Tafakari Dominika ya 12 Mwaka A wa Kanisa: Katika Dhambi Mwanadamu Anapotea
Na Padre Octavian O. Hinju, CP Jordana University College Morogoro, Tanzania.
Kanisa linafundisha kwamba, dhambi ni kosa dhidi ya akili, ukweli na dhamiri sahihi. Ni kushindwa kuwa na mapendo kweli kwa Mungu na jirani kwa sababu ya mapendo potofu ya mambo fulani. Dhambi, hujeruhi tabia ya mtu na kuharibu mshakamano wa kibinadamu. Dhambi inafafanuliwa kama ni tamko, tendo au tamaa kinyume cha sheria ya milele (Rej. KKK, 1849). Tena inasemwa hivi, dhambi ni kumkosea Mungu. Maandiko Matakatifu yanasisitiza tunaposoma hivi “nimekutenda dhambi wewe peke yako na kufanya maovu mbele za macho yako (Zab. 51:4). (Rej. KKK, 1850). Dhambi huleta giza na hofu moyoni, hivyo kuwa chanzo cha anguko na kuangamia kwa roho ya mwanadamu. Kifo na mauaji! Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 20 Juni 2026 amefanya hija ya kichungaji kwa kutembelea Mkoa wa Lombardia, Kaskazini mwa Italia katika miji miwili ya Pavia na Sant’Angelo Lodigiano; miji ambayo imeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Leo XIV. Mtakatifu Augustino ni Muasisi wa Shirika la Waagostiniani: “The Order of St. Augustine, OSA.” Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Baba Mtakatifu Leo XIV alitia nia ya kutembelea maeneo ya maisha na utume wa Mtakatifu Augustino. Mji wa Pavia unahifadhi masalia ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa ambaye katika mafundisho yake aliutazama unyenyekevu kama msingi wa imani ya Kikristo. Kwa tajiriba ya maisha na utume wake, Mtakatifu Augustino hatimaye alitambua kwamba ni mtu tu aliye na unyekekevu ndiye anaweza kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni unyenyekevu wenyewe maana “hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu.” (Flp. 2:6-7.)
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 12 ya mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo katika Dominika hii umejikita katika kutukumbusha kuhusu matokeo ya dhambi katika roho na maisha ya mwanadamu. Ni kwa dhambi ndipo kifo na mauti viliingia ulimwenguni na kuwa kikwazo cha mwanadamu (Mwz. 3:1-24). Kwa kulitambua hilo, kanisa siku zote linatoa mwaliko wa kuielekea sakramenti ya kitubio na upatanisho ili kulinda ndani mwenu hadhi na wito wa utakatifu na maisha adilifu. Kadhalika ni kwa njia ya kifo cha Yesu msalabani tunajipatia uzima wa milele, “kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu (Rum. 6:23), Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu, aliumizwa kwa sababu ya maovu yetu. Kwa kuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai; kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote tumepotea kama kondoo, kila mmoja wetu ameelekea njia yake. Lakini Mwenyezi-Mungu alimtwika adhabu, ambayo sisi wenyewe tuliistahili (Is. 53:5-6). Kumbe huruma ya Kristo ndiyo hasa hupelekea ushindi dhidi ya dhambi na maotea ya shetani. Kanisa linaendelea kufundisha kwamba, ‘dhambi hujiweka dhidi ya mapendo ya Mungu kwa ajili ya kuigeuza mioyo yetu mbali nao. Kama ilivyo kuwa dhambi ya kwanza, ni ukaidi, ni kumwasi Mungu kwa kutaka kuwa saw ana miungu kwa kujua na kuamua mem ana mabaya. Kwa hivi dhambi ni kujipenda mwenyewe mpaka kumdharau Mungu. Kwa sababu ya kiburi cha kujitukuza, dhambi ni kinyume kabisa na utii wa Yesu unaoleta wokovu (Rej. KKK, 1850.)
