Tafuta

2026.06.15:Misa wakati wa Mkutano wa ufunguzi wa Mkutano wa Mpango wa Mfuko wa Conrad N.Hilton. 2026.06.15:Misa wakati wa Mkutano wa ufunguzi wa Mkutano wa Mpango wa Mfuko wa Conrad N.Hilton. 

Ask.Mkuu Ruwa'ichi atoa Wito kwa watawa kudumisha uaminifu,utume na karama za shirika!

Mkutano ulioandaliwa na Mfuko wa Hilton na Chama cha Watawa Wakatoliki barani Afrika,ulifanyika Dar es Salaam,Tanzania ukiwaleta pamoja watawa wa mashirika mbalimbali wa Mpango wa Mfuko huo kutoka duniani.Askofu Mkuu Ruwa'ichi,O.F.M.Cap.,aliongoza Ibada ya Misa Takatifu Juni 11,ambapo katika mahubiri aligusia sala,tafakari, ushirika na majadiliano juu ya utume wao wa pamoja katika huduma ya Kanisa na jamii.Watoa mada wengi walikuwa ni wakuu wa Mabaraza ya Kipapa.

Na Christine Masivo,Cps – Vatican.

Yesu aliwaagiza wanafunzi wake kutangaza kwamba “Ufalme wa Mungu umekaribia,” na wito huu si kwa wanafunzi wa kwanza pekee bali kwa kila Mkristo aliyebatizwa. Watawa zaidi ya utambulisho wao kama Wakristo, wamepokea wito maalum wa maisha ya wakfu, kila mmoja ndani ya Shirika lake, wakiwa wamebarikiwa na karama zao za kipekee, wanapaswa  kujitahidi kubaki waaminifu kwa wito wao wa ubatizo na urithi wa kiroho wa mashirika yao. Haya yalisikika tarehe 11 Juni 2026 kutoka kwa Askofu Mkuu Jude Thaddeus Ruwa'ichi, O.F.M. Cap., wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam Tanzania, wakati wa mahubiri kwenye ibada ya misa kwa ajili ya ufunguzi wa  Mkutano Mkuu wa Washiriki wa Mpango wa Watawa Katoliki wa Mfuko wa Conrad N. Hiliton, siku ambayo Mama Kanisa alikuwa anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Barnaba.  Mkutano huo ulifanyika jijini Dar Es Salam kuanzia tarehe 10 hadi 12 Juni 2026, ukiwakutanisha zaidi ya watawa miamoja(130)kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao uliandaliwa na mfuko huo kwa ushirikiano na Umoja wa Watawa Barani Afrika(ACWECA).

Misa ya Ufunguzi wa Muktano wa Mtandao Katoliki wa Watawa wanahusiana na Mpango wa Mfuko wa  Conrad N.Hilton
Misa ya Ufunguzi wa Muktano wa Mtandao Katoliki wa Watawa wanahusiana na Mpango wa Mfuko wa Conrad N.Hilton

Kuiga Fadhila za Mtakatifu Barnaba

Katika mahubiri yake Askofu Rwa’ichi kwa kutazama masomo ya siku na Mtakatifu wa siku hiyo, Askofu Mkuu aliwataka watawa wa kike na kiume na watu wote kuiga fadhila za Mtakatifu Barnaba za wema, imani, na uwazi kwa Roho Mtakatifu. Akitafakari bidii ya umisionari ya mtume na huduma ya unyenyekevu, aliwahimiza watu waliowekwa wakfu kubaki waaminifu kwa wito wao wa ubatizo na karama zao za kipekee. Askofu Mkuu alisisitiza kwamba uaminifu kwa wito wa mtu huchangia ujenzi wa Ufalme wa Mungu na huimarisha maisha ya Kanisa.

Mtakatifu Barnaba mfuasi mwaminifu

Askofu Mkuu alitafakari maisha na ushuhuda wa Mtakatifu Barnaba kama mmoja wa wanafunzi wa kwanza wa Kanisa, akimtambulisha kama kielelezo kwa Wakristo wa leo, akimtaja kama mtu muhimu katika Kanisa la kwanza ambaye alikuwa wa jumuiya ya kwanza ya wanafunzi wa Kristo. Anakumbukwa kama mshirika wa karibu wa Mtakatifu Paulo wakati wa safari zake za kimisionari na kama mwakilishi anayeaminika wa mitume.

Wakati wa misa
Wakati wa misa

Sifa Tatu zilizomtambulisha Barnaba

Akifafanua somo la kwanza, Askofu Mkuu, aliakisi sifa tatu za Mtakatifu Barnaba zilizomfanya Barnaba kuwa kielelezo cha kudumu kwa waamini wote, alikuwa: "mtu mwema, aliyejazwa Roho Mtakatifu na mtu wa imani ya kina. “Kupitia ubatizo, kila Mkristo anaitwa kukuza wema, uwazi kwa Roho Mtakatifu, na imani isiyoyumba,”Askofu Mkuu alisisitiza. Aliomba kwamba kupitia maombezi ya Mtakatifu Barnaba, wote waweze kukua katika fadhila hizi na kuwa mashahidi halisi wa Kristo katika ulimwengu wa leo. Askofu Mkuu alibainisha zaidi kuwa kutokuaminiana kwa Barnaba ni utimilifu wa utume wa Mungu aliokabidhiwa.

