Tafuta

Umoja wa mataifa, New York -Marekani. Umoja wa mataifa, New York -Marekani. 

Vatican,ECOSOC 2026:ikiwa tunakubali wanadamu wote ni sawa,tusipuuze tofauti zao!

Kiini cha ufadhili wa maendeleo,kama ilivyothibitishwa na Ahadi ya Sevilla,ni"kuwaweka watu katikati ya vitendo vyetu vyote na kuthibitisha tena njia ya mustakabali mzuri zaidi kwa wanadamu wote."Alisema hayo Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa katika hafla ya Jukwaa la ECOSOC la 2026 kuhusu‘Ufuatiliaji wa Ufadhili wa Maendeleo’huko New York,Marekani Aprili 23.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

“Jambo la kuhangaikia zaidi ni pengo linaloongezeka kati ya ahadi zilizotolewa katika mifumo ya kimataifa na hali halisi ya mabilioni ya watu, hasa katika nchi zenye maendeleo duni, nchi zinazoendelea zisizo na bandari, na nchi ndogo zinazoendelea za visiwa. Mizigo ya madeni inazuia uwekezaji wa umma katika huduma ya afya, elimu, na ulinzi wa kijamii. Ahadi za misaada ama hazitimiziwi au zinavunjwa huku matumizi ya silaha yakiongezeka.” Alisema hayo Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa wakati wa  hotuba yake katika hafla ya Jukwaa la Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa(ECOSOC) la 2026, kuhusu ‘Ufuatiliaji wa Ufadhili wa Maendeleo,’  huko New York Marekani tarehe 23 Aprili 2026. Ujumbe wake ulikaribisha kuitishwa kwa “Jukwaa la mwaka huu, la kwanza tangu Ahadi ya Sevilla ilipopitishwa mwezi Julai  2025. Hati hiyo inakubali kwamba mfumo wa sasa wa ufadhili wa maendeleo unapungua na kwamba mbinu zenye malengo makubwa na usawa zinahitajika haraka.”

Thamani yao lazima ipimwe kwa uwezo wao ya kuumbwa kwa mfano wa Mungu

Mwakilishi wa Vatican alisisitiza kuwa “Kiini cha ufadhili wa maendeleo, kama ilivyothibitishwa na Ahadi ya Sevilla, ni "kuwaweka watu katikati ya vitendo vyetu vyote na kuthibitisha tena njia ya mustakabali mzuri zaidi kwa wanadamu wote." Kwa hivyo, tunapojadili vipengele vya kiufundi vya ufadhili wa kimataifa, watu lazima wawe katikati ya maendeleo. Mifumo na zana za kifedha ni njia tu ya kufikia lengo. Hatimaye, thamani yao lazima ipimwe kwa uwezo wao wa kudumisha hadhi ya asili iliyotolewa na Mungu ya kila mtu, na kukuza ustawi wa wote, hasa maskini zaidi na wenye uhitaji zaidi.”

Mizigo ya madeni inazuia uwekezaji wa umma katika huduma ya afya,elimu na ulinzi wa kijamii

Vatican aidha inabainisha kwamba,  “Jambo la kuhangaikia zaidi ni pengo linaloongezeka kati ya ahadi zilizotolewa katika mifumo ya kimataifa na hali halisi ya mabilioni ya watu, hasa katika nchi zenye maendeleo duni, nchi zinazoendelea zisizo na bandari, na nchi ndogo zinazoendelea za visiwa. Mizigo ya madeni inazuia uwekezaji wa umma katika huduma ya afya, elimu, na ulinzi wa kijamii. Ahadi za misaada ama hazitimiziwi au zinavunjwa huku matumizi ya silaha yakiongezeka. Wale walio katika hali hatarishi wanaendelea kubeba gharama kubwa zaidi za migogoro ambayo hawakusababisha. Hili si tu kushindwa kwa sera, bali pia ni jambo la kimaadili.”

Ikiwa tunakubali kuwa wanadamu wote wana utu sawa, tusipuuze tofauti zao

Kwa njia hiyo himizio la  ufadhili wa kibinafsi lazima uelekee sio tu kwa faida ya uwekezaji, bali kwa manufaa ya wote. Pia inazitaka nchi zenye madeni kuwajibika zaidi kwa matumizi yao na kuhakikisha kwamba fedha zinatumika kwa maendeleo. Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican alihitimisha kwa kunukuu neno kutoka kwa Papa Leo XIV ambaye anathibitisha kwamba "ikiwa tunakubali kwamba wanadamu wote wana utu sawa, bila kujali mahali pao pa kuzaliwa, tofauti kubwa zilizopo kati ya nchi na maeneo hazipaswi kupuuzwa."

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

25 Aprili 2026, 14:59