Kanisa linafundisha kwamba, dhambi ni kosa dhidi ya akili, ukweli na dhamiri nyofu. Ni kushindwa kuwa na mapendo kweli kwa Mungu na Jirani kwa sababu ya mapendo potofu ya mambo Fulani. Dhambi, hujeruhi tabia ya mtu na kuharibu mshakamano wa kibinadamu. Dhambi inafafanuliwa kama ni tamko, tendo au tamaa kinyume cha sheria ya milele (Rej. KKK, 1849). Tena inasemwa hivi, dhambi ni kumkosea Mungu. Maandiko Matakatifu yanasisitiza tunaposoma hivi “nimekutenda dhambi wewe peke yako na kufanya maovu mbele za macho yako (Zab. 51:4). (Rej. KKK, 1850). Dhambi huleta giza na hofu moyoni, hivyo kuwa chanzo cha anguko na kuangamia kwa roho ya mwanadamu. Dhambi hupofusha roho kiasi cha kutoona utukufu wa Mwenyezi Mungu, neema na baraka ndani ya mwanadamu. Dhambi ni matokeo ya mlundikano wa mizizi ya dhambi ambayo kwa kuipalilia kwa matendo ya kibinaadamu yasiyofaa huzaa dhambi. Dhambi ni matokeo ya kile kibaya tunacho kifanya kwa kukirudia rudia. Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kumuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua. “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” (Flp 4:8.)
Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Yeremia (Yer 20:10-13). Somo hili linatupa masimulizi kutoka katika kinywa cha Yeremia mwenyewe. Nabii Yeremia anatabiri namna itakavyo kuwa adhabu atakayoitoa Bwana kwa watu wa Yerusalemu. Adhabu hii ni matokeo ya dhambi yao, yaani kumdhania Yeremia kuwa ni mtu mchongezi na mchochezi, hivyo watu wa mji huo walimtishia kumshtaki na kumuua. Dhambi katika maisha ya mwanadamu huleta wivu na visasi kiasi cha kuwachukia wanaoona madhaifu yetu na kuchukua jukumu la kutusahihisha. Hawa ndio wale waobebeshwa misalaba mizigo kwa gharama ya ukweli ambao ni Kristu mwenyewe kama ilivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji na Herodia mke wa Herodi. Lakini hata Kristu mwenyewe alishtakiwa na kuhukumiwa kwa makosa ya uongo na uzushi hata kufa kifo cha aibu msalabani. Tabia hii imeshamiri na kushika kasi sana katika jamii zetu kiasi cha kuzuia uhuru wa Habari na haki ya kutoa maoni na Mawazo mbadala hupingwa na kufungiwa kabisa. Kumbe upendo wa kweli uambatane na kuambiana ukweli ili kuiponya jamii yetu inazongwa kwa kiasi kikubwa na utamaduni mpya wa uongo na uzushi, ‘tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru (Yoh. 8:32). Tunashuhudia kote barani Afrika na ulimwengu kwa ujumla namna ambavyo viongozi wa dini na siasa wenye kupenda kukemea maovu na kusema ukweli wakidhulumiwa hata kupelekea kifo kama ilivyotokea hivi karibuni kwa Askofu Osório Citora, IMC, Askofu wa jimbo Katoliki la Quelimane ambaye aliuawa tarehe 6 Juni 2026 na watu waliovamia makazi yake na kumuua kwa kumpiga risasi kifuani huko nchini Msumbiji. Hata katika hali ya namna hii watu wa Mungu wasichoke wala kuogopa kukemea mabaya na kuusema ukweli kwani Mungu bado ndiye ngao na kimbilio.
Kama wajumbe wa Mungu wasimame kidete katika kusambaza na kueneza neno la Mungu pasi na hofu wala mashaka yoyote. Ni mwito na mwaliko wa kuchota nguvu na uimara kutoka katika msalaba wa Yesu mwenyewe. Ifahamike kwamba kazi ya kuwa mjumbe wa Mungu kwa watu wake, sharti ijengwe katika uadilifu wa maisha ya sala bila kupindisha utume wa kinabii ili kulinda na kutetea maslahi ya mwanadamu; haya yote kwa Pamoja humletea mtu maadui katika maisha yake. Katika somo la Kwanza Nabii Yeremia mwenyewe anasema amesikia watu wanamshutumu na wanapanga mipango wamuangamize. Mbele ya tishio hili kubwa, Yeremia anafanya nini? Yeremia anaweka matumaini yake kwa Mungu. Kadiri hofu inavyozidi kuwa kubwa, imani na matumaini kwa Mungu vinapaswa kuongezeka. Yeremia hakati tamaa, harudi nyuma wala hasemi “sifanyi tena kazi ya kuwa nabii”. Anachosema ni kuwa “Bwana yu pamoja nami”. Neno hili analolisema Yeremia kuwa “Bwana yu pamoja nami” ni utimilifu wa sala. Nabii Yeremia anamwomba Mungu asimuache peke yake katika hofu inayomkabili na katika hatari inayomkabili. Ni sala ambayo inakuwa ni kana kwamba imekwisha sikilizwa kwa maana anayeisali ana uhakika kuwa itasikilizwa. Ni kwa sababu hii Yeremia anaongeza katika sala hiyo mategemeo ya kibinadamu katika lugha ambayo ni ya kibinadamu. Nasi tusiache kusali tupitapo katika magumu na changamoto za maisha.
Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Paulo Mtume kwa Warumi (Rum 5:12-15). Somo hili linapanua wigo wa tafakari yetu juu ya hofu katika maisha ya mwanadamu. Hofu isipotawaliwa wakati mwingine hutupelekea Kutenda dhambi. Somo letu la pili ndilo linalokuja kutuonesha kuwa mwanadamu hakabiliwi na hofu za kimwili tu au hofu za nje zinazogusa maisha yake ya kawaida, bali maisha ya kila siku. Mwanadamu anakabiliwa pia na hofu za kiroho ambazo chimbuko lake ni dhambi, yaani kukokuwa na mahusiano mazuri na Mungu. Mtume Paulo analionesha hilo kwa kueleza madhara ya dhambi ya Adamu na matokeo yake kwa binadamu wote na hapo hapo anaonesha karama ya upatanisho aliouleta Kristo na matokeo ya upatanisho huo kwa binadamu wote. Ni somo linalokuja kutuonesha kuwa dhambi ni chanzo kikubwa cha hofu na kutokuwa na amani ya roho maishani. Upatanisho na Mwenyezi Mungu ni njia ya kuondokana na hofu hizo na ni njia ya kukaribisha amani ya roho maishani. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika mafundisho yake kuhusu Sakramenti ya Upatanisho alipata kusisitiza kwa kuonesha kuwa “kupokea Sakramenti ya upatanisho ni hatua muhimu sana kwa anayetaka kuanza maisha mapya au kupiga hatua katika maisha yake.” Mtume Paulo anatukumbusha kwamba kwa njia ya Adamu wa kwanza ndipo dhambi iliingia duniani na kumtenga mtu na Mungu aliye muumba wake hivyo mauti ikawa ni adhabu yake, ‘Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu (Rum. 6:23). Kwa neema ya Mungu, tunakumbushwa na somo hili kuwa kwa njia ya Adamu wa pili yaani Bwana wetu Yesu Kristu, tumeletewa neema nyingi zinazo shinda dhambi na adhabu yake. Nasi basi kwa mfano na maisha adilifu ya kisakramenti, tujitahidi kutopoteza uhusiano wetu na Mungu katika dhambi. Tuipokee sakramenti ya kitubio na upatanisho kila wakati ili kuponya majeraha yatokanayo na dhambi.
Injili ni kama ilivyo andikwa na Mathayo (Mt. 10: 26-33). “Non abiate paura” yaani “msiogope” ni maneno ya Kiitaliano yanayo fungua tafakari yetu katika Injili ya siku ya Dominika ya 12 ya Mwaka A wa Kanisa. Mwaliko wetu ni “msiogope wauuao mwili wasiweze kuiua na roho” ni mananeo yenye kubeba tumaini na faraja kwani yanatoka kinywani mwa Kristu mwenyewe. Mitume wanatiwa moyo kuwa wasiogope kwani watahubiri kwa watu wote yale waliyoyasikia faraghani na hadharani, yaani Habari njema ya wokovu. Kristu aliye Bwana na Mwalimu wao, anawasisitiza wasiogope kwa sababu anawajulisha wazi ugumu unao wakabili. Wajiandae kwa maana watapambana na matatizo mengi katika kazi hiyo njema wanayo iendea. Kumbe hata sisi katika shauku yetu ya kumtangaza Kristu katika nyakati na mahali petu, tutapingwa vikali na kusukumwa pembeni. Tusikate tamaa wala kuogopa kwani yeye aliye tuita na kututeua kuiendea kazi hiyo njema ni mwema, mwaminifu na mwenye nguvu na uweza wote. Katika magumu ya kitume na Imani, zipo nyakati tunajishauri kutoendelea na kuacha kabisa kile tulicho itiwa. Fundisho la Yesu ya kuwa tusiogope ni kiashiria kwetu pia kumtazama Yeye ili atupe nguvu na mwanzo mpya. Tunasali leo kuombea neema ya kudumu waaminifu katika wito na Imani mpaka kufa ili siku moja tuweze kushiriki Pamoja na Kristu raha zote za ufalme wa Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.