Wito wa Uaminifu kwa Utume na Karama

Askofu Mkuu akiwageukia watawa alikiri kwamba zaidi ya utambulisho wao kama Wakristo, wamepokea wito maalum wa maisha ya wakfu, kila mmoja ndani ya Shirika lake  akiwa amebarikiwa na karama yake ya kipekee, na hivyo wanapaswa kujitahidi kubaki waaminifu kwa wito wao wa ubatizo na urithi wa kiroho wa mashirika yao, huku wakitambua mipango na huduma nyingi za kichungaji zinazofanywa na jumuiya za kitawa, na alisisitiza umuhimu wa “kuhifadhi na kuishi kwa karama zao za mwanzilishi.”

Wakati wa Misa
Wakati wa Misa

Ufalme wa Mungu umekaribia

Askofu Mkuu alisisitiza kwamba Yesu aliwaagiza wanafunzi wake kutangaza kwamba “Ufalme wa Mungu umekaribia,” na kwamba wito huu si kwa wanafunzi wa kwanza pekee bali kwa kila Mkristo aliyebatizwa. “Wakati watawa wanapokuwa waaminifu kwa karama yao maalum, wanaimarisha Kanisa na kujenga Ufalme wa Mungu,”alisema. Hatimaye Askofu Mkuu alimwomba Roho Mtakatifu, ambaye alimwongoza Mtakatifu Barnaba kwa bidii ya kichungaji na shauku ya kimisionari, kuwaimarisha wote walioitwa kutumikia Kanisa. Aliomba kwamba waweze kuendelea na utume wao kwa kujitolea, ujasiri, na uaminifu, wakisaidia kuufanya Ufalme wa Mungu uwepo duniani.

Jumla ya washiriki 130 watawa wawakilishi wa mashirika ya ulimwengu
Jumla ya washiriki 130 watawa wawakilishi wa mashirika ya ulimwengu

Watoa mada

Wageni waalika/waalikwa na watoa mada awali ya yote walikuwa Sr. Jane Wakahiu, LSOSF, Makamu Rais Mshiriki wa Operesheni za Programu na Mkuu wa Mpango wa Masista Wakatoliki katika Mfuko wa Conrad N. Hilton, Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, Askofu Luis Manuel Alí Herrera, Katibu Mkuu wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto, Askofu Mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican, Nchini Tanzania, Padre Hans Zollner, SJ, Mkurugenzi wa Taasisi ya Anthropolojia: Masomo ya Taaluma Mbalimbali kuhusu Utu na Utunzaji wa Binadamu(IADC),Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, Roma, Padre Aitor Jimenez, CMF, Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya kitawa na Vyama vya Kitume,  Sr. Alessandra Smerilli, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Nataša Govekar Mkurugenzi wa Idara ya Kitaalimungu-Kichungaji ya Baraza la Kipapa la Mawasiliano na maafisa wengine, Padre Anthony Makunde, Katibu Mkuu wa Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki(AMECEA), Sr. Grace Kyomugisha, Rais wa Chama cha Watawa Afrika Mashariki na Kati (ACWECA), Mapadre, Watawa na wanahabari.

Misa iliudhuria na viongozi wa Curia Romana pia pamoja na AMECEA
Misa iliudhuria na viongozi wa Curia Romana pia pamoja na AMECEA

Mtakatifu Barnaba

Kuhusu Mtakatifu Barnaba,  tunasoma kwamba "Na kundi la waamini lilikuwa na moyo mmoja na roho moja, wala hakuna mtu aliyesema kwamba mali yake ni yake mwenyewe, bali walikuwa na vitu vyote shirika… Kwa maana hapakuwa na mtu yeyote miongoni mwao aliyehitaji, kwa maana wote waliokuwa na mashamba au nyumba waliviuza, wakaleta fedha na kuziweka miguuni pa mitume. Kila mtu akagawiwa kadiri alivyohitaji. Basi Yosefu, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake 'Mwana wa Faraja,') Mlawi, mzaliwa wa Kupro, aliyekuwa na shamba, aliliuza, akaleta fedha na kuziweka miguuni pa mitume”(Mndo 4:32-37).

Biblia inamtaja Barnaba kwa mara ya kwanza miongoni mwa wale waliokusanyika karibu na mitume huko Yerusalemu baada ya kifo cha Yesu. Ni jumuiya ya waamini wanaoishi katika udugu, wakishiriki mali zao. Lakini mapokeo, yaliyoripotiwa na Eusebius wa Kaisaria, anayemtegemea Clement wa Aleksandria pia yanamtaja miongoni mwa wanafunzi 72 waliotumwa na Yesu kwenda katika utume wa kutangaza Ufalme wa Mungu, hivyo tayari akiwa ndani ya mzunguko wa wafuasi wa Kristo. Kuhusu asili yake, tunajua kutoka katika Maandiko Matakatifu kwamba, alizaliwa katika kisiwa cha Kupro(Cyprus), alikuwa Myahudi na jina lake lilikuwa Yosefu.

Watoa mada za mafunzo  katika Mkutano wa watawa huko Dar Es Salaam
Watoa mada za mafunzo katika Mkutano wa watawa huko Dar Es Salaam
ASK.MKUU RUWA'ICHI NA WITO KWA WATAWA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

13 Juni 2026, 11:50