Tafuta

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 25 Aprili 2026, anatarajiwa kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 17 kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 25 Aprili 2026, anatarajiwa kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 17 kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana.  

Historia ya Maisha na Wito wa Gabriel Masangu Mwandu, Jimbo Kuu la Tabora, Tanzania

Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo; ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu katika maisha ya Sala, Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara.

Na Gabriel Masangu Mwandu, - Roma.

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Mashemasi ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha ya wakfu! Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 25 Aprili 2026, anatarajiwa kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 17 kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Mashemasi wapya wanatakiwa kujenga na kudumisha uhusiano na mafungamano ya dhati kabisa na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na huduma makini kwa watu wa Mungu. Watambue kwamba urafiki wao na Kristo Yesu, unawawezesha kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huduma kwa maskini. Daraja Takatifu ya Ushemasi ni Sakramenti ya Kristo Yesu inayomtambulisha kama mhudumu ambaye alikuja “kutumika na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” (Mk 10:45).

Waseminari kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma
Waseminari kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma   (Vatican Media)

Kimsingi, wabatizwa wote wanapaswa kumfuasa Kristo Yesu, aliye mpole na mnyenyekevu wa moyo; Mtumishi wa Mungu na binadamu. Mashemasi wajenge mahusiano ya pekee na Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu ili waendelee kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na kujifunza kutoka kwake, kupenda na kusadaka maisha kwa ajili ya Mungu na huduma kwa jirani. Urafiki, uhusiano na mafungamano thabiti na Kristo Yesu, yatauwezesha utume wao kuwa na mafanikio makubwa. Upendo kwa Kristo Yesu unafumbata pia upendo kwa Kanisa lake kwa njia ya utii. Mimi Gabriel Masangu Mwandu mtoto wa Baba Mwandu Buchambi na Mama Sado Luhende ambaye ametangulia mbele za haki mwaka 2016. Ni mtoto wa saba kati ya watoto saba; Kaka wanne na dada wawili. Nilizaliwa katika kijiji cha Mwabalaturu wilayani Igunga, Tabora. Ni mwana Parokia ya Mtakatifu Margaret Maria Alakok, Igunga Jimbo kuu Katoliki la Tabora. Nilisoma Shule ya Msingi katika kijiji cha Mwabalaturu mwaka 2002 hadi 2008 na kufaulu kujiunga na Sekondari ya Itunduru, wilayani Igunga kwa muda mfupi tu na baadaye kuomba kupokelewa katika Seminari ndogo ya Mt. Karoli Borromeo, Jimbo Kuu katoliki la Tabora kuanzia mwaka 2011 hadi 2014 na kwa masomo ya kidado cha tano na cha sita katika Sekondari ya Ufundi Moshi (Moshi Technical Secondary School), Moshi Kilimanjaro. Baada ya kuhitimu nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kambi ya Mafinga no. 841KJ, Iringa kwa mjibu wa sheria. Tarehe 10 Oktoba 2010 nilijiunga na Nyumba ya Malezi ya Askofu Mkuu Mario Epifanio Abdallah Mgurunde jimbo kuu Katoliki Tabora. Mwaka 2018-2021 nilianza Elimu ya Falsafa na majiundo katika Seminari Kuu ya Malkia wa Malaika Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi. Mnamo mwezi Juni 2021 Jimbo Kuu Katoliki la Tabora chini Baba Askofu mkuu mstaafu Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka lilinituma kusoma Taalimungu katika Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana hadi sasa naendelea na masomo ya uzamili katika Maandiko Matakatifu (Biblical Theology) kwa muda wa miaka 3 nikiwa bado katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma.

Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana
Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

MAISHA YA IMANI NA WITO Mwaka 2009 nilipata Sakramenti ya Ubatizo, Komunyo na Kipaimara kwenye Kigango cha Itunduru Parokia ya Igunga. Ninayo furaha kubwa kwa Mwenyezi Mungu kwa mambo makuu aliyonitendea katika maisha yangu hasa kwa kuendelea kuniongoza katika safari ya malezi na majiundo ya Upadre. Safari yangu ya Ukristu ilianza nikiwa Shule ya msingi katika mazingira ya Kijiji nilichozaliwa ambacho watu wengi kwa asilimia kubwa zaidi si wakristu. Hatua ya awali kabisa nilipata ujuzi wa kwanza wa kujifunza Imani Katoliki katika kikao cha kwanza cha sala kilichoongozwa na Katekista shuleni. Na katika juhudi mbalimbali ya kujifunza shuleni nilipata bahati ya nyenzo za mafundisho ya Imani kama vile Biblia, Katekismu Ya Kanisa Katoliki vilevile na kwa kupitia nyenzo za mawasiliano kama Redio Maria na Redio Faraja. Hivi vilikuwa nyenzo muhimu sana zilizonisaidia kukua kiimani. Kutokana na changamoto za kimazingira niliendelea kujitahidi katika kujifunza shuleni na kuvuta subira huku nikiwa na tamanio kubwa kwamba wakati utafika siku moja lazima niwe mkristu. Baada ya kufaulu kujiuunga na shule ya sekondari, kwangu ilikuwa ni nafasi na fursa ya pekee ya kuwa mkristu na kuuishi ukristu. Nilipojiunga na sekondari nilipata fursa ya kupokea mafundisho kwa muda mfupi sana na hivyo kubatizwa na kupata komunyo ya kwanza. Nilibatizwa na kupata kipaimara kutoka kwa Wamisionari wa Afrika (White Fathers) katika Parokia ya Igunga. Baada ya hatua hii muhimu, ndipo nilipoanza kusikia kiu ya kumtumikia Mungu na kutangaza Neno lake na nikajiunga kwenye malezi na masomo seminari ndogo. Mungu ambaye ananiongoza katika safari ya wito wangu. Nawashukuru sana makatekista, waamini na wale wote walionisaidia katika kukua kiimani. Mara baada ya hatua hii muhimu nilipata wito wa Upadre ili kumtumikia Mungu katika wito wa Daraja Takatifu yaa Upadre. Nawashukru sana wote walionisaidia katika kukua kiroho na kiimani ambao wameacha alama ya matumaini.

Ushemasi ni siku pia ya utamadunisho wa imani
Ushemasi ni siku pia ya utamadunisho wa imani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

DARAJA YA USHEMASI 25 Aprili 2026 Mwaka huu ninayo furaha kubwa sana katika hatua nyingine kuelekea kupewa Daraja takatifu ya Ushemasi tarehe 25 Aprili 2026 katika Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Mwadhama Kardinali Luis AntonioTagle, Mwenyekiti mwenza “Pro-Prefect” wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambayo itafanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Mjini Vatican. Tunamshukuru Mungu kwa baraka kubwa ya wito na kwa kupitia mafungo ya Kiroho ya maandalizi ya kupokea daraja ya Ushemasi yaliyofanyika tarehe 27 March hadi tarehe 1 Aprili 2026 katika Seminari yetu (Pontificio Collegio Urbano “De Propaganda Fide”) ambayo ilihitimishwa kwa masifu ya jioni kwa kukiri Imani, kisha kuweka viapo vya uaminifu (Professione di Fede, Declaratio e Giuramento alla fedeltà). Tuko waseminari 17 ambao tunataraji kupata Daraja takatifu ya Ushemasi. 6 kati ya hao ni kutoka Shirikisho la Maaraza la Maaskofu Afrika Mashariki na Kati AMECEA (The Association of Member of Episcopal Conferences in Eastern Africa: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1; Sudan Kongwe 2 na Sudan ya Kusini 1; Uganda 4); Ghana 2; Nigeria 2; Benin 1; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 1 na Cameroon 1. Na katika Bara la Asia wako 4, India 2, Pakistani 1 na Timor ya Mashariki 1.   Nawashukuru sana wazazi wangu na Familia yangu ambao waliniimarisha katika malezi. Namshukru sana Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora mapadri, watawa na walei, wafadhili na wote wenye mapenzi mema ambao ambao wamekuwa msaada katika safari ya wito wangu. Nawashukuru sana Mapadri ambao wamenilea katika safari yangu ya wito katika Parokia yangu na Seminarini na wengine ambao wametangulia mbele za haki, Mwenyezi Mungu awajalie pumziko la Amani. Leo, ninapojitayarisha kwa daraja ya Ushemasi, ni wakati muhimu sana kwangu kutafakari na kusoma upya historia ya maisha yangu kwa njia ya msaada wa Mungu. Tafakari hii inakuja kama tendo la shukrani na utambuzi: shukrani kwa yale ambayo Bwana ametenda na anaendelea kutenda katika maisha yangu, na utambuzi wa wajibu unaokuja kwa kuitikia wito wake.

