Tafuta

Kanisa linalosafiri duniani, kwa tabia yake ni la kimisionari, sababu limepata asili yake katika kutumwa kwa Mungu Mwana na kutumwa kwa Roho Mtakatifu, kufuatana na azimio la Mungu Baba. Kanisa linalosafiri duniani, kwa tabia yake ni la kimisionari, sababu limepata asili yake katika kutumwa kwa Mungu Mwana na kutumwa kwa Roho Mtakatifu, kufuatana na azimio la Mungu Baba.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 11 ya Mwaka A wa Kanisa: Wito na Utakatifu wa Maisha

Kanisa linaendelea kutafakari kuhusu: Ukuu na utakatifu wa Fumbo la wito, maisha na utume wa Kipadre na Maisha ya kuwekwa wakfu, ili kuweka bayana, thamani yake isiyoweza kupimika kwa mizani ya kibinadamu. Lengo ni: kulinda, kuhifadhi na kudumisha usafi na utakatifu wake kama wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Mapadre na watawa watambue kwamba, Kanisa linawahimiza kuwa kweli ni watumishi waaminifu, watakaomuakisi Kristo fukara, mtii na mseja.

Na Padre Octavian O. Hinju, CP. - Jordan University College, Morogoro.

Kiini cha masomo ya Dominika ya Kumi na Moja ya Kipindi cha Mwaka A wa kanisa ni ukumbusho juu ya wito wetu wa kuwa watumishi, wajumbe na mashuhuda wa Neno la Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anasema kwamba, Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha kutoka katika sehemu mbalimbali za Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Masomo yanatilia mkazo kwamba mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache, na Mungu ametuteua kuwa taifa lake teule ili kueneza Injili kwa watu wengine, “Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya Masihi wangu milele” (1 Sam. 2:35).

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa linalosafiri duniani, kwa tabia yake ni la kimisionari, sababu limepata asili yake katika kutumwa kwa Mungu Mwana na kutumwa kwa Roho Mtakatifu, kufuatana na azimio la Mungu Baba, chemchemi ya huruma na upendo, ili kuwatangazia watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Kristo Yesu alilisimika Kanisa lake kama Sakramenti ya wokovu na hivyo kuwatuma Mitume wake wakaihubiri Injili kwa watu wote wa Mataifa, kwa Sakramenti na vyombo vingine vya neema, lipate kuwaongoza watu kufikia imani, uhuru na amani ya Kristo Yesu, na hivyo liwaandalie njia nyeupe na thabiti ifikishayo kwenye kushiriki kikamilifu Fumbo la Kristo Yesu. Rej. AG. 1- 9. Tena waamini wanakumbushwa na Kristo Yesu kwamba, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.” Lk 10:2. Kanisa linaendelea kujitahidi kutafakari kwa kina na mapana kuhusu: Ukuu na utakatifu wa Fumbo la wito, maisha na utume wa Kipadre na Maisha ya kuwekwa wakfu, ili kuweka bayana, thamani yake isiyoweza kupimika kwa mizani ya kibinadamu. Lengo ni: kulinda, kuhifadhi na kudumisha usafi na utakatifu wake kama wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Jambo la msingi kwa Mapadre na watawa ni kutambua kwamba, Kanisa linawahimiza kuwa kweli ni watumishi waaminifu, watakaomuakisi Kristo fukara, Kristo mtii na Kristo msafi katika useja.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu
Waamini wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu   (@Vatican Media)

Msingi na ujumbe wa masomo ya dominika ya kumi na moja ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa ni wito wa kuishi tunu na zawadi ya utakatifu kwa kila mbatizwa. Kiini cha masomo ya Dominika hii ya leo ni ukumbusho juu ya wito wetu wa kuwa watumishi, wajumbe na mashuhuda wa Neno la Mungu. Masomo yanatilia mkazo kwamba mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache, na Mungu ametuteua kuwa taifa lake teule ili kueneza Injili kwa watu wengine, “Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele” (1 Sam. 2:35). Ukweli huu unadhihirishwa kwa tendo na mfano wa kuitwa na kuteuliwa kwa wana wa Israeli kuwa taifa teule. Vilevile katika kuitwa, kuchaguliwa na kutumwa kwa Mitume kumi na wawili “Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu” (Mt. 4:19); na wito wa Jumuiya ya kikristo kuishi kadiri ya mpango wa Mungu “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao” (Mt. 18:20). Licha ya kuwa wito huu ni wa kila mtu mmoja mmoja “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi” (Yoh. 15:16), lakini unapaswa kujidhihirisha katika maisha ya kifamilia, kijumuiya na Kanisa kwa ujumla wake ili kumpa kila mmoja nafasi ya kuiishi amri ya mapendo kwa kutenda matendo ya huruma kwa wale anaoishi nao kwa msaaada wa neema za Mungu “Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika” (Mdo. 4:32). Hii ni kwa sababu binadamu ni kiumbe ambaye hajakamilika, ana mapungufu na bila Mungu hawezi chochote, “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote” (Yoh. 15:5).

