Tafuta

Kongamano la Sita la Kitaifa la Utoto Mtakatifu lililokuwa limepangwa kufanyika kuanzia tarehe 18 hadi 22 Juni 2026 katika Jimbo Katoliki la Kigoma limeahirishwa. Kongamano la Sita la Kitaifa la Utoto Mtakatifu lililokuwa limepangwa kufanyika kuanzia tarehe 18 hadi 22 Juni 2026 katika Jimbo Katoliki la Kigoma limeahirishwa. 

Kongamano la Utoto Mtakatifu Nchini Tanzania Limeahirishwa

Ni katika muktadha wa malezi na makuzi ya watoto Tanzania, Kongamano la Sita la Kitaifa la Utoto Mtakatifu lililokuwa limepangwa kufanyika kuanzia tarehe 18 hadi 22 Juni 2026 katika Jimbo Katoliki la Kigoma limeahirishwa hadi hapo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania litakapo tangaza tena. Uamuzi huu mzito ni matunda ya tafakari ya kina iliyotolewa na Maaskofu kwa kusoma alama za nyakati na kwa kusukumwa na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Utoto Mtakatifu lilianzishwa kunako mwaka 1843 na Askofu Charles Toussaint de Frobin Janson wa Jimbo Katoliki la Nancy. Kunako mwaka 2023, Shirika la Utoto Mtakatifu limeadhimisha Jubilei ya Miaka 180 tangu kuanzishwa kwake. Askofu Charles de Frobin Janson kwa njia ya barua kutoka China, alitambua kwamba, kuna watoto wengi waliokuwa wanapoteza maisha yao kutokana na kukumbwa na baa la njaa pamoja na kuishi katika mazingira magumu na hatarishi na huo ukawa mwanzo wa Shirika la Utoto Mtakatifu, ili kuhakikisha kwamba, watu wote wanapata wokovu kiroho na kimwili kwa sababu Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kuwakomboa watu wote! Itakumbukwa kwamba, Shirika la Utoto Mtakatifu, lilianzishwa ili kujibu changamoto na hivyo kutoa mwaliko kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari, moyo na mwamko wa kimisionari ili kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia.

Utoto Mtakatifu Ulianzishwa kunako mwaka 1843
Utoto Mtakatifu Ulianzishwa kunako mwaka 1843

Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; watoto wanaokumbana na magonjwa, baa la njaa, ujinga na umaskini. Hata katika umaskini wao, watoto bado wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia! Kristo Yesu, alitoa kipaumbele cha pekee kwa watoto katika maisha na utume wake. Watoto wanapaswa kujifunza na kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Mshikamano wa upendo, umewawezesha watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuguswa na mahangaiko ya watoto wenzao kiasi cha kujinyima na kuchangia kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao! Leo hii, haki msingi za watoto sehemu mbalimbali za dunia zinaendelea: kusiginwa na kuvunjwa, kiasi kwamba, watoto wananyanyaswa na kudhulumiwa; wanapokwa haki yao ya utoto kwa kufanyishwa kazi za suluba; kwa kusumbuliwa na: umaskini, magonjwa, ujinga, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; kwa vita na majanga mbalimbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu!

Watoto wakimwomba baraka Askofu Msonganzila
Watoto wakimwomba baraka Askofu Msonganzila

Watoto hata katika changamoto zote hizi, bado wanaweza kusaidiwa kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimisionari, kwa kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano. Kwa njia hii watoto wamesaidia kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuwapatia watoto wenzao mahitaji msingi kama vile: chakula, elimu, makazi na huduma bora ya afya. Ni katika muktadha wa malezi na makuzi ya watoto nchini Tanzania, lile Kongamano la Sita la Kitaifa la Utoto Mtakatifu lililokuwa limepangwa kufanyika kuanzia tarehe 18 hadi 22 Juni 2026 katika Jimbo Katoliki la Kigoma limeahirishwa hadi hapo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania litakapo tangaza tena. Uamuzi huu mzito ni matunda ya tafakari ya kina iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kwa kusoma alama za nyakati na kwa kusukumwa na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wao. Ofisi ya Mashirika ya Kipapa, Taifa inatoa pole nyingi kwa usumbufu utakaojitokeza na kuwaomba waamini kuyapokea mabadiliko haya ambayo yamefanyika kwa kuzinagatia maslahi mapana zaidi ya watoto nchini Tanzania na Kanisa katika ujumla wake. Ofisi inawashukuru wale wote waliokwisha kukamilisha michango ya ona kwamba, michango yote ya ushiriki ambayo imekwisha kuwasilishwa ofisini, iko mikononi salama na ile ambayo bado iko majimboni iendelee kuhifadhiwa vizuri, hadi hapo tarehe mpya ya kongamano itakapo tolewa tena na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC.

Kongamano Utoto Mtakatifu
30 Mei 2026, 14:50