Tume ya Ulinzi wa Watoto yapokea Sheria mpya,mamlaka mapya
Vatican News
Papa Leo XIV ameidhinisha Sheria mpya za Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto, akichukua nafasi ya zile zilizotangazwa mwaka 2015 na kuleta muundo na mamlaka ya Tume sambamba na Katiba ya Kitume ya Uinjilishaji. Sheria mpya zimeidhinishwa kwa majaribio kwa kipindi cha miaka mitatu na zilichapishwa Jumamosi, tarehe 13 Juni 2026. Maagizo yaliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin yanabainisha kuwa Baba Mtakatifu aliidhinisha maandishi yaliyorekebishwa wakati wa Mkutano mnamo tarehe 20 Mei 2026 na kuamuru yaanze kutumika mara moja.
Jukumu la Tume ya Kipapa katika kukuza uwajibikaji
Katika taarifa kwa vyombo vya habari inayoambatana na uchapishaji wa Sheria, Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto ilisema maandishi yaliyorekebishwa yanaimarisha jukumu lake katika kukuza desturi za ulinzi katika Kanisa zima na ni sehemu ya juhudi pana "kuhakikisha kwamba ulinzi unajumuishwa kikamilifu katika maisha na miundo ya Kanisa."
Askofu Mkuu Thibault Verny, Rais wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto, alisema Sheria hizo "zinaashiria hatua muhimu katika kuimarisha jukumu letu la pamoja la kuwalinda na kuwatunza walio hatarini zaidi." "Zinaakisi kuwasikiliza, waathiriwa/wanusura, wataalamu wa ulinzi, na uzoefu wa Makanisa mahalia na zinathibitisha tena kwamba ulinzi unabaki kuwa kipaumbele kikuu," aliendelea.
Vipengele vipya vya mamlaka ya Tume
Kulingana na Tume, Sheria zilizorekebishwa zinaimarisha mamlaka yake na ufanisi wa uendeshaji, zinaendelea kusisitiza mbinu zinazoelekezwa kwa waathiriwa na walionusurika. Sheria hizo pia zinafafanua uhusiano wa Tume na Mabaraza mengine ya Curia Romana, na zinaimarisha jukumu lake katika kukuza "uwajibikaji, uwazi, na desturi nzuri za ulinzi duniani kote." Tume inaripoti moja kwa moja kwa Papa na kumshauri kuhusu ulinzi wa watoto na watu walio katika mazingira magumu kutokana na unyanyasaji.
"Imeanzishwa pamoja na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya kanisa na kwa hivyo inashirikiana kwa karibu na Baraza la Kipapa katika kubadilishana taarifa, maendeleo ya mbinu za ulinzi, maandalizi ya Ripoti ya Mwaka na programu za uundaji," ilibainisha taarifa kwa vyombo vya habari. "Rais au Katibu ni wajumbe walioteuliwa wa Baraza la Kipapa na afisa mmoja au zaidi wa Baraza la Kipapa huteuliwa na Mkuu wa Baraza kama waangalizi katika Mikutano ya Wajumbe ya Tume." Tume haiongoi lakini husaidia kuongoza huduma ya Curia kwa Kanisa la ulimwengu kwa kukuza uwajibikaji wa ndani na uwezo wa Baraza mbalimbali la Kipapa la Vatican. Miongoni mwa maendeleo yaliyoangakisiwa na Tume ni kuendelea kwake kusaidia Makanisa mahalia katika kuunda mifumo ya ulinzi na kukuza mifumo thabiti na inayopatikana kwa urahisi ya kuripoti, pamoja na vituo vya kusikiliza ambavyo "vinawakaribisha, vinawasikiliza na kuwasindikiza waathiriwa/wanusurika", huku vikilinda usiri na data binafsi.
Ripoti za mwaka
Tume pia ilibainisha jukumu lake la kuandaa Ripoti ya Mwaka kuhusu Sera na Taratibu za Kanisa za Kulinda. Ripoti hiyo inatokana na michango kutoka kwa Mabaraza ya Kipapa na mashirika yaKanisa mahalia na inatafuta kuchora ramani ya "hadhi ya ulinzi katika Kanisa la kimataifa" kwa kutofautisha kati ya sera zilizothibitishwa, desturi zilizotangazwa, taarifa zilizopokelewa, masuala ya kimfumo, na mapendekezo. Papa Leo XIV amethibitisha mara kwa mara kwamba ulinzi wa watoto na watu walio katika mazingira magumu ni jukumu la msingi la Kanisa. Tume ilisema Sheria zilizorekebishwa zinathibitisha tena ahadi hii na zinaunga mkono dhamira yake ya kuambatana na Makanisa mahalia katika kuimarisha juhudi za ulinzi kote ulimwenguni.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here.