Tafuta

Misa kwa ajili ya Mkutano Mkuu ulioandaliwa na Mfuko wa Conrad N. Hilton pamoja na Umoja wa Watawa Wakatoliki barani Afrika(ACWECA). Misa kwa ajili ya Mkutano Mkuu ulioandaliwa na Mfuko wa Conrad N. Hilton pamoja na Umoja wa Watawa Wakatoliki barani Afrika(ACWECA). 

Ask.Mkuu Accattino:Tunapotetea haki,tunaonesha moyo wa Kristo

Tumechaguliwa na upendo,tumeitwa kupenda,tunadumishwa na upendo,na tunasukumwa na upendo.Ni maneno yaliyoongoza mahubiri ya Askofu Mkuu Accattino,Balozi wa Vatican nchini Tanzania katika hitimisho la Mkutano Mkuu wa Mpango wa Watawa Katoliki wa Mfuko wa Conrad N.Hiliton,Juni 12,Dar Es Salaam.Balozi alihimiza watawa kutumia fursa waliyopewa kuwanufaisha wengine kama watu binafsi,jamii,au taasisi,wakisukumwa na furaha ya Injili.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Tunapozingatia mahitaji ya wale ambao wako katika aina yoyote ya dhiki ya kijamii, kiuchumi, au kisaikolojia, tunagusa majeraha ya Kristo, tunapotetea haki, tunaonesha moyo wa Kristo, tunapojenga madaraja kati ya watu, tunaakisi ushirika wa Kristo. Haya na mengine mengi yamo katika mahubiri ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, katika hitimisho la Mkutano mkuu wa Mpango wa Masista Wakatoliki 2026 ulioandaliwa na Mfuko wa Conrad N. Hilton pamoja na Umoja wa Watawa Wakatoliki barani Afrika(ACWECA), uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania kuanzia tarehe 10 hadi 12 Juni 2026 huku ukiwakutanisha pamoja watawa 130 wa mashirika mbalimbali wanaohusika katika Mpango wa Mfuko huo kutoka duniani kote.

Picha ya pamoja ya kundi la washiriki wa Mkutano huko Dar es Salaam 10-12 Juni 2026
Picha ya pamoja ya kundi la washiriki wa Mkutano huko Dar es Salaam 10-12 Juni 2026

Mkutano huo  uliongozwa na kauli mbiu: "Kusafiri Pamoja katika Mshikamano na Matumaini: Kuimarisha Jumuiya na Kukuza matokeo ya pamoja kwa ajili ya Manufaa ya Wote.”Katika mahubiri yake Mwakilishi wa Baba Mtakatifu, yalizingatia Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ya siku hiyo ambapo  tafakari yake iligawanywa katika sehemu kuu nne ikiwa na utangulizi ambao pia alizungumza juu ya Waraka wa Kwanza wa Baba Mtakatifu Leo XIV wa  Magnifica Humanitas: tumechaguliwa na upendotumeitwa kupendatunadumishwa na upendo, na tunasukumwa na upendo katika matendo. Tunachapisha taakari hii ya kina.

Akianza Askofu Mkuu alieleza kiini cha kukutana "Tunakusanyika leo kutoka mataifa, tamaduni, na mazingira mengi. Lakini tumeunganishwa na wito mmoja, kuwa wa Kristo na kuwatumikia watu wake, hasa walio dhaifu zaidi. Kwa namna ya pekee, Mungu anawahimiza kufanya kazi bila kuchoka kwa bidii na ujasiri. Na kwa msaada wake, mnaweza kufikia na kugusa maisha ya watu wengi kwa kuinua hadhi yao. Mkutano huu wa kimataifa wenyewe ni ishara hai ya Kanisa, lenye utofauti, lakini lenye mizizi katika upendo, lakini limetumwa kwenye utume. Tanzania imebarikiwa kuandaa mkutano huu mwaka huu. Sifurahii tu, bali pia nimebahatika kuwakaribisha Dar es Salaam, idadi nzuri ya wakuu na maafisa kutoka mabaraza tofauti ya Curia Romana Vatican, ambao uwepo wao umeleta uboreshaji maalum kwa tukio hili."