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Kristo Yesu
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha Kutoka (Kut.19:2-6). Somo hili linaangazia huruma na upendo wa Mungu kwa wana wa Israeli. Tunu hizi mbili yaani huruma na upendo zinaoneshwa wazi na Mungu anaye mweleza Mtumishi wake Musa kuhusu hali ya Agano analotaka kulifanya na waisraeli. Agano hili litamfanya Israeli awe taifa lake pekee, takatifu la Mungu kati ya mataifa yote.  Tena kwa njia ya Agano, Israeli atafanywa kuwa ukoo wa makuhani wa Bwana wajiwekao wakfu kwa ibada ya torati “Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli” (Yoh 17:19). Hakika kwa tendo hili, yaani Agano kwa maisha yote waisraeli watawadai ibada ya uaminifu na uchaji kwa Mungu, kwani kulishika agano ni mafanikio na kulipuuza ni dhambi na laana kwao na kwa vizazi vyao. Itakumbukwa kuwa Agano katika lugha ya kisheria ni mkataba baina ya pande mbili zinazo Fanya makubaliano au mapatano yao yawe rasmi na yenye kumfunga kila mmoja na kuhitaji utekelezaji. Kumbe kwa agano Mungu anakuwa Baba kwao wana wa Israeli na wana wa Israeli wanakuwa wana wateule wa Mungu sawasawa na wimbo wetu wa Katikati leo unao imba ukisema “Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake” (Zab. 100:3). Agano kwa Israeli lilikuwa ni ukumbusho kwamba Mungu ndiye kwao ngao, kinga na kimbilio; daima wamtumainie Yeye naye yuko tayari kuwasikiliza endapo watamgeukia wakilia na kuomboleza kama anavyo Sali Mzaburi “Ee BWANA, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu. Uliposema, “Nitafuteni uso wangu,” Moyo wangu umekuambia, BWANA, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako, Usimkatalie mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu” (Zab. 27:7,9.)

Mkazo ni ushuhuda wa Injili na utakatifu wa maisha
Mkazo ni ushuhuda wa Injili na utakatifu wa maisha   (@Vatican Media)

Agano kadhalika lilimaanisha uaminifu na utimilifu wa ahadi za Mungu. Lilikuwa ni ukumbusho wa matendo makuu ya Mungu kwa watu wake hasa ukombozi wao kutoka utumwani Misri chini ya Farao na jeshi lake. Mungu anawaambiwa kwamba ni kwa kutii na kulishika Agano watakuwa tunu yenye thamani kubwa kwake. Masimulizi ya kihistoria kutoka katika taifa la Misri inasema hivi, waisraeli walimwabudu mungu aliyeitwa horus. Huyu ni ndege ambaye ishara ya kuonekana kwake ilikuwa ni kwa mfano wa mwewe. Huyu ni ndege aliyeashiria nguvu na mamlaka. Kumbe Mungu anatumia lugha ya picha kuashiria nguvu na uwezo wake wa kuokoa. Ya kwamba kama mwewe anyakuavyo kifaranga cha kuku kwa nguvu ya mbawa zake kadhalika Mungu anao uwezo wote wa kuokoa. Sisi nasi, kwa ubatizo na maisha ya kisakramenti tumefanya agano na Mwenyezi Mungu basi na tuliishi agano hilo kiaminifu ili kujipatia wokovu; kwani huku ni kuzaliwa kwa jumuiya mpya yenye muungano na Mungu wa kweli, jumuiya inayozaliwa inategemea utii na usikivu wao kwa sauti ya Mungu na uaminifu wao kwa Agano lake naye Mungu anachukua jukumu la kuwalinda na kuwakinga na kila baya litakalojitokeza mbele yao maana wao sasa watakuwa taifa teule la Mungu. Hivyo Mungu mwenyewe atawafanya kuwa watakatifu. Kulishika agano ndilo jambo lenye kufurahisha nafsi ya mtu na Mungu “Sheria ya BWANA ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa BWANA ni amini, Humtia mjinga hekima. Maagizo ya BWANA ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya BWANA ni safi, Huyatia macho nuru” (Zab. 19:7-9).  Kama ambavyo kwa kulitii agano wana wa Israeli wangefanikiwa na kuikalia nchi sisi nasi tusali kuomba Hekima ya kushika amri za Mungu ili tuweze kuirithi nchi.

