Mkataba wa Vyombo vya Habari vya Vatican na Vituo 10 vya Radio-Poland
Na Wojciech Rogacin - Vatican.
Baraza la Kipapa la Mawasiliano limesaini makubaliano ya ushirikiano na vituo kumi vya radio vya kikanda nchini Poland. Vituo hivyo kwa pamoja vinawafikia mamilioni ya wasikilizaji na vinatamani kutoa taarifa kuhusu Papa na Kiti Kitakatifu. Wakurugenzi wao walikutana na Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya Katekesi yake siku ya Jumatano tarehe 18 Machi 2026. Wakuu hawa saba wa vituo vya radio vya kikanda vya Poland kutoka Lublin, Kraków, Gdańsk, Opole, Poznań, Wrocław, na Łódź. Vituo vinne vya radio vya ziada kutoka Rzeszów, Kielce, na Białystok vitasaini makubaliano kwa njia ya mawasiliano.
Salamu na Zawadi kwa Papa Leo XIV
Walipofika Roma, wageni wa Poland walihudhuria Katekesi ya Papa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na baadaye wakamsalimia Papa Leo XIV. Hawa walisindikizwa na Dk. Andrea Tornielli, mkurugenzi Mkuu wa uhariri wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano; Massimiliano Menichetti, naibu mkurugenzi wa uhariri wa Vyombo vya habari vya Vatican, Mhusika Mkuu wa Vatican Radio-Vatican News; na Padre Paweł Rytel-Andrianik, mkuu Idhaa ya Kipoland ya Radio Vatican -Vatican News na Osservatore Romano.
Wakurugenzi wa radio wa Poland walimpatia Papa sanamu ya mashua ndogo ya fedha iliyowekwa kwenye msingi uliotengenezwa kwa kaharabu, ambayo imekusanywa kwa karne nyingi kwenye ufuko wa Bahari ya Baltiki. Zawadi hiyo iliambatana na maneno ya Kilatini: "Kwa heshima kubwa na umoja wa kiroho, tunampatia Baba Mtakatifu zawadi hii kama ishara ya shukrani na umoja kwa niaba ya jamii zinazounda ofisi za utangazaji za kikanda za Radio ya Kipolandi."
![]()
Zawadi aliyopewa Papa Leo XIV kutoka kwa wakurugenzi wa Radio za Poland (@Vatican Media)
Ujumbe wa Matumaini Wakati Ulimwengu Unateseka Vita
Baadaye, makubaliano yalitiwa saini katika Baraza la Kipapa la Mawasiliano na Padre Lucio Adrian Ruiz, Katibu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza hili Dk. Paolo Ruffini. "Huu ni wakati muhimu, kwa sababu sisi sote, kama wataalamu wa mawasiliano, tuna jukumu kubwa kwa ulimwengu: kusambaza ukweli na kupanda matumaini mioyoni," alisema Padre Ruiz. "Kwetu sisi, ni muhimu kuunganisha mtandao," alisema Dk Andrea Tornielli, Mwariri Mkuu wa Taariri ya Baraza la Kipapa la Mawasiliano "na kufikia makubaliano na vyombo vya habari vya Kikatoliki na visivyo vya Kikatoliki vinavyopenda kutoa habari kuhusu Papa katika lugha mbalimbali. Tayari leo hii, watangazaji na vyombo vya habari 1,500 ulimwenguni kote vinatoa habari za Vatican.
Shukrani kwa makubaliano haya, tunapanua fursa zetu za kuwa na washirika wa uchapishaji katika nchi mbalimbali, kuboresha utoaji wetu wa habari na wakati huo huo kupambana na jambo la habari za uongo.” Haya yalisemwa na Massimiliano Menichetti akiunga hisia hiyo, kwa kuongeza: “Makubaliano na vituo vya radio vya umma vya Poland ni hatua zaidi katika kujenga umoja wa mawasiliano halisi na ya kidugu. Katika enzi hii ambapo pia tunakabiliwa na changamoto za Akili Unde (AI), kuunganisha nguvu ya sauti kupitia radio kunatukumbusha kwamba Akili unde haiwezi kuwepo bila watu.”
![]()
Wakati wa kutia saini Mkataba katika Ukumbi wa Marconi wa Jumba la Pio.
Mamilioni ya wasikilizaji wapya
Kwa upande wake, Mirosław Kasprzak, mkurugenzi wa Radio Lublin nchini Poland, alisema kwamba kwa vituo vya radio vya kikanda nchini Poland, ushirikiano na vyombo vya habari vya Vatican unamaanisha kutimiza dhamira ya vyombo vya habari vya umma. Aliongeza kuwa maudhui ya vituo vya radio vya kikanda nchini Poland yanafikia karibu wasikilizaji milioni 60 wanaoweza kuzungumza Kipoland, takriban milioni 37 ndani ya nchi na karibu milioni 20 nje ya nchi. "Tunatumaini kwamba mfano wetu utahimiza sehemu zingine za lugha za Radio Vatican-Vatican, Vatican News kusaini makubaliano kama hayo," rais wa kituo hicho aliongeza. Mwaka mmoja uliopita, timu tano za wahariri wa Kipoland zilisaini makubaliano kama hayo. Mwaka huu, idadi ya makubaliano yaliyosainiwa imeongezeka maradufu, ikionyesha athari chanya za ushirikiano huo.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.