Mbegu za matumaini:Mahali ambapo imani inaishi na miito huongezeka!
Na Sr. Christine Masivo,CPS – Vatican.
Siku ya Maombi kwa Miito Duniani, iliyoanzishwa na Papa Paulo VI mwaka 1964, inaendelea kurudia mwaliko wa Kristo, "Mwombeni Bwana wa mavuno awatume watenda kazi katika mavuno yake" (Mt 9:38). Katika Dominika ya Mchungaji Mwema, ni siku hii inayoelekeza umakini kwenye nia maalum na hitaji kubwa ya miito ya upadre na utawa katika Kanisa. Katika Dominika ya Nne ya Pasaka ambayo kiutamaduni inaitwa Dominika ya Mchungaji Mwema iliadhimisha kwa mwaka kuu tarehe 26 Aprili 2026. Baba Mtakatifu Leo XIV aliongoza hata Misa Takatifu katika Basilika ya Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa kuwapatia draja la Upadre, kwa mapadre wapya kumi wa Jimbo la Roma.
Wito uliojikita katika moyo wa Kanisa
Katika ulimwengu ambapo neno "wito" mara nyingi hujumuisha njia yoyote ya maisha au taaluma, Kanisa linatuita turudi kwenye maana yake muhimu yani, mwaliko wa kimungu kwa upadre na utawa. Siku hii si ya mfano tu, ni mvuto wa kiroho unaotokana na ukweli kwamba Kanisa bado linahitaji wachungaji, wa kike nawa kiume walio tayari kujitolea maisha yao yote kutangaza Injili kwa kutumikia Kanisa.
Ishara za matumaini kutoka maeneo ya utume wa kimisionari
Takwimu za hivi karibuni zilizoshirikishwa zinaonesha mwelekeo wa ajabu, kwani miito inaongezeka kwa kasi, hasa barani Afrika na Asia. Kuanzia seminari 778 zenye waseminari 82,859 mwaka 2023/24 hadi seminari 801 zenye waseminari 88,156 mwaka 2024/25, ni ishara ya kutia moyo. Ongezeko hili si la kitakwimu tu, bali linaonesha imani hai ya jamii ambapo Ukristo unaishiwa kwa imani na furaha. Kwa mujibu wa Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides, katika fursa ya Siku hii, lilibainisha kwamba, asilimia kubwa ya vijana wanaoitikia wito huo wanatoka katika malezi ya unyenyekevu. Mara nyingi uzoefu wao huzidisha usikivu wao kwa mateso ya wanadamu na kuamsha hamu ya kutumikia. Katika ukimya, sala, na ustahimilivu, hugundua sauti ya upole ya Mungu ikiwaalika kwenye jambo kubwa zaidi, alibainisha Padre Guy Bognon. Kama Mtakatifu Papa Yohane Paulo wa II alivyowahi kuthibitisha kuwa “wito wa Mungu hauzuii uhuru wa binadamu bali unautimiza. Pale imani inapokuwa hai, miito huota mizizi kiasili.”
Imani hai na inayoishi uzoefu
Miito hustawi pale ambapo imani si vuguvugu. Jumuiya zinazoadhimisha sakramenti kwa uaminifu, hutoa katekesi imara, na kubaki wazi kwa mafundisho kamili ya Kanisa huwa ardhi yenye rutuba ya utambuzi. Katika maeneo kama hayo, vijana hukutana na imani yenye furaha, inayohitaji nguvu, na yenye mabadiliko. Muhimu vile vile ni uwepo wa wahudumu wa kichungaji waliojitolea, mapadre, watawa, na makatekista wanaotembea, wakiwasaidia na kuhimiza vijana katika safari ya imani. Utume wa miito haihitaji kuwa na ugumu bali inahitaji kufanywa kwa ukaribu, uhalisi, na kwa uangalifu na upendo. Pale ambapo vijana wanasikilizwa na kuongozwa, wao hupata uhuru wa kuitikia wito wa Mungu kwa ukarimu na kwa hiari. Umuhimu unaoendelea wa Seminari ndogo pia unajitokeza wazi. Taasisi hizi hulea ishara za mwanzo za wito, zikiwasaidia vijana kukua kiroho na kibinadamu. Bado ni chanzo muhimu cha wote wenye nia ya kumtumikia Mungu kama mapadre na watawa, hasa katika maeneo ya umisionari.
Wajibu wa pamoja kwa Kanisa la Ulimwengu wote
Ukuaji wa miito ni kazi ya utulivu lakini isiyoweza kuepukika ya Shirika la Kipapa la Mtakatifu Petro Mtume. Imejitolea kusaidia miito katika maeneo ya umisionari, hutoa rasilimali muhimu kwa seminari na vituo vya malezi. Kuanzia kufadhili shughuli za kila siku hadi kutoa ufadhili wa masomo na kusaidia miundombinu, misheni yake inahakikisha kwamba hakuna wito wa kweli unaopotea kutokana na ukosefu wa kitu chochote. Takwimu hizi zinashangaza, mamia ya Seminari nyingi na maelfu ya Waseminari na Manovisi wanaotegemea msaada huu, wengi wao wakiwa Afrika na Asia. Bila msaada kama huo, taasisi nyingi zingefungwa, na vijana wengi hawangeweza kuendelea na wito wao. Hata hivyo, jukumu hilo haliko juu ya taasisi moja pekee. Uundaji wa mapadre na watawa wa baadaye ni wa Kanisa lote. Kila sala, kila tendo la ukarimu, huchangia katika kudumisha utume.
Mavuno bado ni mengi
Licha ya ukuaji unaotia moyo, hitaji la miito linabaki kuwa la dharura. Mashamba ni mengi, na utume mwingi unaendelea kupanuka. Kuongezeka kwa miito barani Afrika na Asia ni ishara yenye nguvu ya matumaini, lakini pia ni ukumbusho kwamba, Kanisa lazima liendelee kuwa makini kusali, na kuungana. Katika Siku ya Maombi ya Miito Ulimwenguni, mwaliko uko wazi, kusali, kwa kuomba sana, kuunga mkono, na kuamini kwamba Mungu anaendelea kuwaita vijana wengi. Na kwamba pale ambapo imani ni hai, wito husikika na kujibiwa kwa ukarimu.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.