Tafuta

2026.03.18 Kardinali Michael Czerny katika Mkutano wa XIV wa CEAMA. 2026.03.18 Kardinali Michael Czerny katika Mkutano wa XIV wa CEAMA. 

Kard.Czern:Amazonia inatoa njia mpya ya utunzaji wa uumbaji

Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu,katika mahubiri yake katika Misa siku ya Jumanne,Machi 17,huko Bogotá,wakati wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Mkutano wa Kanisa la Amazonia,alitoa wito wa ubadilishaji wa kichungaji,ikolojia na sinodi."Kutembea pamoja na watu wa Asilia kunasaidia Kanisa kuelewa kuwa utunzaji wa Nyumba Yetu ya Pamoja,si kazi ya kiufundi au kisiasa ni uongofu wa kiroho."

Vatican News

Kanisa linaona katika Amazonia udhihirisho wa uzuri na udhaifu wa kazi ya Mungu. Hii ni mojawapo ya dhana zilizotolewa na Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu, katika mahubiri yake katika Misa ya Utunzaji wa Uumbaji  tarehe 17 Machi 2026 iliyoadhimishwa huko Bogotá wakati wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Mkutano wa Kanisa la Amazoni (CEAMA).

Sherehe hiyo ilifanyika katika makao makuu ya Baraza la Maaskofu la Amerika Kusini na Karibea (CELAM) na kuwakutanisha Makardinali, maaskofu, makuhani, wanaume na wanawake watawa, watu wa kawaida, na wawakilishi wa watu wa Amazonia wanaoshiriki katika Mkutano huo. Mwanzoni mwa mahubiri yake, Kardinali alisisitiza kwamba wakati huu wa kikanisa si mwanzo tu wa mkutano wa kufanya kazi, bali ni tendo la imani na utambuzi, ambapo Kanisa hukusanyika kumsikiliza Roho Mtakatifu na kutembea pamoja katika njia ya sinodi.

Kristo, Kitovu cha Uumbaji Wote

Akitafakari masomo ya kiliturujia, hasa wimbo wa Kikristo kutoka kwa Barua kwa Wakolosai, Kardinali alikumbuka kwamba Kristo ndiye kitovu cha uumbaji wote. "Vitu vyote viliumbwa na Kristo," alisema, "vitu vyote viko ndani yake, na vitu vyote vimepatanishwa katika Yeye." Kutoka katika mtazamo huu, alielezea kwamba uumbaji hauwezi kuonekana tu kama rasilimali inayopatikana kwa wanadamu, bali kama kazi ya upendo wa Mungu, inayoungwa mkono na Kristo, na iliyokusudiwa kutimizwa katika Roho Mtakatifu. Akirejea Amazonia alisisitiza kwamba Kanisa linahisi jukumu maalum kuelekea eneo hili, si tu kwa sababu ya umuhimu wake wa kiikolojia.

Mtazamo wa Tafakari kuhusu Uumbaji

Kardinali Czerny pia alitoa wito wa mtazamo mpya wa tafakari kuhusu ulimwengu. Kwa maana hiiyo alitambua kwamba watu wa Amazonia wanatoa ushuhuda wa thamani kwa ulimwengu, wakiishi uhusiano na ardhi, maji, na msitu unaoonyeshwa kwa heshima na usawa. Kutembea pamoja na watu hawa—alisisitiza—kunasaidia Kanisa kuelewa kwamba kutunza Nyumba yetu ya Pamoja si kazi ya kiufundi au kisiasa tu, bali ni usemi wa uongofu wa kiroho.

Yesu yuko kwenye mashua katikati ya dhoruba

Akitafakari simulizi la Injili la Yesu akituliza dhoruba, Mkuu wa Baraza la Kipapa la Kukuza Maendeleo Fungamani ya Binadamu alilinganisha mandhari ya Injili na migogoro inayoikabili sayari ya leo. Dhoruba zinazopiga Nyumba Yetu ya Pamoja, kama vile mgogoro wa hali ya hewa, upotevu wa bayoanuwai, au vitisho kwa maeneo na jamii, zinaweza kusababisha hofu na kutokuwa na uhakika. Hata hivyo, alikumbuka, Yesu yupo kwenye mtumbwi. "Hata kama anaonekana amelala, hayupo. Uwepo wake ni dhamana kwamba historia haitaachwa kwenye machafuko." Uhakika huu, aliongeza, unatualika kufanya upya matumaini na kujitolea kwa Kikristo katika kukabiliana na changamoto za ikolojia na kijamii za wakati wetu.

Uongofu wa Kichungaji, Kiikolojia, na Sinodi

Wakati wa tafakari yake, Kardinali alisisitiza kwamba CEAMA ni tunda halisi la safari iliyoanzishwa na Sinodi ya 2019 huko Amazonia, usemi wa Kanisa linalotaka kutembea pamoja: maaskofu, watu waliowekwa wakfu, walei, na watu wa kiasili. Katika muktadha huu, Kardinali alikumbusha kwamba utume wa Kanisa katika Amazon unahitaji maendeleo katika nyanja tatu za msingi: uongofu wa kichungaji, ili jamii zizidi kuwa za kimisionari; uongofu wa kiikolojia, kuunganisha utunzaji wa uumbaji katika mambo ya kiroho na maamuzi halisi; na uongofu wa kisinodi, ili kuendelea kujifunza kumsikiliza Roho Mtakatifu anayezungumza kupitia Watu wote wa Mungu.

"Kila Kitu Kimeunganishwa" katika Kristo

Katika mahubiri yake, Kardinali pia alikumbuka waraka wa Papa Francisko Laudato Si', unaosema kwamba "kila kitu kimeunganishwa." Ufahamu huu wa kiikolojia, alielezea, unapata utimilifu wake wa kitaalimungu katika imani ya Kikristo kwamba uumbaji hupata umoja wake katika Kristo. Mwanzoni mwa Mkutano, Czerny aliwaalika washiriki kumwomba Bwana zawadi tatu: kutafakari kutambua uwepo wa Mungu katika Uumbaji; utambuzi wa kufanya maamuzi unaoongozwa na Roho Mtakatifu; na ujasiri wa kimisionari wa kutetea uhai, watu, na Nyumba yetu ya Pamoja. Hatimaye, alikabidhi safari ya Mkutano kwa maombezi ya Mama Yetu wa Aparecida na Mama Yetu wa Guadalupe, ili waweze kuongozana na Kanisa la Amazonia katika utume wake. Kwa sherehe ya Ekaristi, CEAMA inaanza wakati mpya wa kutafakari, ushirika, na utambuzi katika huduma ya Amazonia, watu wake, na utunzaji wa Nyumba yetu ya Pamoja.

KARD.CZERNY

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.

18 Machi 2026, 18:30