Waamini watumie karama zao kwa ajili ya ujenzi wa Ufame wa Mungu
Waamini watumie karama zao kwa ajili ya ujenzi wa Ufame wa Mungu   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la Waraka Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 5:6-11). Huu ni Waraka mrefu kuliko nyaraka zote alizo ziandika Mtume Paulo. Itakumbukwa kuwa Paulo hakupata nafasi ya kuhubiri katika jiji la Roma. Akiwaka shauku ya kufika kwao na kuhubiri Neno la Mungu aliamua kuwaandikia na kuituma barua hii ili isomwe kabla yeye hajafika. Kinyume na matarajio yake Paulo alikamatwa na aliuawa kwa kukatwa Kichwa chini ya utawala na amri ya Mtawala Nero yapata mwaka 64 AD huko jijini Roma na hivyo akafa kama shuhuda na shujaa wa imani. Katika somo hili Mtume Paulo anatufundisha kuwa utukufu na heri yetu ya milele ni hakika, kwa vile Mungu ametukomboa kwa damu ya Mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo tulipokuwa bado wenye dhambi, “Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake aliyotukirimia bila kipimo” (Waef. 1:7). Kama msaada wa Mungu wa kututakia ukombozi kutoka dhambi ni mkubwa hivyo, basi msaada huo utakuwa mkubwa zaidi siku ya hukumu ya mwisho kwa wale wanaoweka tumaini lao kwake. Huu ni mwaliko wa kujiandaa na maisha ya umilele mbinguni. Paulo Mtume anaonyesha pendo la Mungu kwetu sisi linalo bubujika kwa kifo cha Yesu msalabani. Hili ni tumaini linalo okoa kama anavyo tafakari hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika araka wake wa Kitume Spe Salvi anasema kwamba tumepatanishwa na Mungu kwa njia ya Kristo. Basi tukubali daima kuendelea kupatanishwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo hasa katika Sakramenti ya Kitubio kila tunapojitenga kwa dhambi zetu. Tuikimbilie daima Sakramenti hii ili tusuluhishwe na kupatanishwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo anayefanya kazi hii katika nafsi za Mapadre kama anavyo sema nasi mwandishi wa Waraka kwa Waebrania kwamba “basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji (Waebr. 4:16.)

Uinjilishahi uanzie nyumbani, Kanisa dogo
Uinjilishahi uanzie nyumbani, Kanisa dogo   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyo andikwa na Mwinjili Mathayo (Mt. 9:36-10:8). Sehemu hii ya Injili inaleta kwetu mambo makuu matatu ya msingi. Kwanza ni huruma ya Mungu. Sehemu hii inatuonesha jinsi huruma ya Mungu ilivyo kuu kwa watu wake aliyoidhihirisha kwa njia ya Yesu Kristo mwanae wa pekee. Kwa huruma yake Mungu hakutuacha hata tulipokuwa bado wenye dhambi, bali ametukomboa kwa damu ya Mwanae. Pili ni Wito na Utume wetu; ya kwamba tumechaguliwa na kutengwa na Mungu ili tuwe mashahidi wake na kuombea miito mingine katika Kanisa. Tatu na mwisho ni ukweli kwamba Mavuno ni mengi. Somo la Injili linatukumbusha kuwa ulimwengu unahitaji Neno la Mungu, na Yesu anatuita tuwe watendakazi ili kueneza upendo na wokovu. Katika sehemu ya Injili hii, tunamwona Yesu anayejali na kufikiri kuhusu wengine, “na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji” (Mt. 9:36). Kadhalika anatoa suluhisho kwa changamoto hiyo anaposema, “Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini wafanya kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, atume wafanya kazi katika mavuno yake, (Mt. 9:37-38). Leo tuna sali kuombea miito mbalimbali na kumsihi Mungu Baba na Bwana wa historia ili aendelee kuita na kulijalia Kanisa miito mitakatifu itakayo walisha kondoo wake kwa wema, uadili, moyo mkuu na uaminifu. Tumwige Kristo na tumwombe atujalie neema ya kuona mahitaji ya wengine na kuyatimiza kwa ari na upendo mkuu. Tusiwe watazamaji tu pale wengine wanapo zongwa zongwa na matatizo bali tuwe sehemu ya faraja zao kwa kufanya hivyo tutaendelea kuziishi tunu za Injili “nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea” (Mt. 25:36). Upendo na ukarimu kama fadhila za kikristu. Tumsifu Yesu Kristo.

Liturujia D 11 Mwaka A
13 Juni 2026, 11:48