Kifo cha Askofu Mfumbusa wa Jimbo la Kondoa! Salam za Rambirambi Kutoka Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC linasikitika kutangaza kifo cha Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, kilichotokea tarehe 14 Aprili 2026 Majira ya Saa 11:45 asubuhi kutokana na ugonjwa wa shambulio la moyo kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa, BMH iliyoko Jijini Dodoma alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya dharura. Askofu Mfumbusa anatarajiwa kuzikwa Jumatano tarehe 22 Aprili 2026 Jimboni Kondoa. Itakumbukwa kwamba, tarehe 9 Aprili 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV alikuwa amemteua Askofu Bernardin Francis Mfumbusa, Rais wa Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, “Pan African Episcopal Conference For Social Communication, CEPACS,” kuwa ni Mjumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasilianiano ya Jamii. Askofu Mfumbusa alichaguliwa kwa nafasi hii kunako mwezi Agosti 2025, huko Kigali nchini Rwanda na angemaliza uongozi wake mwaka 2028. Katika kipindi hiki cha uongozi wake amekazia sana umuhimu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii sanjari na mitandao ya kijamii, kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu mahalia Barani Afrika. Kwa hakika Kanisa limempoteza Askofu na mtaalam mbobezi wa Mawasiliano ya Jamii.
Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii katika nafsi ya Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii ametuma salam za rambirambi kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akikiri na kutambua mchango wa Hayati Askofu Mfumbusa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii na kwa namna ya pekee kwa mchango wake katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo iliyokuwa inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” kwa ajili ya Ulimwengu wa mawasiliano ya jamii. Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii linapenda kuiweka roho ya Hayati Askofu Mfumbusa katika huruma ya Mungu, ili Mwenyezi Mungu asili ya maisha, apende kumpokea Mtumishi wake Askofu Mfumbusa katika Ufalme wake wa mwanga wa milele na hatimaye, amkirimie amani katika ushirika na Baba wa milele. Amina. Wakati huo huo, Askofu Emmanuel Adetoyese BADEJO wa Jimbo Katoliki la Oyo, nchini Nigeria, Rais mstaafu wa Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, “Pan African Episcopal Conference For Social Communication, CEPACS,” anasema, amepokea habari za kifo cha Askofu Mfumbusa kwa mshtuko na kwamba, ni hivi karibuni tu walikuwa wakijadili kuhusu mchango wake katika kukuza na kudumisha mawasiliano ya jamii Barani Afrika na wala hakujua kwamba, Mwenyezi Mungu alikuwa anamtayarisha kwa ajili ya kwenda kushiriki maisha na uzima wa milele, kwa hakika Askofu Mfumbusa alikuwa Mwamba na Gwiji wa Mawasiliano ya Jamii. Askofu Emmanuel Adetoyese BADEJO ametumia nafasi hii kutoa salam zake za rambirambi kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Kondoa, Tanzania, Kamati ya Kudumu na Sekretarieti kuu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katokiki Afrika na Madagascar, SECAM, SIGNIS na UCAP wadau muhimu sana katika utume wa Mawasiliano Barani Afrika na kwamba, wafarijike kwa sala na salamu hizi za rambirambi.
Hayati Askofu Mfumbusa amekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya elimu na hasa katika taaluma ya mawasiliano ya jamii, aliyoitendea haki tangu mwaka 2002 hadi mwaka 2011 wakati akifundisha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT. Kwa hakika alikuwa ni: Mwalimu, Baba, Rafiki na Mlezi, wanasema wanafunzi wake aliowafundisha SAUT. Itakumbukwa kwamba, Hayati Askofu Bernardin Francis Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa, alizaliwa tarehe Mosi Aprili 1962 Jijini Arusha na ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 64 tangu alipozaliwa. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 14 Juni 1992 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Askofu Matthias Joseph Isuja, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma. Jimbo Katoliki la Dodoma likamtuma kujiendeleza kwa masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma na huko akajipatia Shahada ya Uzamili ya Mawasiliano ya Jamii, kunako Mwaka 1997. Baada ya Masomo yake alirejea tena Tanzania na kuendelea kufundisha kwenye Taasisi ya “Nyegezi Training Social Institute.” Baadaye alitumwa tena Roma kwenda kuendelea na masomo na hatimaye akajipatia Shahada ya Uzamivu katika Mawasiliano ya Jamii kutoka katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Cornell cha New York, Marekani. Akarejea tena nchini Tanzania kama Mhadhiri na kuteuliwa kuwa ni Mkuu wa Kitivo cha Sayansi Jamii, na baadaye akateuliwa pia kuwa ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma hadi alipoteuliwa kuwa Askofu kwanza wa Jimbo Katoliki la Kondoa.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 12 Machi 2011 akaanzisha Jimbo Katoliki la Kondoa na kumteuwa Askofu Bernardin Francis Mfumbusa kuwa Askofu wake wa kwanza, na hivyo kuwekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, aliyekuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 15 Mei 2011, akisaidiana na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi aliyekuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza pamoja na Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp., wa Jimbo Katoliki la Zanzibar. Kumbe Askofu Bernardin Francis Mfumbusa amefariki dunia akiwa amelitumia Kanisa kama Padre kwa Miaka 33 na kama Askofu mwenye dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa miaka 14. Anakumbukwa na watu wengi ndani na nje ya Kondoa katika ulinzi, utunzaji na uboreshaji wa mazingira nyumba ya wote, leo hii, Kondoa ni kijani kibichi, juhudi na kazi ya Baba Askofu Mfumbusa; akawa ni chombo cha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam. Aliwekeza sana katika sekta ya elimu, akiamini sana mchango wa elimu katika kuwakwamua watu kutoka katika umaskini, ujinga na maradhi; akawa ni mwanga wa imani, elimu na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na mwamini bora wa matumizi bora wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika mawasiliano ya jamii kama sehemu ya utekelezaji sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, uinjilishaji, elimu na ubunifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani ya Kondoa, Tanzania, Afrika na Ulimwengu katika ujumla wake. Kanisa limempoteza Askofu, wataalam wa tasnia ya mawasiliano wanasema wamempoteza mwanazuoni hayo yamesemwa na wanafunzi wake kutoka SAUT.
Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo!
Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton”. Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya, inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kum” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka.” Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbukumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kuitupa mkono dunia Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Maswali haya ni muhimu kwa waamini wote, ili kuweza kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo!
Wakati huo huo, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi anasema, Mwili wa Hayati Askofu Mfumbusa utapelekwa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo kuu la Dodoma, Jumanne tarehe 21 Aprili 2026 saa mbili asubuhi kwa ajili ya Misa Takatifu na Majira ya Saa 6: 00 Mchana mwili utapelekwa Jimboni Kondoa na baadaye kufuatiwa na Ibada ya Misa Takatifu itakayoanza majira ya Saa 10:00 Jioni sanjari na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kupata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho na kuuaga mwili wa Hayati Askofu Mfumbusa. Jumatano tarehe 22 Aprili majira ya Saa 4:00 Asubuhi itaanza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Askofu Bernardin Francis Mfumbusa.