Tafuta

Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa katika tafakari ya kipindi cha Kwaresima. Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa katika tafakari ya kipindi cha Kwaresima.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari ya Kwaresima:Mamlaka yetu hayatokani na jukumu letu ni maisha yanayokubali nguvu ya upendo

Katika Tafakari ya III ya Kwaresima Machi 20,katika Ukumbi wa Paulo VI,mbele ya Baba Mtakatifu Leo XIV,Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa amejikita na mada ya uinjilishaji, kwa kuzingatia maisha ya Mtakatifu Francis,wa Assisi:"Kumtangaza Kristo kwa nafasi ya ukuu au udhibiti ina hatari ya kusaliti Injili yenyewe.Injili haitangazwi ili kushinda bali kukutana."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa, Padre Roberto Pasolini, alitoa tafakari yake ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima kuhusu mada: Kutangaza Injili kwa Kila Kiumbe," Ijumaa tarehe 20 Machi 2026, katika Ukumbi wa Paulo VI, mbele ya Baba Mtakatifu Leo XIV. Kwa njia hiyo alisisitiza kuwa kujibeba kwa unyenyekevu, kukubali kutegemea hisia za wengine, kuandaa mazingira kwa ajili ya kukutana na Yesu, si kutoa majibu bali kuuliza maswali, kuacha nafasi ya mazungumzo, tayari kupokea mema ya wengine katika "nguvu ya upendo." Ni safari ngumu na yenye kutia moyo, inayozingatia uinjilishaji kuanzia na uzoefu wa kiroho wa Mtakatifu Francis wa Assisi.

Onyo kutumia mambo ya Mungu kutafuta kibali au kutambuliwa 

Kwa njia hiyo kutangazwa kwa Injili, Padre Pasolin alisema , hakupaswi kupendekezwa kutoka nafasi ya ukuu au udhibiti, kwa sababu hii ingehatarisha kuisaliti. Mamlaka yetu hayatokani na jukumu, bali na maisha yanayokumbatia nguvu hii ya upendo. Hili ndilo Francis alielewa alipowaita watawa wenzake kuwa "wadogo:" kuwapatia sio cheo, bali njia halisi ya kuwa duniani. Ni udogo huu, unyenyekevu huu ulioishi, ndio hufanya tangazo la Injili liwe na matunda. Utume, utimilifu wa uongofu na udugu, hutokana na "shauku ya kushiriki na wengine uzoefu na tangazo la Injili," lakini kila kitu hutoka katika Neno. "Mtu hawezi kusema kweli, juu ya kile ambacho hakijaota mizizi maishani mwake. Hatuwezi kubaki katika ulinzi bali uvumilivu unahitajika: kuthamini kile tulichokiona na kukisikia, kukiacha kikomae katika maombi, hadi kiwe uzima hata kabla hakijawa neno. Lazima kujiadhari  na jaribu la kutumia mambo ya Mungu kutafuta kibali au kutambuliwa. Lazima tulinde kile kilicho cha thamani, tukiache kikomae, kisha tukibadilishe kuwa ushuhuda.

Kristo si habari ya kupitishwa ni fumbo linalokaa ndani ya mwanadamu

Kristo si habari ya kupitishwa, bali ni fumbo linalokaa ndani ya wanadamu na linalodai kutambuliwa ili liweze kujitokeza katika maisha. Injili haiwasilishwi kama habari rahisi; hutolewa kama maisha ambayo huchukua umbo polepole. Padre Pasolini katika tafakari hiyo alitumia mfano unaofaa kuelezea jinsi uwepo wa Mungu katika moyo wa mwanadamu unavyobadilisha maisha yetu na mahusiano yetu na wengine. Ni uzoefu wa mama: kwanza humbeba mtoto wake ndani yake, humpatia muda wa kukua, na kisha humzaa tu. Vivyo hivyo kuhusu imani. Kwanza Kristo huchukua nafasi ndani yetu, kimya kimya, katika maombi, katika chaguzi zetu za kila siku. Na hapo ndipo anaweza kuonekana kwa nje, katika ishara zetu na jinsi tunavyohusiana na wengine. Tukiondoka bila uhakika, tukijiandaa kwa ajili ya mkutano ambao Yesu mwenyewe anatamani. "Sisi sio kitovu cha ujumbe, bali uso wa Mungu, ambao tunaweza, kwa urahisi, kuufanya uwe wazi na wa kufikika, alisisitiza Padre Pasolini.

Kutambua thamani ya wengine

Harakati iliyo wazi inaibuka: kujiruhusu kukaribishwa na kisha kutangazwa, tukitambua thamani ya wengine. Hii inamaanisha kuchukua ubinadamu wao kwa uzito, uwezo wao wa mema, upatikanaji wao." Ili kufanya hivyo kunahitaji umaskini halisi, kujiwasilisha bila kuwa na kila kitu na bila kudhibiti kila kitu, kukubali kutegemea wema na usikivu wa wengine, na kutambua kwamba ufalme wa Mungu tayari upo, kwa njia iliyofichwa, hata katika maisha ya wale ambao bado hawajaujua. Kuinjilisha, kwa mtazamo huo, kunamaanisha kuwaambia wengine, hata bila kusema chochote, kwamba ni vizuri wapo, na maisha yao yana thamani. Sio tu kuwathibitisha katika kile ambacho walicho nacho, bali kuwasindikiza katika kutambua, kidogo kidogo, ukweli na uzuri walio nao ndani, bila kukimbilia kuwarudisha kwenye mawazo yetu.