Nyakati za misa na sala
Nyakati za misa na sala

Balozi wa Vatican alitoa shukrani  na kutambua kwa  "heshima kubwa Mfuko wa Conrad N. Hilton, ambao umekuwa msingi katika mpangilio huu wa haya yote. Nadhani sababu kubwa zaidi kwa nini tuko hapa kukusanyika katika sherehe kama hii ni kwa sababu bado tunaamini katika ubinadamu. Tunajiona bado ni binadamu, katika ulimwengu ambao hauonekani kuwa na uhakika zaidi kwamba hii bado ni thamani. Ndiyo, sisi ni wa ubinadamu huo mzuri ambao Papa wetu mpendwa Leo XIV aliuweka wakfu Waraka wake wa kwanza ya hivi karibuni wa Magnifica Humanitas.  Ni lazima tutiwe moyo na maneno ya Baba Mtakatifu wakati, katika kifungu cha  pili cha  hati hiyo anasema: “Kwa msingi wa Kristo, jiwe lililo hai, tunapata uzoefu wa utendaji wenye nguvu na wa ajabu wa Roho Mtakatifu na tunaamini kwamba kila jitihada za kweli za kibinadamu za kushirikiana Naye na kwa wema zitabarikiwa na Baba yetu wa Mbinguni ambaye tunaweka tumaini letu."

Kutafuta njia mpya kwa manufaa ya wote

Askofu Mkuu alileza kwamba katika hili inawezekana "kuchangia kwa bidii kwa kila mpango unaojenga ulimwengu wenye haki zaidi na tunaweza kuwaita wengine kushirikiana katika kuhamasisha maendeleo fungamani  ya kila mwanadamu. Tunataka kushiriki katika mazungumzo na wanaume na wanawake wote wa wakati wetu, ambao tunashiriki nao, katika matukio haya, maswali na matarajio ya ubinadamu. Pamoja nao, tunatafuta kutambua njia mpya kwa manufaa ya wote na kwa ajili ya kuendeleza maisha yenye heshima kwa wote. Hakika, uwazi kwa mazungumzo ni sehemu muhimu ya wito wa Kanisa…,”(Humanitas Magnifica n.2). Ni rahisi kuona katika nukuu hii maneno machache muhimu: Ushirikiano, mpango, ushiriki, maendeleo fungamani, mazungumzo, mema ya wote, n.k."

Askofu Mkuu Accattino "Hili si eneo na wakati sahihi wa kuchanganua kila moja, lakini kwa pamoja, yanatupatia hisia na uhakika kwamba pia mpango ambao mmekuwa mkisherehekea na kuuimarisha katika siku zilizopita, ikiwa mmejikita vizuri katika Injili, katika ushirika kamili na Baba Mtakatifu na kuongozwa na Roho Mtakatifu, ni ushiriki wa asili na wito wa Kanisa. Lakini kitovu cha sherehe yetu leo hii ni Fumbo la Moyo Mtakatifu wa Yesu, moyo unaofunua kina cha upendo wa Mungu, moyo unadunda kwa huruma ya wanadamu, moyo unaotualika sio tu kutafakari upendo, bali pia kuudhihirisha. Leo, tunaalikwa kutafakari upendo wa kibinadamu na wa kimungu wa Kristo, unaowakilishwa na moyo uliochomwa kama ishara ya upendo usio na masharti na wenye huruma kwa wanadamu wote. Liturujia inatupatia njia ya kufuata."

Wakati wa kutembelea mipango ya masista katika vitengo tofauti hata elimu
Wakati wa kutembelea mipango ya masista katika vitengo tofauti hata elimu

Kwanza:Tumechaguliwa kwa upendo na huu ndio msingi wa safari

Katika somo la Kwanza, alisema kuwa "Musa anawakumbusha watu, "Ninyi ni watu watakatifu kwa Bwana, Mungu wenu. Amewachagua ninyi kutoka mataifa yote juu ya uso wa dunia kuwa watu wake wa pekee. Anaweka moyo wake juu yenu kwa sababu Bwana anawapenda." Hapa ndipo kila kitu kinapoanza, si kwa utume wetu, si kwa mkakati wetu, si hata kwa ukarimu wetu, bali kwa upendo wa Mungu. Taswira ya Mungu akiweka moyo Wake kwa watu Wake inagusa sana ibada ya Moyo Mtakatifu. Hatuchaguliwi kwa sababu tuko wengi, wenye nguvu, au wenye uwezo, bali kwa sababu moyo wa Mungu upo juu yetu."

