Tafuta

 Maria Montserrat Alvarado Mwenyekiti Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii, ana umri wa miaka 40 na alizaliwa huko Mexico City. Maria Montserrat Alvarado Mwenyekiti Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii, ana umri wa miaka 40 na alizaliwa huko Mexico City. 

Maria Montserrat Alvarado, Mwenyekiti Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii

Papa Leo XIV amemteuwa Maria Montserrat Alvarado kuwa ni Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii na hivyo kuchukua nafasi ya Dr. Paolo Ruffini anayemaliza muda wake, kwa kutimiza umri wa miaka 70, hapo mwezi Oktoba, 2026 tayari kuendeleza mageuzi yaliyoanzishwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko mintarafu vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican na kwamba, ataanza utume wake, tarehe Mosi Nov. 2026.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV amemteuwa Maria Montserrat Alvarado aliyezaliwa huko Mexico City, mwenye umri wa miaka 40 kuwa ni Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii na hivyo kuchukua nafasi ya Dr. Paolo Ruffini anayemaliza muda wake, kwa kutimiza umri wa miaka 70, hapo mwezi Oktoba, 2026 tayari kuendeleza mageuzi yaliyoanzishwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko mintarafu vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican na kwamba, ataanza utume wake, tarehe Mosi Novemba 2026. Hadi kuteuliwa kwake Maria Montserrat Alvarado alikuwa ni Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Utangazaji la “Eternal Word Televishen Network, EWTN” kutoka nchini Marekani. Hili ni Shirika ambalo limejikita sana katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya: Luninga, radio, magazeti pamoja na mitandao ya kijamii katika mifumo ya kidijitali.

Dr. Paolo Ruffini anayemaliza muda wake kama Mwenyekiti wa Baraza
Dr. Paolo Ruffini anayemaliza muda wake kama Mwenyekiti wa Baraza

Maria Montserrat Alvarado anakuwa ni mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuongoza Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii na Mlei wa Pili kuongoza Baraza hili baada ya Dr. Paolo Ruffini. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Juni 2015 alianzisha mchakato wa mageuzi kwa vyombo vinavyomilikiwa na kuongozwa na Vatican; kwa kuongezewa na idara ya Taalimungu na Shughuli za Kichungaji mintarafu sekta ya mawasiliano ndani ya Kanisa. Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii Maria Montserrat Alvarado baada ya uteuzi huu anapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Baba Mtakatifu Leo XIV na kwamba, ametia nia ya kumhudumia Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake. Anamshukuru Dr. Paolo Ruffini kwa uongozi wake madhubuti tangu alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2018, kama Mwamini Mlei wa kwanza kuongoza Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii. Anasema, ataendeleza urafiki kati yake na Dr. Paolo Ruffini ili kuendeleza mchakato wa mawasiliano kwa ajili ya Kanisa, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Dr. Paolo Ruffini aliteuliwa na Papa Francisko Mwaka 2018
Dr. Paolo Ruffini aliteuliwa na Papa Francisko Mwaka 2018   (Vatican Media)

Dr. Paolo Ruffini katika barua yake kwa wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii ambalo lina vinasaba vya mawasiliano, kuwa macho na makini daima, kwa kusoma alama za nyakati katika muktadha wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Huu si muda wa kusimama na kuanza kuangalia, bali ni fursa ya kusonga mbele na hivyo kuendelea kuwa ni chombo kinachodumisha umoja na ushirika. Anasema, atamrithisha ushuhuda wake Mwenyekiti Mpya wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii. Anawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wote kwa safari waliyoifanya kwa pamoja ili kuendelea kulifanya Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii kutekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa, katika roho ya umoja, ukweli na uwazi. Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji la “Eternal Word Televishen Network, EWTN” kutoka nchini Marekani wanamtakia heri na baraka na kumhakikishia sala zao Maria Montserrat Alvarado apoanza maisha na utume wake kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii na huduma kwa ajili ya Baba Mtakatifu Leo XIV anapoendelea na maisha pamoja na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa Leo XIV Uteuzi

 

02 Juni 2026, 16:31