Kanisa halikui kwa propaganda ya dini, bali mvuto na ushuhuda

Padre Pasolini alikumbusha maneno ya Papa Francisko kuhusu uinjilishaji  kwa sababu "Kanisa halikui kwa kufanya propaganda ya  dini, bali kwa mvuto, wakati uwepo wetu hauzuii uhuru wa wengine, bali huamsha upya. Kutambua uwepo wa Mungu katika mwingine, kumkaribia kwa heshima: haya ndiyo masharti muhimu ya mazungumzo. "Sio tu suala la kujua jinsi ya kuzungumza, lakini zaidi ya yote kujua jinsi ya kusikiliza. Na, wakati utakapofika, kujua jinsi ya kuwasilisha maneno ya matumaini yanayotoka kwa Mungu. Si kutoa majibu ya haraka bali kujua jinsi ya kusubiri maswali kwa sababu ni Mungu ambaye "anakamilisha ushuhuda wetu mbaya." Padre Pasolini alikumbuka tukio la majambazi walioishi karibu na watawa katika mtaa wa juu ya Kaburi Takatifu kuwa, kuishi pamoja kwa shida kulimpelekea Francis kupata mwanga wa kweli: kuwapa mkate na divai na kisha kumtangaza Mungu.

Kutangaza Injili kunaamini kuyakaribia maisha ya wengine kwa heshima

Ni kwa njia hiyo tu, majambazi wanaweza kubadilisha maisha yao kwa sababu wanapata "ukaribisho, heshima, na uaminifu.  Kinachoandaa mkutano huo kweli ni safari tunayofanya pamoja, ambayo inawaongoza watu kujiuliza. "Maswali hayo, ni mahali ambapo Mungu yupo na anafanya kazi." Maneno yanapoibuka kutokana na uzoefu halisi, yanawafikia wengine. Yanapobaki kuwa ya kufikirika na yasiyo na utu, hayamshawishi mtu yeyote. Hata sisi tunaoyazungumza. Kutangaza Injili kunamaanisha kuyakaribia maisha ya wengine kwa heshima na kutambua kwamba, katika ugumu wa maisha yao, tayari kuna utafutaji wa maana, wema, na ukweli.

Mkutano wa Mtakatifu Francis na Sultani

Tukio muhimu katika maisha ya Mtakatifu Francis wa Assisi pia  lilikuwa ni kukutana kwake na Sultani wa Misri, Al-Malik al-Kamil, wakati wa Vita vya Tano vya Msalaba. Kwa mtazamo wa kwanza," Padre Pasolini alieleza kuwa,  hakuna kinachoonekana kutokea: Sultani hakubadilika,na Francis hakupata imani aliyoitafuta." Lakini kukutana kwao ilikuwa ni chanzo cha mazungumzo na ukuaji. Francis anajionesha kama "mnyenyekevu, maskini, asiye na ulinzi. Hakutafuta  kulazimisha mawazo yake mwenyewe; alijionyesha kwa mwingine kama alivyo." Sultani alitambua ndani yake umaskini na unyenyekevu wa Kristo. Hakujisikia kushambuliwa au kuhojiwa, na kwa sababu hiyo alifunguka. Muujiza ni kwamba wanaume wawili, katikati ya vita, waligundua ubinadamu wa kila mmoja na kuachana kwa amani.

Injili haitangazwi ili kushinda,bali kukutana

Injili haitangazwi ili kushinda, bali kukutana. Mwingine si shabaha ya kufikiwa, bali ni kizingiti ambacho tunasimama mbele yake, tukisubiri kukaribishwa. Kuinjilisha haimaanishi kuunganisha umbali kwa gharama yoyote, bali kuuvuka bila kuufuta, kuhifadhi tofauti kama nafasi ambayo Mungu anaendelea kutenda katika moyo wa kila mtu. Kukutana na mwingine kunamaanisha si kutoa tu bali pia kupokea. Katika mtazamo huo  wa uwazi mkubwa kwa mwingine,"Francis aliwashauri watawa wake kubaki watiifu mbele ya watu wa imani tofauti. Utiifu kwa mujibu wa Mhubiri Padre Pasolini alifafanua, haimaanishi kupoteza utambulisho wa mtu, wala kujisalimisha kwa mwingine kutokana na udhaifu.

Mungu hakujilazimisha kwa mwanadamu,alimpatia nafasi

Hili ni chaguo huru la heshima na mazungumzo. Inamaanisha kutambua kwamba mwingine si eneo la kushinda, bali ni maisha ya kukutana, kuheshimiwa, na kukaribishwa.” Wale wanaokubali mbinu hii huwaruhusu wengine kufunguka, kujitokeza, na kujionesha jinsi walivyo. Mbinu hii, yenyewe, ni kitendo kikubwa cha  uinjilishaji. "Mungu hakujilazimisha kwa mwanadamu, bali alimpatia nafasi. Hakujilinda kwa wivu ukuu wake mwenyewe bali aliuacha kandoni ili mwingine aweze kuupokea na kuishi. Wakati kuna kukubalika, wema hujitokeza, wema huo,ambapo, kwa njia iliyofichwa, fumbo la Kristo tayari lipo, alihitimisha Padre Pasolini.

TAFAKARI PADRE PASOLINI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.

20 Machi 2026, 12:00