Musa anawakumbusha watu kutambua utu wao kulingana na upendo 

Balozi wa Vatican aliendelea kudadavua kwamba, "hili ni kweli kwa kila mmoja wetu, na hasa kwa kila mmoja wenu: wito wenu, dada wapendwa, utakaso wenu, kujitolea kwenu kwa mshikamano wa kimataifa, haya ni majibu ya upendo uliokuja kwanza. Ukweli huu lazima ubaki kuwa msingi wa safari pamoja, bila huo, utume unakuwa uanaharakati, ushirikiano unakuwa uratibu tu, na huduma ina hatari ya kuwa mzigo. Kinyume chake, tunapokumbuka kwamba tumechaguliwa na upendo, kila kitu hubadilika kazi yetu inakuwa ushiriki katika tendo la upendo la Mungu mwenyewe duniani. Musa anawakumbusha watu kutambua utu wao kulingana na upendo usio na kikomo wa Mungu, unaoonyeshwa na hatua mbalimbali za kukabiliana na mahitaji yao, hasa wakati wa hali ngumu, Mungu alichagua kushiriki ubinadamu wetu na akawa kama sisi, isipokuwa dhambi."

Nyakati mbalimbali za furaha wakati wa mkutano wao
Nyakati mbalimbali za furaha wakati wa mkutano wao

Kwa kusisitiza zaidi juu ya upendo wa Mungu alisema,  "Hili lazima litusukume kutambua sisi ni nani na jinsi maisha yetu yalivyo ya thamani. Kwa kusikitisha, tuna mifano mingi ya hali ambazo ubinadamu unajeruhiwa na ukosefu wa upendo. Hebu tuwafikirie wale kaka na dada, wanaoishi katika maeneo ya migogoro, wamenaswa katikati ya vita ambavyo hawakuvitaka na hata hawaelewi au wamegubikwa tu na changamoto zinazotokana na migongano ya ulimwengu wa leo, ambapo ongezeko la ustawi na chaguzi linapingana na vikwazo vya haki za kiraia na za binadamu, na kufanya maisha kuwa magumu. Tunakabidhi   kwa uangalizi wa huruma ya Kristo, na awaguse mioyo ya wale waliohusika ili kukomesha mateso ya wanadamu na kutoa mwanga wa matumaini, uhuru, haki, na furaha kwa kila mtu."

Hatua ya pili:Mungu ni upendo

Balozi wa Vatican aliendelea kusema kuwa "Upendo huu ndio moyo wa utume wetu, kwa sababu somo la pili kutoka Waraka wa Kwanza wa Yohane linatuleta kwenye kiini cha imani yetu, yaani “Mungu ni upendo, na yeyote anayekaa katika upendo anakaa ndani ya Mungu.” Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kielelezo halisi cha ukweli huu, si wazo la kufikirika, bali ni moyo ulio hai, uliojeruhiwa, wenye huruma unaoendelea kupenda, kusamehe, na kuwavuta watu wote kwake. Kitendo chochote cha mshikamano kinachochipuka kutoka kwenye maji na damu inayotiririka kutoka kifua wazi cha Kristo, katika kiwango chake cha ndani kabisa, ni ushiriki katika upendo huu. Lakini somo hili pia linatupatia changamoto. Tupendane kwa sababu upendo ni wa Mungu, hapa ndipo mada ya mkutano wenu inakuwa thabiti sana kusafiri pamoja katika mshikamano na tumaini linamaanisha kwanza kupendana, si kwa njia ya kufikirika, bali katika uhalisia wa kila siku wa maisha ya jumuiya, ushirikiano, na umoja."

Washiriki wa Mkutano
Washiriki wa Mkutano

Uvumilvu katika utofauti na msamaha katika mivutano

"Inamaanisha uvumilivu katika utofauti, msamaha katika mivutanoukarimu katika kushiriki, na unyenyekevu katika kujifunza, tunapozingatia mahitaji ya wale ambao wako katika aina yoyote ya dhiki ya kijamii, kiuchumi, au kisaikolojia, tunagusa majeraha ya Kristo, tunapotetea haki, tunaonesha moyo wa Kristo, tunapojenga madaraja kati ya watu, tunaakisi ushirika wa Kristo." Wito huu wa Mtakatifu wa Yohane ni wito wa kufuata amri mpya za kupendana kama Kristo alivyotupenda kwa kutoa maisha yake kwa ajili yetu, hii inahusisha kujitolea, na kila kitu kinahusisha kujitolea. Pia msingi wenu unahusisha kujitolea, kwa muda, nguvu, na, bila shaka, pesa, ni sadaka iliyotolewa kwa furaha na watu tofauti ambao, kutokana na upendo na kuunganishwa na upendo, wanatoa tabasamu na uaminifu kwa wale ambao wamepoteza tumaini, Mungu awabariki, na aruhusu juhudi zenu kufikia, iwezekanavyo, makundi mengi ya watu duniani kote."

