Kard.Parolin:Chuo cha Kipapa cha Kanisa kinatoa njia za amani kwa ulimwengu
Vatican News
Katika mahojiano na Vatican News kuhusu kuadhimisha miaka 325 ya kuanzishwa kwa Chuo cha Kipapa cha Kanisa, Kardinali Pietro Parolin alisema Taasisi hiyo inaitwa leo hii kusaidia kupanga "njia thabiti za amani, zilizoundwa na kanuni,sheria na miundo inayohakikisha utulivu miongoni mwa mataifa, hasa katikati ya mgogoro wa sasa wa utaratibu wa kimataifa. Maoni ya Katibu Mkuu wa Vatican, alisema hayo wakati chuo kinampokea Papa Leo XIV, Jumatatu alasiri tarehe 27 Aprili 2026 katika Makao Makuu yake huko Uwanja wa Minerva jijini Roma kwa ziara yake ya kwanza huko tangu kuchaguliwa kwake.
Kuunda wanadiplomasia wa kipapa
Kardinali Parolin alielezea kuwa Chuo hicho kama Taasisi inayounganisha historia na urejesho, akibainisha kuwa ingawa ni sehemu ya Sekretarieti ya Vatican, pia imepewa jukumu la kuwaandaa wale wanaomwakilisha Mrithi wa Petro ulimwenguni kote. Wanadiplomasia wa Kipapa lazima wawe na uwezo wa kutathmini hali kwa uwazi, kushiriki katika mazungumzo, na kutambua mahitaji ya watu na mataifa. "Wanahitaji ari hiyo ya kimisionari inayowafanya kuwa mashuhuda halisi na walioandaliwa vizuri kwa umakini wa Papa kwa Makanisa mahalia na Watu wa Mungu," alisema.
Zaidi ya nguvu rahisi na laini
Akitafakari utume wa Chuo hicho, Kardinali Parolin alibainisha kuwa kazi yake ya elimu kimsingi ni ya kikanisa, kwani hatua ya kidiplomasia ya Vatican inaenea zaidi ya nguvu rahisi laini. Chuo, huwaandaa wanadiplomasia wa siku zijazo kutafsiri maendeleo ya kimataifa kwa kuzingatia mafundisho ya kijamii ya Kanisa na kushirikisha miundo ya jumuiya ya kimataifa kwa utambuzi mzuri. Wanafunzi huundwa si tu katika ubora wa kitaaluma, bali pia katika fadhila za kikuhani kama vile kusikiliza, mazungumzo, unyenyekevu, na ukaribu na wengine.
Mageuzi chini ya Papa Francisko
Kardinali Parolin pia alikumbuka mageuzi yaliyofanywa na Papa Francisko katika Chuo hicho kupitia Barua yake ya Mkono “ Il Ministero Petrino, akielezea kama uboreshaji muhimu wa dhamira na muundo wa taasisi hiyo. Alibainisha kuwa Papa Francisko aliwahi kuwaelezea wanadiplomasia wa Vatican kama "mapadre wakiwa na masanduku mkononi," akisisitiza tabia ya kichungaji na uinjilishaji wa huduma yao. Chini ya mabadiliko hayo, Chuo kimeundwa upya kama Taasisi ya Elimu ya Juu katika Sayansi ya Kidiplomasia na sasa kinatoa shahada za Leseni na Uzamivu.
Akijibu mgogoro wa kidiplomasia
Akizungumzia hali ya sasa ya kidiplomasia ya kimataifa, Kardinali Parolin alionesha wasiwasi ulioenea kuhusu uwezo mdogo wa diplomasia wa kuzuia au kutatua migogoro. Alisema jibu la Chuo hicho ni kutoa malezi mapya katika sayansi ya kidiplomasia, ikiwa ni pamoja na masomo ya kisheria, kihistoria, kisiasa, na kiuchumi, yaliyounganishwa na taaluma za kikanisa na utume wa Kanisa la kuinjilisha. Hata hivyo, alisisitiza kwamba maandalizi ya kiufundi pekee hayatoshi. "Mwanadiplomasia anaitwa kwanza kabisa kutoa ushuhuda na kisha tu kujadiliana," alisema. Kardinali Parolin alihitimisha akisema kuwa mgogoro wa utaratibu wa kimataifa uliooneshwa na matumizi mapya ya nguvu na kupuuza sheria za Kimataifa unaweza kushughulikiwa kwa "kuchora njia halisi za amani tu. Hilo ni jukumu lililokabidhiwa leo katika Chuo cha Kipapa cha Kanisa, miaka 325 baada ya kuanzishwa kwake.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here