala, ya tafakari ya kina. Kwa hiyo hilo nafikiri ni jukumu langu la kwanza kuwasaidia watu kuwa na ibada kwa Bikira Maria wa Mlima Karmeli na kuweza kuwasaidia kuelewa na kuivaa skapulari ili waweze kupata matunda ya kiroho yatokanayo na ibada hiyo. Lakini kingine ni kuendelea kuwasisitiza zaidi wawe na uwelewa, ni nafasi gani aliyo nayo Bikira Maria katika maisha yetu ya kiimani. Kama ulivyosema kwamba inapigwa vita nafikiri shida kubwa sana pia inaweza kuwa kwamba watu hawana uelewa wa kutosha kuhusu hilo. Kwa hiyo ninapohitimisha masomo yangu naamini pia katika kozi nilizofanya ipo kozi ambayo ilikuwa ni maalum kwa “Maria, ukombozi na nafasi ya Maria katika Kanisa.” Kwa njia hiyo, hilo nafikiri pia ni moja kati ya majukumu ambayo tunapewa au tunayo ya kuendelea kuitangaza injili.
Ni jambo jema kabisa la kuweza kumuenzi Mama Maria ambaye ni Mama wa Kanisa, mbali na kuwa Mama wa Mkombozi, lakini ni Mama wa Kanisa na asante kwa jukumu hili ambalo mnajiwekea kama mtihani wa kwenda kukabiliana nao. Sijui unalo jambo jingine lolote unapenda kuwaeleza wasikilizaji wetu hasa ambapo tumekwisha ingia mwezi wa Saba ambao ndani mwake tunaadhimisha sikukuu Bikira Maria wa Mlima Karmeli?
Kwanza napenda kuwakaribisha kuwa na ibada kwa mama yetu Bikira Maria wa Mlima Karmeli na kuwa na ibada ni sehemu mojawapo ya kuvaa skapulari. Skapulari hizi zinaweza kubarikiwa na kuvaliwa kwa hiyo kama mtu anaweza kuipata , mimi mwaliko wangu ni kwamba tuwe na ibada kwa Mama huyu ambaye aliwaahidi Wakarmeli ulinzi. Utajiri huu unashirikishwa pia kwetu sisi kama Wakristo tunapoishi katika ulimwenguni wa sasa wenye changamoto mbalimbali. Lakini la pili kwa sababu sasa, mimi nimehitimu masomo yangu hapa Roma na ninaporejea Tanzania, kiukweli ninajawa na moyo wa shukrani. Napenda kumshukuru Mungu kwa ulinzi wake, kwa neema zake alizonijalia kwa miaka hii mitatu. Lakini pia napenda kuwashukuru ndugu zangu Wakarmeli hasa hasa wakuu wa shirika walioona inafaa na kunipatia nafasi hii ya kuwa hapa kwa miaka mitatu. Nafahamu na ninatambua walivyojitolea na ni gharama kubwa sana. Lakini pia ninapenda kuwashukuru wafadhili wote wanaotusaidia katika masomo yetu na utume wetu kama Shirika na Kanisa la Tanzania. Na mwisho kabisa ni kuwashukuru ndugu, wazazi na marafiki wote waliokuwa pamoja nami katika safari hii ya miaka mitatu ambapo kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu imeweza kukamilika salama. Kwa hiyo moyo wangu wa shukrani kwa wale wote ambao wamekuwa wakisindikiza daima katika kuijongea altare ya Bwana.
Wimbo uliotungwa na Mtakatifu Simon Stock
Kwa Mtakatifu Simon Stock, ambaye alieneza ibada kwa Mama Yetu wa Mlima Karmeli na kumtungia wimbo mzuri, Flos Carmeli, Mama Yetu anahakikisha kwamba wale wanaokufa wakiwa wamevaa skapulari wangeachiliwa kutokana na maumivu ya Toharani.
Ua zuri la Karmeli, mzabibu unaochanua, utukufu wa mbinguni,wewe pekee ndiye Mama bikira. Mama mpole na asiye na lawama, uwahurumie watoto wako, nyota ya bahari. Mzizi wa Yese, unaozaa ua, Tujalie kubaki nawe milele. Yungi yungi iliyokua, miongoni mwa miiba mirefu, bado linda akili dhaifu na utoe msaada. Silaha kali ya wapiganaji, vita vinapamba moto: Weka scapulari kama ulinzi. Kwa kutokuwa na uhakika, utupe ushauri; Katika bahati mbaya, tuombe faraja kutoka mbinguni. Mama na Bi wa Karmeli yako, ishibishe mioyo yetu na furaha hiyo inayokufurahisha. Ee ufunguo na lango la Mbingu, tufikie ambapo umevikwa taji la utukufu. Amina.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.