Hatua ya tatu:Upendo wa pamoja, hii ni kujifunza njia ya moyo

Katika Injili, Yesu anatoa sala na mwaliko, anamshukuru Baba kwa kufunua siri za ufalme kwa wadogo, hii ni fundisho kubwa kwetu, hasa katika mkutano wa Kimataifa ambapo uzoefu wa pamoja, utaalamu, na uwajibikaji ni mwingi. Yesu anatukumbusha kwamba hekima ya ndani kabisa haihifadhiwi kwa wenye nguvu waliojifunza, bali kwa wanyenyekevu. Hii inatuita kwenye mwelekeo mpya, njia ya kutangulia ambayo inathamini kusikiliza kuliko kudhibiti, kujifunza kuliko kujidhania na unyenyekevu kuliko kujitosheleza. Wito huu unatutia moyo kukuza ndoto na mipango yetu bora lakini kisha tunatambua kwamba, peke yetu, tunaweza kufanya kidogo sana, ikiwa kuna chochote.

Sr. Jane Wakahiu,LSOSF,Makamu Rais na Mkuu wa Mpango wa Masista Wakatoliki katika Mfuko wa Conrad N.Hilton,
Sr. Jane Wakahiu,LSOSF,Makamu Rais na Mkuu wa Mpango wa Masista Wakatoliki katika Mfuko wa Conrad N.Hilton,

"Umoja ni nguvu"

Balozi wa Vatican nchini Tanzania alieleza kuwa "Hapa ndipo tunapaswa kuwa wanyenyekevu sana ili kutambua umuhimu wa msemo maarufu wa Kiitaliano unaosema, L’unione fa la forza, yaani Umoja ni Nguvu.” Katika hali yenu halisi, mtazamo huu umekuwa muhimu katika ushirikiano kati ya Shirika la Kimataifa la Watawa na taasisi ya upendo kama vile Mfuko wa Conrad N. Hilton, liliounda Mtandao wa Kimataifa na mipango ya kimkakati, kila mtu analeta kitu kwa ajili ya matokeo bora zaidi. Kwa namna fulani, inawezekana kuona katika hali hii njia ya sinodi ambayo tumeitwa sio tu kuleta maarifa, bali kuyapokea, sio tu kutumikia, bali kubadilishwa na huduma tunayotoa, sio tu kuongoza, bali kutembea pamoja. Hii ni kujifunza njia ya moyo wa Kristo, ambao ni mpole na mnyenyekevu. Kinyume cha hili, wakati ubinafsi unapotawala kila kitu kingine, ni mkusanyiko wa ubinafsi badala ya kushiriki, kiburi badala ya unyenyekevuutajiri kama sababu pekee maishaniufisadi badala ya uadilifu, na muda unaotumika kwa wengine, kiukweli, kuwa, chombo cha kupata maslahi binafsi tu."

Hatua ya nne:Upendo katika matendo, ambayo ndiyo nguvu ya safari

"Yesu anaendelea, “Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Tunatiwa moyo na maneno haya, kwa kuwa upendo wa Mungu unategemea kujitolea na kujitolea. Dada wapendwa, utume kama wenu ni mzuri, lakini pia unahitajika, unamaanisha kushughulikia hali halisi ya umaskiniukosefu wa haki, kuhama, na mateso, ukifanya kazi duniani kote, mizigo hii inaweza kuzidishwa kwa umbalikwa tofauti za kiutamaduni, au kwa changamoto za kimuundo. Yesu hakatai mapambano, anakubali na anatualika sote tusijiondoe kwenye utume, bali tupate nguvu ndani Yake, na Moyo Mtakatifu ni mahali pa kupumzika. Ni mahali ambapo aina yoyote ya uchovu hupokelewa, ambapo majeraha huponywa, ambapo tumaini hurejeshwa. Lakini Yesu pia anasema, “Jitwikeni nira yangu na mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.” Hili si kuhusu kupokea pumziko tu, bali pia ni kuhusu kushiriki njia Yake ya kubeba utume, nira yake ni rahisi si kwa sababu kazi ni nyepesi, bali kwa sababu hubebwa katika upendo, katika ushirika, na katika uaminifu."