Ibada ya Misa Takatifu ya Daraja Takatifu ya Ushemasi
Ibada ya Misa Takatifu ya Daraja Takatifu ya Ushemasi   (@VATICAN MEDIA)

Fumbo la Wito Mtakatifu: Mungu ndiye anayeanzisha wito yeye ni chemchemi na chimbuko la miito, siyo sisi tunaojichagua wala kujiita bali ni Mungu anayetuita. Kama asemavyo Bwana kupitia Nabii Yeremia: “Kabla sijakuumba tumboni mwa mama yako, nalikujua” (Yer 1,5). Neno hili linafunua ukweli wa kina: maisha yetu si matokeo ya bahati. Mungu ndiyo chanzo cha miito. Mara nyingi katika wito kuna nyakati za kutaka kuona ishara za wazi, si rahisi lakini Mungu pia hunena katika ukimya, katika maisha ya kila siku, na katika msukumo wa ndani wa moyo. Ni kumfuata Kristo yaani kuingia katika uhusiano hai unaogusa maisha yote kwa kujikabidhi kwake mwili na roho kwa ajili ya kumtumikia. Katika nyakati za hofu na mashaka, Mungu hutuongoza na kututhibitishia kuwa neema yake yanitosha. Ushemasi: sura ya Kristo Mtumishi: Daraja la Ushemasi ni hatua muhimu sana ambayo ni kufananishwa kwa kweli na Kristo Mtumishi. Katika Matendo ya Mitume tunasoma: “Wakachagua watu saba, waliojaa Roho Mtakatifu na hekima” (Mdo 6,3). Tukio hili linaonyesha mwanzo wa huduma ya Ushemasi. 3 Shemasi anaitwa kutumikia: Neno la Mungu, Liturujia, Upendo. Kristo mwenyewe asema: “Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika” (Mk 10,45). Huu ndiyo msingi na moyo wa huduma ya Ushemasi. Msingi wa mafundisho kuhusu Ushemasi: Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafundisha kuwa Ushemasi ni sehemu ya Sakramenti ya Daraja (n. 1569). Mtaguso wa Pili wa Vatican, katika Lumen gentium, 29 inaelezea thamani halisi ya Ushemasi na kusisitiza nafasi yake katika maisha na utume ya Kanisa hasa katika huduma (Diaconia). Hitimisho Daraja ya Ushemasi si mwisho, bali mwanzo. Ni mwanzo wa huduma iliyo ya ndani zaidi, kamili zaidi, na ya kweli zaidi. Kwa imani, narudia tena “mimi hapa” Bwana, chukua maisha yangu uyafanye chombo cha upendo wako. Amina. Mimi na wenzangu tukiwa tunajiandaa kupewa Daraja ya Ushemasi tunaendelea kuomba msaada wa sala Mwenyezi Mungu atuongoze vyema kumtumikia kwa uaminifu, upendo na furaha tele.  “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” (Flp 4,13.) Ni mimi Gabriel Masangu Mwandu, Kutoka Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.

Gabriel Mwandu
24 Aprili 2026, 15:47