Askofu Marco Mellino Katibu Mkuu Baraza la Kipapa la Sheria za Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kipapa la Sheria za Kanisa “Dicasterium de Legum Textibus” ni chombo cha Mahakama na ushauri ndani ya Vatican. Kazi yake kuu ni kufafanua sheria za Kanisa Katoliki, kuhakikisha utekelezaji wake sahihi, na kutoa msaada wa kisheria kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Mabaraza ya Maaskofu, Maaskofu mahalia, pamoja na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tarehe 30 Juni 2026 amemteuwa Askofu Marco Mellino kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Sheria za Kanisa hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Sheria za Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Askofu Marco Mellino alizaliwa tarehe 3 Agosti 1966 huko Canale, Jimbo Katoliki la Alba, Pompea Italia.
Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 29 Juni 1991 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Alba. Tarehe 27 Oktoba 2018 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Makardinali na hivyo kupandishwa hadhi na kuwa ni Askofu, hatimaye, akawekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 25 Desemba 20218. Tarehe 15 Oktoba 2020 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Makardinali. Tarehe 12 Aprili 2022 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Katibu wa Sekretarieti kuu ya Vatican mintarafu mabadiliko ya Sheria na kanuni kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Tarehe 7 Machi 2023 Baba Mtakatifu Francisko akamteuuwa kuwa tena Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Sheria za Kanisa. Tarehe 27 Novemba 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa kuwa Katibu mkuu mwambata wa Baraza la Sheria za Kanisa na hatimaye, tarehe 30 Juni 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Sheria.