Padre Hans Zollner, SJ, Mkurugenzi wa Taasisi ya Anthropolojia: Masomo ya Taaluma Mbalimbali kuhusu Utu na Utunzaji wa Binadamu(IADC), ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, Roma,
Padre Hans Zollner, SJ, Mkurugenzi wa Taasisi ya Anthropolojia: Masomo ya Taaluma Mbalimbali kuhusu Utu na Utunzaji wa Binadamu(IADC), ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, Roma,

Upendo ndiyo rasilimali kuu

Kwa hivyo, kwa kuhitimisha, Askofu Mkuu Accattino alisema kuwa "upendo ndiyo rasilimali kuu, tukiwa na mawazo yetu yaliyowekwa kwenye Moyo Mtakatifu wa Yesu, tumesindikizwa na tafakari hizi kwa neno linalodumu, ambalo ni upendo. Tunatafakari tena ukweli mkuu wa ujumbe wa leo: tumechaguliwa na upendotumeitwa kupendatunadumishwa na upendo, na tunasukumwa na upendo. Upendo upo kila wakati, katika wakati wowote wa kuwepo kwetu, tumeumbwa kutokana na upendo, tumeelimishwa kutokana na upendo, tunaweza kufanya tofauti katika uelewa wetu wa kila siku tukitenda kutokana na upendo, na mwishoni mwa maisha yetu, tutahukumiwa kwa upendo. Ni kwa kiasi gani tumeweza kuruhusu kukua katika mbegu hiyo ya upendo iliyopandwa ndani yetu tangu tuwe tumefikiriwa na Mungu kama ahadi ya wokovu wetu wa milele?"

Tumieni fursa hii mkisukumwa na furaha ya Injili

"Dada wapendwa, fursa mliyopewa ya kutekeleza mipango ya maendeleo ya aina yoyote na kuwanufaisha wengine kama watu binafsi, jamii, au taasisi, ni fursa." Askofu Mkuu alisisitiza, "Tumieni fursa hii mkisukumwa na furaha ya Injili, kama vile Papa wetu mpendwa Francisko alivyowaalika wanadamu wote kufanya, lakini pia kwa busara na ufanisi daima, kama ilivyosemwa mwanzoni, katika ushirika mkamilifu na Baba Mtakatifu, Kiti Kitakatifu, na Majisterio ya Kanisa, kwa kuwa haya ndiyo matawi na uhakikisho unaotufanya kuwa matawi ya mzabibu wa ulimwengu wote, yaliyopandwa na Mkombozi wetu na kusaidiwa kila siku na mlinzi wa mzabibu, ambaye ni Roho Mtakatifu. Mungu Mwenyezi asindikize shughuli zenu kila wakati, na matokeo ya mkutano huu yawe chanzo cha nguvu ya kusonga mbele, na pia malengo mliyojiwekea yatimizwe kwa neema ya Mungu. Amina."

Balozi wa Vatican akiwa katikati ya wanawakwaya wa kike
Balozi wa Vatican akiwa katikati ya wanawakwaya wa kike
Balozi wa Vatican nchini Tanzania akiwa katikati ya Wanakwaya wa kiume
Balozi wa Vatican nchini Tanzania akiwa katikati ya Wanakwaya wa kiume

Wageni waalikwa na wato mada

Kuhusu Mkutano huu wageni waalika/waalikwa na watoa mada awali ya yote walikuwa Sr. Jane Wakahiu, LSOSF, Makamu Rais Mshiriki wa Operesheni za Programu na Mkuu wa Mpango wa Masista Wakatoliki katika Mfuko wa Conrad N. Hilton, Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, Askofu Luis Manuel Alí Herrera, Katibu Mkuu wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto, Askofu Mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican, Nchini Tanzania, Padre Hans Zollner, SJ, Mkurugenzi wa Taasisi ya Anthropolojia: Masomo ya Taaluma Mbalimbali kuhusu Utu na Utunzaji wa Binadamu(IADC), ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, Roma, Padre Aitor Jimenez, CMF, Katibu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya kitawa na Vyama vya Kitume,  Sr. Alessandra Smerilli, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Nataša Govekar Mkurugenzi wa Idara ya Kitaalimungu-Kichungaji ya Baraza la Kipapa la Mawasiliano na maafisa wengine, Padre Anthony Makunde, Katibu Mkuu wa Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki(AMECEA), Sr. Grace Kyomugisha, Rais wa Chama cha Watawa Afrika Mashariki na Kati (ACWECA), Mapadre, Watawa na wanahabari.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

 

15 Juni 2026, 09:05